Latest Post

Monday, 24 July 2017

JE WAJUA KUFUNGA NDOA NA MWANAMKE AMBAYE HAJAPEWA TALAKA NI KOSA LA MIAKA 3 JELA ?.

|1 comments

Image result for KUOA NDOA
NA  BASHIR  YAKUB - 

Mwanamke  ameachwa  na  mume  wake  wa  zamani.  Lakini  hajamuacha  kisheria.  Hakumpa  talaka  isipokuwa  waliachana  tu  kila  mtu  akaendelea  na  maisha  yake tena  kwa  muda  sasa.  Wewe  umekutana  na  huyo  mwanamke  na  umeanzisha  naye  mahusiano.  Umeanza  kuishi  naye  au  umeamua  kabisa  kumuoa.

Ulimuuliza  kuhusu  mahusiano  yake  ya  zamani   akakueleza  bila  kukuficha  yaliyomsibu.  Na wewe  ukaona  kwa kuwa  tayari  hayuko  na  huyo  mume  wake  wa  zamani  kwa  muda  mrefu  au  muda  kiasi    basi  haina  shida. Kitu  cha  msingi  kwako   ulichozingatia  ni  kuwa   hawa  watu  hawako   wote  tena  kwa  maana  mahusiano  yao  waliyasitisha.

Je  sheria  inasemaje  kuhusu  hali  hii.  Je  kukaa  na  mwanamke  wa  namna  hiyo  kwa  maana  ya  kuishi  naye  bila  ndoa,  au  kuishi  naye  kwa  ndoa  au  kuwa  naye  katika  mahusiano  bila  kuishi  naye  kumezungumziwaje   na  sheria.  Je  uko  salama.  Je  hakuna  lolote  linaweza  kukutokea   likakusababishia  usumbufu,  gharama,  na   kurehani  mustakabali  wa  maisha  yako.  Je  nini  ufanye  ikiwa  umo  katika  hali  kama  hiyo.

Haya  na  mengine  yataelezwa  hapa  chini. Sura  ya  29 ya  sheria  ya  ndoa  ,  iliyorekebishwa  mwaka  2010   itatupatia  majawabu  ya  maswali  haya.

1.NI  WAKATI  GANI  NDOA  HUHESABIKA  IMEVUNJIKA.

Ndoa  ni  zao  la  sheria  na  kufa  kwake  hufa  kisheria. Ndoa  haivunjiki  isipokuwa  taratibu  za  kisheria  zimefuatwa.  Ndoa  inaweza  kuvunjika  kwa  kifo  cha  mmoja  wana  ndoa,  kwa  kupotea  kwa  mda  mrefu  na  kuihisiwa  kufa  kwa  mmoja  wa  wanandoa( presumption  of  death), lakini  pia  ndoa  hufa/huvunjika  kwa  talaka.

Kama   mojawapo  ya  hayo  juu  halijajitokeza  ndoa  hiyo  bado  inaishi.  Kwahiyo  mwanaume  unatakiwa  kujua  kuwa  mwanamke  uliyemuoa  au  unayeishi  nae  bila  ndoa  au  uliye naye  tu  katika  mahusiano  ya  kawaida  ,  ikiwa hapo  awali  alikuwa  katika  ndoa   na  mojawapo  ya  yaliyotajwa  hapa  juu  hayajatokea  basi  mwanamke  huyo  ndoa  yake  bado  inaendelea.  Hapo  badae  itaelezwa  hatari   kubwa zinazokukabali .

2.    JE  KUTENGANA  NI  TALAKA.

Unaweza  kudhani  kuwa  uko  salama  kwasababu  una  uhakika   mwanamke  uliyenaye  ametengana  na  mme  wake  wa  mwanzo  na  hivyo  wewe  uko  salama. Kisheria  kuna  tofauti  ya  kutengana  na kuachana/kutalikiana.  Kutengana  sio  talaka.  Talaka  ni  talaka  mpaka  itolewe  kwa  mujibu  wa  sheria.

