Wednesday 10 August 2022

KWA WANAONUNUA ARDHI WAKALIPA KIASI NA KUBAKIWA NA DENI LA KUMALIZIA.



NA BASHIR. YAKUB, WAKILI  - 

Kesi ya ardhi Na. 115/2021 kati ya KASSIM NAGOROKI  vs HASSANI KINGUMBI inatupatia funzo muhimu.

Kassim alinunua ardhi ekari 4 kutoka  kwa Hassani. Bei ya manunuzi jumla ilikuwa Tsh Milioni moja huko Ihango, Malinyi, Morogoro.

Siku ya mauziano Kassim alilipa laki moja na akaahidi kumalizia laki tisa baadae mwezi wa 11.

Ilipofika mwezi 11 hakumalizia hela kama alivyokuwa ameahidi na hivyo kumfanya Hassan kudai hela yake.

Hata hivyo Kassim hakulipa hela hiyo mpaka ilipofika January alipomwita Hassan kumpatia kiasi hicho kilichobaki.

Hassan alipoitwa kupokea kiasi hicho kilichobaki alikataa kukipokea na kusema kuwa hauzi tena ardhi na hivyo hataki tena hiyo hela na akaweka wazi kuwa ardhi imemrudia.

Yakapita malumbano ya mda mpaka Kassim akafungua kesi dhidi ya Hassan kwa kuchukua ardhi ambayo ameshamuuzia.

Kutokana na hilo Mahakama kuu ya Tanzania ikatoa uamuzi wake kuwa Hassan yuko sahihi kujirudishia ardhi yake kwakuwa Kassim alivunja mkataba. 

Kitendo cha kutolipa hela iliyobaki katika muda ambao umekubaliwa ni kuvunja mkataba na hivyo huwezi tena kumiliki hiyo ardhi.

Kutokana na hilo ni muhimu wanunuzi wa ardhi kujua kuwa ukinunua ardhi iwe kiwanja, nyumba, ama shamba , halafu ukalipa kiasi na kikabaki kiasi una wajibu wa kulipa hicho kiasi bila kukosa katika mda ambao mmekubaliana.

Kushindwa kufanya hivyo muuzaji ana haki kujimilikisha tena ardhi yake na akaichukua mwenyewe kwa matumizi yake ama kuiuza kwa mwingine.

Ushauri ni kuwa kama ukiona muda wa kumalizia hela umekaribia na wewe hujapata hela basi Sheria inaruhusu kumuomba muuzaji akuongezee muda ili uweze kupata hiyo hela na kumalizia.

Ukikaa kimya muda ukapita unahesabika umevunja mkataba na utapoteza hiyo ardhi.

0 comments:

Post a Comment