Wednesday 1 November 2023

USIPOSOMEWA MAONI YA WAZEE WA BARAZA KWENYE KESI ZA ARDHI, HIYO KESI NZIMA NI BATILI.

 

Bashir  Yakub., WAKIL

Kwa wale ambao mna kesi za ardhi katika mabaraza/mahakama za wilaya mnapaswa kujua kuwa ni lazima kusomewa maoni ya wazee wa baraza kabla ya kusomewa hukumu.

Kutokusomewa maoni ya wazee wa baraza ni kosa kisheria na inabatilisha kesi nzima. 

Hivyo ikiwa umekuwa na kesi baraza la ardhi la wilaya, na hukumu imesomwa na kabla ya hukumu wazee wa baraza hawakujitokeza kuwasomea maoni yao, basi kesi hiyo nzima ni batili  na hivyo ukikata rufaa kwa kigezo hicho utashinda.

Kesi zote za ardhi mbele ya mahakama/mabaraza ya ardhi ya wilaya(DLHT)  husikilizwa na hakimu/mwenyekiti pamoja na wazee wa baraza. 

Kwa uelewa, hapa Hakimu huitwa pia Mwenyekiti na pia mahakama huitwa baraza, yote humaanisha kitu kimoja.

Sasa tujue kuwa ni lazima  inaposikikizwa kesi  katika mabaraza haya wawepo wazee wa baraza(assessors) na hili ni takwa la lazima kisheria. 

Hivyo basi kwakuwa wanakuwepo kwenye kusikiliza basi usikilizaji unapoisha sheria inawataka na wao kutoa maoni yao kwa kueleza nani anashinda na nani anashindwa kutokana na namna walivyosikiliza shauri.

Maoni hayo huwa yanazingatiwa na hakimu/mwenyekiti hata hivyo halazimiki  kuyafuata na ndio maana yanaitwa Maoni(opinion), ikiwa na maana kuwa kuna uhiari, yanaweza kufuatwa au kuachwa.

Hata hivyo, ikiwa hakimu/mwenyekiti  ameyafuata au hakuyafuata ni lazima aeleze kwenye hukumu, mosi kwamba yalitolewa, na pili kama aliyafuata au hakuyafuata na kwanini.

Pamoja na hayo, kuna jambo moja ambalo limekuwa halifanyiki ambalo sasa unapaswa kulijua ikiwa una kesi ya ardhi.

Jambo hili ni takwa na lazima wazee hao wa baraza kusoma maoni yao mbele ya wenye kesi(parties) kabla ya kusomewa hukumu.

Hili ni takwa la lazima kuwa mnapaswa kusomewa maoni ya wazee wa baraza kabla kusomewa hukumu, ili mpate kujua wao walionaje shauri lenu  na walitoa maoni gani.

Ikiwa hamkusomewa maoni ya wazee wa baraza basi shauri lenu lote ni batili, na ikiwa ulishindwa katika shauri la namna hii yafaa ukate rufaa na utafaulu.

Katika Rufaa Na.7/2021 kati ya ATHUMANI HAMIS BENTA  vs ISSA MOHAMMED BENTA hukumu iliyotolewa na Mahakama ya rufaa tarehe 29 / 9 /  2023  mahakama imebatilisha shauri zima na kuamuru likarudiwe upya kutokana na kosa la kutowasomea wahusika wa kesi(parties) maoni ya wazee wa baraza.

Maamuzi kama hayohayo pia yametolewa katika Shauri Na.154/2015  AMEIR MBARAKA&WENGINE dhidi ya EDGAR KAHWILI.


Kwahiyo tujue sasa kuwa haya ndio mahitaji ya sheria na kama una shauri la ardhi wilayani basi ni lazima usomewe maoni ya wazee wa baraza ili ujue wao walilionaje hilo shauri.


Ikiwa hawakuwasomea maoni yao na shauri limeisha, basi hii sababu nzuri(ground) ya kukata rufaa kubatilisha shauri zima.


0 comments:

Post a Comment