Pia  kutelekeza  sio  kuachana/talaka.  Watu  wanaokuwa    wametengana  au  wametelekezana  bila  talaka  fahamu  kuwa  watu  hao  kisheria  bado  ni  wanandoa.  

3.  KIFUNGO  CHA  MIAKA  3.

Kifungu  cha  152 ( 1) cha  sheria  ya  ndoa   kinakifanya  kitendo  cha  kufunga  ndoa  na  mwanamke  ambaye  bado  ndoa  yake  haivunjwa  kisheria  kuwa  kosa.  
Kifungu  kidogo ( 1 )  na ( 2 ) kinasema  kuwa  mme  aliyemuoa  mke  huyo  na  mke mwenyewe  aliyeolewa  wote  kwa  pamoja  wanahesabika  kutenda  kosa  hili.  Na  kifungu  kidogo  cha  ( 3 )  kinasema  kuwa  hao  wote  wawili  wakithibitika  kutenda  kosa  hilo  basi  adhabu  yao  ni  kifungo  kisichozidi  miaka  3  jela.    

Lakini  pia  kifungu  kidogo  cha ( 4 )  kimemuingiza  kila  mtu  ambaye ameshiriki  kwa  namna  moja  ama  nyingine  katika ndoa  hiyo  kuwa  ametenda  kosa  na  adhabu  yake  kuwa  kifungo  kisichozidi  miaka  mitatu  kama  ilivyo  kwa  wahusika  wakuu.

Kwa  ujumla hili   linahesabika  ni  kosa  la  mwanamke  kuolewa  mara  mbili  na  wanaume  wawili  tofauti  kwa  wakati  mmoja(Polyandry).
Aidha  kuishi  naye  tu  bila  kumuoa  mwanamke  ambaye  ndoa  yake  haijavunjwa  kisheria au kuingia  naye  katika  mahusiano  ya  kimapenzi   bila  kuishi  naye,  ni  kosa  la  zinaa( adultery) . Sheria  yetu  inatambua kosa  la  zinaa. Kifungu  cha  72  cha  sheria  ya  ndoa kinatoa  adhabu ya  kulipa fidia  kwa atakayezini  na  mke  wa  mtu  au  mme wa  mtu.

Ni  vema  kujihadhari  ili  kuepuka  kuingia  katika  msukosuko  wa  sheria.  Hakikisha  mwanamke  anapata  talaka  kwa  mujibu  wa  sheria  halafu  wewe  sasa  uendelee  naye  kwa  amani. Usiseme  huyu  si  ameachika  tuu,  hapana,  hakikisha  amepata  talaka.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA  JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


Wednesday, 19 July 2017

KAMA HAIJAPITA MIAKA 12 UNAWEZA KURUDISHA ARDHI ULIYODHULUMIWA.

|0 comments
Image result for KIWANJA

NA  BASHIR  YAKUB -

1.UKOMO  WA  HAKI.

Hakuna  haki  isiyo  na  ukomo wa  muda  unapokuwa  unaidai. Huwezi  kudai  haki  muda  wowote  unaotaka  wewe. Ni  lazima   udai  haki  ndani  ya  muda.Na  ni  ule  muda tu uliowekwa  na  sheria. Ipo  sheria  rasmi  inayoeleza  muda  wa  kudai  haki  mbalimbali.  Inaitwa Sheria  ya  Ukomo  wa  Muda ,  Sura  ya  89.  Katika  sheria  hiyo   hapajaelezwa tu   ukomo  wa  kudai  haki  katika  masuala  ya  ardhi  bali  pia  katika  masuala  mengine  yote  ya  haki  unazoweza  kudai.

