NA BASHIR YAKUB -
Usimpe wakili kesi yako akusimamie halafu ukalala nyumbani na
kujisahau. Ni lazima uhakikishe unafuatilia kujua kinachoendelea. Na kufuatilia
sio lazima kila siku kesi inapoitwa
mahakamami nawe uwepo,laa hasha. Hii ni kwasababu kama utalazimika kila kesi
inapoitwa na wewe uwepo mahakamani kwa namna fulani tunaweza kupoteza maana ya
kumweka wakili. Ninachomaanisha ni kuwa, ni muhimu ukawa unapata mrejesho wa mara
kwa mara kujua kinachoendelea, hata kwa kupiga simu.
Umuhimu na ulazima wa kufuatilia unatokana na ukweli kuwa
kesi ni yako. Kesi sio ya wakili. Wakili yeye ni mwakilishi tu. Kwa msingi huu
ikiwa kuna jambo litakwenda mrama madhara yanakuja kwako mwenye kesi na sio kwa
wakili.
Mfano mmoja wapo upo
kwenye kesi ya Edga Msola vs Dr. Edward Wilson
Ngale na Philip Japhet Mangula,Maombi Namba 442/2018. Katika kesi hii ndugu Edga alimpa wakili
kazi ya kuandaa na kupeleka mahakamani mawasilisho ya hoja za rufaa(submission
in support of grounds of appeal). Hata hivyo inaonekana muda aliopewa wakili
kupeleka mawasilisho hayo uliisha bila kupeleka.
Matokeo yake rufaa nzima ikafutwa. Pia inaonekana hayo
yalifanywa bila Ndugu Edga ambaye ni mwenye kesi kujua. Na hii ilitokana na
kuamini kwake kuwa kesi anayo wakili na hivyo kila kitu atafanya yeye. Hata
hivyo baadae Ndugu Edga alikuja kujua kuwa rufaa yake imefutwa kwa kushindwa
kupeleka mawasilisho mahakamani.
Kutokana na hilo akamtafuta wakili mwingine ambaye aliamua kupeleka
maombi ya kuomba rufaa iliyofutwa kusajiliwa upya(re-admission). Katika maombi
hayo hoja na sababu kubwa aliyoitoa ndugu Edga ili rufaa yake iliyotupwa iweze
kukubaliwa kusajiliwa upya ni kuwa, alimuamini na kumkabidhi wakili wake kazi
yote na hivyo hakujua kama wakili alishindwa
kupeleka mawasilisho na hivyo kupelekea kesi yake kufutwa.
Kwahiyo aliishawishi mahakama kuwa hilo halikuwa kosa lake
bali la wakili, na hivyo kufutwa rufaa yake kwa kosa la wakili sio jambo la
haki , na kwasababu hiyo aliiomba
mahakama ikubali kusajili upya rufaa yake ili aweze kusikilizwa anasema nini
kwenye hiyo rufaa.
Maamuzi ya mahakama katika hili ilisema kuwa, sababu ya kuwa
wakili hakufanya kitu fulani sio sababu ya msingi ya kuishawishi kukubali kusajili
upya rufaa yake. Kwa msingi huu haya maombi yake ya kuomba rufaa yake irejeshwe
nayo yakatupwa.
Maana yake kwa kosa lile la wakili la kutopeleka mawasilisho
kwa wakati limesababisha huyu ndugu Edga apoteze rufaa yake moja kwa moja kwakuwa
amekataliwa hata kuirudisha. Kama alikuwa na haki ya kushinda kwenye rufaa maana
yake amepoteza hiyo haki.
Na wakati mahakama ikitupa maombi yake ya kurejesha rufaa
ilisisitiza kuwa, pamoja na kuwa kesi yake alimkabidhi wakili bado alikua na wajibu
wa kufuatilia kujua kinachoendelea huko mahakamani. Ilisema kama angefuatilia
angejua kinachoendelea na hivyo kumuweka katika nafasi nzuri ya kuchukua hatua
mapema.
Kitendo chake cha kutokufuatilia mpaka haya yote yakatokea
mahakama ilikiita uzembe kwa upande wa ndugu Edga ambaye ndiye mwenye kesi. Na
hapa ndipo ninapowashauri kuhakikisha mnafuatilia kesi zenu hata kama zipo kwa wakili
kwasababu madhara yanakuja kwenu.
Nimesema kuwa hii haimaanishi kuwa mawakili hawafanyi kazi
zao vizuri, hapana. Isipokuwa wakili naye ni binadamu, anaweza kupitiwa, anaweza
kukutwa na dharula iliyo nje ya uwezo wake kama ugonjwa ghafla,kufiwa ama naye akawa
mzembe.
Kwa hiyo myazingatie hayo.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment