Thursday 18 August 2022

MAHAKAMA INASEMA MWENYE HATIMILIKI NDIYE MWENYE ARDHI UKITOKEA MGOGORO.



BASHIR. YAKUB, WAKILI. -    


Kwanini tunawahimiza watu kuhakikisha unaponunua kiwanja, nyumba ama shamba unapata hatimiliki,  majibu yapo kesi No. 35/2019 kati ya AMINA MAULID&others   Vs RAMADHAN JUMA.

Mahakama ya rufaa  mara zote ikiwemo kupitia kesi hii niliyotaja hapa juu imekuwa ikisisitiza kuwa mwenye hatimiliki ndiye mmiliki wa ardhi. 

Naongelea Hatimiliki "TITLE DEED" au "CERTIFICATE OF OCCUPANCY" sio mkataba wa serikali za mitaa, tuelewane hapa.

Maana yake ni kuwa ikiwa wewe  huna hati, na mwenzako ana hati na mnagombea ardhi moja, basi huyu mwenye hati ndiye atahesabika mmiliki wa hiyo ardhi.

Hii imerudiwa tena  kwa msisitizo na mahakama ya rufaa tarehe 22 April 2022  katika kesi ya James Makundi vs Dunstan Rutageruka No. 181/2021.

Huu ndio msimamo na hivyo ndivyo sheria inavyosema. Kwahiyo ni muhimu kuwa na hatimiliki ili kujiweka katika nafasi nzuri na kuepuka kabisa hii migogoro ya ardhi.

Hakikisha una hatimiliki yako. Yawezekana kabisa ni kweli wewe usiye na hati ndiye mwenye ardhi kweli, na yawezekana kabisa huyu mwenye hati anakuonea.

Lakini hili halitakusaidia ikiwa mwenzako anayo hati kutokana na huu msimamo wa sheria ambao ndio unaoangaliwa na mahakama. Mahakama haijui historia yenu inachoangalia ni sheria inasemaje.

Vinginevyo wewe usiye na hati uwe na ushahidi wa kujitosheleza kuwa mwenye hati aliipata kwa ujinai.  Jambo ambalo wakati mwingine ni vigumu kulithibitisha. 

Muhimu nunua ardhi, itafutie hati uwe salama.

0 comments:

Post a Comment