Ndani  ya  Sheria  ya  Ukomo  wa  Muda  kumeelezwa ukomo  wa  kudai  haki  iliyotokana  na  masuala  ya  mikataba na  makubaliano, ukomo   wa  kudai  haki  katika  masuala  ya  udhalilishaji, ukomo  wa rufaa, ukomo  wa  haki  katika  masuala  ya bima, madai  ya  fedha,  rehani  za  mikopo, na mambo  mengine  mengi.

2.  HUJAPITWA  NA  MDA  BADO UNAWEZA  KUIDAI  ARDHI  YAKO.

Wako  watu  huko  nyuma  walidhulumiwa  ardhi  muda  mrefu  na  sasa  wamekata  tamaa.  Wamekata tamaa  kutokana  na  kuona   ni mda  mrefu  umepita  tangu  haki  hiyo  iporwe  na  sasa  wanadhani  kuwa   hawawezi  tena  kudai  haki  hiyo.

Wako  watu wamedhulumiwa  ardhi  katika  masuala  ya  mirathi,  katika  masuala  ya  mikopo,  katika  masuala  ya  mikataba  na  makubaliano,  katika  masuala  ya  ndoa  na  machumo  ya mali  za  ndoa, katika  masuala  ya  uvamizi, katika  masuala  ya  kuharibu  mipaka  n.k. Na  ardhi  hapa  tunazungumzia  mashamba,  viwanja  na  nyumba. Hivi  kwa  pamoja  ndivyo  huitwa  ardhi.

Basi  yafaa  ujue  kuwa kama  wewe  ni  kati  ya  waathirika  wa  jambo  hili  basi  bado unayo  haki  ya  kudai   ardhi  yako  madhali  muda  huo  haujakupita.  Haki  yako  inaishi   mpaka  miaka  12  na  itakufa baada  ya  muda  huo.  Kama  imepita  miaka  sita,  mitano,  nane,  kumi,  n.k.  bado  muda  wako  wa  kudai  na  kurudishiwa  ardhi upo.

3.  KWA  WANUNUZI   WA   ARDHI  ZENYE  UTATA.   

Kwa  wale  wanaonunua/ walionunua  ardhi  zenye  utata  yafaa  nao  wafahamu  kuwa  hawapo  salama  mpaka  miaka  12  ipite  toka  umenunua  ardhi  hiyo.  Muda  wowote  kabla  ya muda  huo  kupita  unaweza  kupokea  wito  wa  mahakama  na  kutakiwa  kujibu  malalamiko  kuhusu  ardhi  uliyonunua au  kupata  kwa  namna  nyingine. 

Ndio  maana   mara  kwa  mara  tumekuwa  tukiandika  na  kusisitiza  
kuhusu  kufuata  utaratibu  katika  kununua/kupata  ardhi  ili  mwisho  wa  siku  uwe  salama  na  uwe  na  amani  na  mali  uliyonunua/pata. Pata  ardhi  kwa  kufuata  taratibu  za  kisheria ili uishi  bila  mashaka  na  ufurahie  mali  yako.  

4.  ISEMAVYO  SHERIA  KUHUSU  MIAKA  12.

Schedule  ya  kwanza ,  Sehemu  ya  kwanza, 22,  ya  Sheria  Ya  Ukomo  wa Muda  ndiyo  iliyoeleza haki hii  ambayo  imeelezwa  hapa  juu. Inasema  kuwa  unatakiwa  kudai  ardhi  ndani  ya  miaka  12.  Muda  huu  unahesabika  tangu  siku  mgogoro  ulipotokea.  Ikiwa  tangu  siku  mgogoro  ulipotokea  mpaka  leo  haijapita  miaka  12  basi  bado  uko ndani  ya  muda ,  kwa  maana  unaweza  kudai  ardhi  yako  na  ikarudishwa.

Lakini  ikiwa  tokea  kutokea  kwa  mgogoro  na  sasa  unapotaka  kudai  kurudisha  ardhi  yako  ni  muda  umepita miaka  12  basi  haki  hiyo  umeiua  mwenyewe  na  muda  tayari  umekupita.

