Friday 19 August 2022

MKOPAJI ANATAKIWA KUDAI FIDIA IWAPO BENKI IMEUZA NYUMBA YAKE BEI NDOGO.

 



BASHIR. YAKUB, WAKILI. -

Ni kosa benki au taasisi yoyote ya fedha kuuza nyumba, kiwanja ama shamba la mkopaji aliyeshindwa kulipa mkopo bei ndogo sana kuliko thamani ya soko..

Kifungu cha 133(1) cha Sheria ya Ardhi, Sura ya 113 kinalazimisha taasisi ya fedha kutafuta bei nzuri inayolingana na thamani ya ardhi inayouzwa. 

Msimamo huu pia ni wa mahakama ya rufaa katika maamuzi mengi ikiwemo katika kesi Na.29/2009   CRDB BANK  PLC vs  JAMES VICENT MGAYA.

Ni kweli mtu kashindwa kulipa mkopo lakini si sawa kuuza mali yake bei mnayojisikia. Ni kinyume cha sheria.

Aidha, kwa wale ambao mali zao zimeuzwa bei chee na Taasisi za fedha Sheria imeelekeza mambo mawili ya kufanya.

Moja, Kifungu cha 133(2) Sheria ya Ardhi,  ni kuwa unaweza kufungua kesi ukiomba mnada au uuzaji huo kubatilishwa.

Pili, katika kesi ya Cuckmere Brick Co. vs Mutual Finance (1971) 2 All E.R., 633 unaweza kufungua kesi kuomba fidia. 

Kwahiyo unaweza kuchukua hatua hizo mbili kwa wakati mmoja au ukachakua hatua mojawapo.

Utatakiwa kujiandaa kuthibitisha thamani halisi ya ardhi yako na kuwa thamani iliyouzwa ni ya chini mno.

Uthibitishaji wa hili ni pamoja na Ripoti ya mthamini(Valuation Report) pamoja na kingine chochote ambacho kinaweza kuonesha ukubwa na thamani halisi ya ardhi yako.

Suala la msingi ni kuwa usikubali ardhi yako iuzwe bei ya kutupa hata kama umeshindwa kurejesha mkopo.

0 comments:

Post a Comment