Mwisho  niseme  kuwa  katika  haki  zote  za  kudai  mali  ni  ardhi  pekee  iliyopewa  muda  mrefu  wa  kudai  kuliko  nyingine. Hii  ni  kutokana  na  umuhimu  na  unyeti wa   ardhi.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


Wednesday, 14 June 2017

NINI UFANYE IKIWA MTU AMEJENGA NA KUZUIA NJIA.

|0 comments
Image result for UKUTA KUZIBA NJIA

NA  BASHIR  YAKUB -

Jirani  yako  au  mtu  mwingine  yeyote  amejenga   na  kuziba  njia. Njia  yoyote iwe  kubwa  kama  barabara  ama  ndogo  ambayo  hata  gari  haiwezi  kupita. Iwe  tu kama  ya   pikipiki  au  baiskeli au hata  ya  miguu  tu.  Yote  haya  hayajalishi  na hizi  zote  ni  njia kwa  mujibu  wa  sheria.

1.HAKI  YA  NJIA  KISHERIA .

Kifungu  cha  151  cha  sheria  namba  4  sheria  ya  ardhi  ya  mwaka  1999 kinaeleza  haki  hii. Kinaitambua  haki  hii  kwa  kusema  kuwa  haki  ya  njia  ipo  kwa  njia  zile  ambazo  ni  kwa ajili  ya  matumizi  ya  umma.  Umma  hapa  humaanisha  watu  wote  lakini  pia  wakazi  wa  eneo  fulani  wanaotumia  njia  hiyo  kwa  ajili  ya  shughuli  zao  mbalimbali.

Kifungu  kimepanua matumizi  ya  njia  ya  umma  kwa   kumaanisha  hata  njia  zilizotengwa  kwa ajili  ya  makampuni  binafsi. Kwa  mfano  kuna  sehemu  ukipita  utaona njia  au  sehemu  ya  lami  ya  barabara imekatwa  maalum  kwa  ajli  ya  kuruhusu watu  au magari  ya  kampuni  fulani  kupata  sehemu  ya  kuingilia.

Lakini  pia  zipo  njia  zimetengwa  kwa  ajili  ya  shughuli  za serikali. Haraka  utaona  kuwa haki  ya njia  haijagusa tu  kule  mitaani  wanakoishi  watu  tu  bali  hata  sehemu  za  makampuni  binafsi  nk.

2.   KUZIBA  NJIA  YA  UMMA.

Kuziba  njia  ya  umma  ni  kosa  kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  177( 4 )  cha  sheria  ya  ardhi. Wako  watu  wakorofi  huko  mitaani  huziba  njia  kwa  makusudi.  Yawezekana kabisa  mtu  akiwa  anajua kabisa eneo  fulani  ni  njia  na  watu  hupita  hapo  lakini  kwa makusudi  au bila  kujali  akajenga  ukuta au akaweka uzio  wa  sinyenge  au  akapanda  mti  pale  au  akaweka  kifusi au  kwa  namna  nyingine  yoyote.  

Na  wengine  huambiwa  na  watu  lakini  wasisikie   kwasababu  ya  pesa,  au  urafiki  na  viongozi  wa  serikali  au  cheo  au  rushwa  au  vinginevyo.  Basi  yatupasa  kujua kuwa  watu  hawa  huwa  wakitenda  makosa  na si  wakunyamazia.

Njia  kuzibwa si  lazima  iwe  imezibwa yote.  Hata kuibana na kuitoa  katika  uhalisia  wake  katika  kiwango  chochote  nako  ni  kuziba  njia.  Njia  yafaa  iachwe  vilevile  ilivyo.

3.   NINI  UFANYE  IKIWA   NJIA  IMEZIBWA.

Yako  mambo  mawili  unaweza  kufanya ikiwa  mtu  amewazibia  njia. Moja  ni  jepesi  na  la  pili  sio  jepesi. La  kwanza  ni  kwenda  mahakamani  kwa  kufungua  malalamiko  na  pili  ni  kupeleka  malalamiko  kwa  kamishna  wa  ardhi.   
Kwenda  mahakamani  ni njia  ambayo  sio  nyepesi sana.  Ina  gharama ,  na  inapoteza  muda  zaidi. Na  ikiwa utaamua  kwenda  mahakamani  basi   mahakama  inayotumika  katika mambo kama  haya  ni  mahakama  ya  ardhi.

Baraza  la  ardhi  la  kata  na  la  kijji ni  sehemu  ya  mahakama  za  ardhi. Hata  hivyo  kama  utaamua  kwenda  mahakamani  ni  vema  zaidi  ukaanza  na  mabaraza  haya ya  kata  na kijiji. 

Na  uzuri  mabaraza  haya  hayana  gharama, na  kesi  haichukui  mda  mrefu.  Ni  tofauti  na  ukiamua  kutumia  baraza  la  ardhi  la  wilaya  au  mahakama  kuu  ya  ardhi.

La  pili  ambalo  sasa  ni  ndilo jepesi ni  kupeleka  malalamiko  kwa  kamishna  wa ardhi . Kifungu  cha 176 ( 1)  kinasema  kuwa  kamishna  wa  ardhi  ana  mamlaka  ya  kutoa  amri  kuhusu  njia  iliyozibwa  ikiwa  ataridhika  kuwa ni  kweli  njia  imezibwa  tena kimakosa.

Kwa  hiyo  badala  ya kuhangaikia  mambo  mengine  ni  bora  basi  ukapeleka  malalamiko  yako  kwa  kamishna wa  ardhi  naye  atatoa  amri  ambayo  ni  lazima  kwa  aliyeziba  njia  kuitekeleza.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com

Monday, 12 June 2017

UFAFANUZI MUHIMU KUHUSU USAJILI WA ACCACIA.

|0 comments
Image result for ACACIA TANZANIA

NA   BASHIR  YAKUB - 

Kwa kutumia kigezo cha usajili, Tanzania tunazo aina kuu mbili za  kampuni. Kampuni za ndani(Local companies) na kampuni za kigeni ( foreign companies).

Kampuni za ndani ni zile  zote zilizoanzishwa  hapa nchini na kusajiliwa hapa nchini. Hata kama wanahisa wake wote ni raia wa kigeni kwasababu tu ya kuanzishwa hapa na kusajiliwa hapa zinakuwa ni kampuni  za ndani.

Kampuni ya kigeni ni ile iliyoanzishwa na kusajiliwa nje ya Tanzania lakini ikaanzisha ofisi/biashara/tawi hapa Tanzania. Sheria Na. 12 Sheria ya Makampuni kifungu cha 433 kinasema hivyo. Kampuni kama imeanzishwa nje hata kama wanahisa wake wote ni Watanzania, hapa kwetu hiyo bado ni kampuni ya kigeni.

Kampuni ya ndani inaposajiliwa hupatiwa cheti cha usajili kiitwacho "Certificate of Incorporation" kwa mujibu wa kifungu cha 15(2) Sheria ya Makampuni. Kampuni ya ndani inapopata cheti hiki basi usajili wake huwa umekamilika na inatambulika rasmi kama kampuni ya ndani.

Kampuni ya kigeni inaposajiliwa hapa Tanzania hupatiwa cheti kiitwacho "Certificate of  Compliance" kwa mujibu wa kifungu cha 435(1) Sheria ya Makampuni. Kampuni ya kigeni inapopata cheti hiki basi  usajili wake huwa umekamilika na hutambulika rasmi kama kampuni ya kigeni.

Acacia ni kampuni ya kigeni. Kwa maana kuwa ilianzishwa nje ya Tanzania na kufungua shughuli zake hapa nchini. Kwa hiyo ili ihesabike imesajiliwa Tanzania ilitakiwa kuwa na cheti kiitwacho"Certificate of Compliance". Kutokuwa na cheti hiki maana yake ni kuwa haijasajiliwa Tanzania na haitambuliki.

Nimesikia mjadala BBC SWAHILI leo wanaojadili wakijiuliza inawezekanaje kampuni kubwa kama hii ikafanya biashara bila usajili. Watanzania wengi pia wanajiuliza swali hili.

Jibu lake ni hili. Acacia ni kampuni tanzu(Subsidiary  Company) ya Barrick. Kampuni inakuwa tanzu pale ambapo zaidi ya nusu ya hisa zake zinamilikiwa na kampuni nyingine. Ile inayomiliki huitwa "holding company" na inayomilikiwa huitwa "subsidiary company". Kwahiyo  Barick ni " holding" wakati Acacia ni "subsidiary".

Barrick inamiliki hisa za Acacia 63.9%. Kwa kusema hivi maana yake Barrick ndiye mwenye Acacia. Hata hivyo kwa mujibu wa sheria hizi zinahesabika kampuni mbili tofauti na kila moja inabeba wajibu na hatia zake yenyewe(its own responsibility& liability).

Basi kumbe kilichotokea ni kuwa Acacia walikuwa wakifanya biashara kwa jina la Acacia lakini wakibebwa na mgongo wa  Barrick. Walijificha hapa na wakaweza kuishi bila usajili wa kwao kama wao. Walijibeba kwenye usajili wa Barrick.

Barrick wao wanao usajili na wanayo " Certificate of Compliance" ya kwao ambayo tayari wameitoa hadharani. Kwakuwa haya ni makampuni mawili tofauti kila moja inatakiwa kuwa na cheti chake  kwa mujibu wa kifungu cha 487 Sheria ya Makampuni na kutokufanya hivyo ni kosa kabisa. Kwa hiyo hivi ndivyo ilivyowezekana kampuni hii kufanya biashara bila usajili miaka hii yote.

Adhabu ya kosa kama hilo ni kifungo jela. Sheria Na. 12 Sheria ya Makampuni iliyofanyiwa Marekebisho mwaka 2002, kifungu cha 472 kinasema hivyo.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com

Monday, 5 June 2017

JE ULIPEWA NOTISI YA SIKU 60 KABLA BENKI HAIJAUZA NYUMBA/KIWANJA CHAKO ?.

|0 comments

Image result for MKOPO
NA  BASHIR   YAKUB - 

Wanaokopa  hela  kwenye  taasisi  za  fedha  wanatakiwa  kujua  haki  walizonazo. Haki  kabla  ya  kuchukua mkopo,  haki  wakati  wa  kuchukua  mkopo,  haki  wakati  wa  kurejesha,  na  haki  baada  ya  kurejesha au  kushindwa  kurejesha. Hautakiwi  kusubiri  taasisi  iliyokukopa  iwe ndiyo ya  kukueleze  haki  ulizonazo  bali  watakiwa ujue   haki    hizo  kwa  jitihada  zako.

Taasisi  ya  fedha  inaweza  kukueleza  baadhi  ya  haki  lakini  ni  muhali  kukueleza  haki  ambazo  wao  zinawabana. Watakueleza haki  ambazo  hazina  madhara  kwao. 
Basi  yakupasa  ulijue  hili.

Masuala  ya  kuweka  rehani  ili  upate  mkopo  yanaongozwa  na  sheria  mbili.  Sheria  namba  4  ya  mwaka  1999    Sheria  ya  ardhi,  pamoja  nayo  Sheria  namba  17  Sheria  ya  rehani  ya  mwaka  2008. Humo  zimo haki  nyingi  za  mtoa  mkopo   wakadhalika  mchukua  mkopo.  Hata  hivyo  tutatizama  haki  moja  tu ya   notisi  kabla  ya  kuuzwa kwa   nyumba/kiwanja  cha  mkopaji.       

1.KUSHINDWA  KUREJESHA  MKOPO.

Kifungu  cha  127 ( 1 ) cha  sheria  ya  ardhi  kinaeleza   habari  ya  kushindwa  kurejesha  mkopo. Kifungu  kimeieleza  habari  hii  ikiwa  miongoni  mwa  mambo  ambayo  yanachukuliwa  kama ukiukwaji wa  masharti  ya  mkataba  wa  mkopo. 

Mengine  ambayo  yanachukuliwa  kama  ukiukwaji  wa  masharti   ya  mkopo  ni  kuweka  rehani  mara  zaidi  ya  mmoja  kwa  taasisi  tofauti, kuuza, kupangisha  wakati  kuna  rehani  bila  taarifa   au  ridhaa kutoka  kwa  mtoa  mkopo n.k.  Hata  hivyo   haya  na  mengine  yatachukuliwa  kama  kukiuka  masharti  ya  mkopo  ikiwa  yamekatazwa  katika  mkataba  wako  na  taasisi  ya  fedha.

Pia  kwa  mujibu  wa  kifungu  hicho  kushindwa  kurejesha  mkopo  kunajumuisha  pesa  kamili  uliyoikopa,  riba, pamoja  na  makato  mengine  ambayo  yanajenga  sehemu  ya  mkopo.

2.  NOTISI  YA  SIKU  60.

Hii  ni  notisi   ya  lazima  kabla  nyumba/kiwanja  chako  hakijauzwa.  Si  tu  lazima upewe  bali  pia ni  lazima   iwe  ya  siku  60. Kamtindo  ka  kuwapa  watu  siku  14  au  chini  yake  au  zaidi  kidogo  kanakiuka  sheria. Na  hapo  baadae   tutaona   ufanye  nini  ikiwa  hilo  limekiukwa.

Kifungu  cha  127( 1 ) ( a ) kimeeleza  kuwa   pale  mkopaji  anapokuwa  ameshindwa  kurejesha  kwa mujibu  wa  makubaliano  ya  mkopo   basi  taasisi  ya  fedha  itampa  mkopaji  taarifa( notice)  ya  siku  60  ambapo  siku  hizo  zikiisha   kabla  mkopaji  hajalipa   basi  taasisi hiyo  inaweza  kuendelea  na  hatua  za  kuuza  ikiwa  itaamua  kufanya  hivyo.

Kwahiyo  ni  lazima  kuwepo  na  taarifa  ya  siku  60. Na  siku  hizo  zinaanza  kuhesabiwa  tokea  siku  ulipopokea  notisi  ya  kwamba  umeshindwa  kulipa. Hivyo  basi  ukipokea  notisi  leo  anza  kuhesabu  mpaka  siku  60.  Humo  katikati  hawataruhusiwa  kuuza  mali  yako. Na  wakiuza  ndani  ya  muda  huo  basi  itakuwa  ni  makosa.

Juu    ya  hilo  ni  vema  pia  ukajua  kuwa notisi  hiyo  ya  siku  60  haihusishi  tu  uwezo  wa  kushindwa  kulipwa.  Bali  pia  lolote  lile  ambalo  ni  sharti  katika  mkataba  wa  mkopo  na  ambalo  taasisi  ya  fedha  inadai   umelikiuka. Hapo  pia  haitachukua  hatua  ya  kuuza  mali  yako  hadi  upate  notisi  hiyo  ya  siku  60.

3.  NINI  UFANYE   IKIWA  NOTISI  HIYO  ITAKIUKWA.

Kwanza   kama  nyumba/kiwanja  hakijauzwa  kimbilia  mahakamani  na   weka  zuio,  na  pili  kama  tayari   mali  imeuzwa   tena kwa  kukiuka  notisi  na muda  wake  basi  unaweza  kufungua  shauri  la  kubatilisha  mauzo  hayo   kwa  msingi  wa  kukiukwa  kwa taratibu  za  mauzo  na  waweza  kurejeshewa  mali  yako.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com