NA BASHIR YAKUB -
Hii ni moja ya sehemu ambayo wanadishaji/madalali(auctioneer) wengi huwa wanawakosea wadaiwa. Huwezi kufikia hatua
ya kuuza nyumba au kiwanja cha mtu kabla hujampa taarifa ya siku 14, na kuhakikisha
hizo siku 14 kuwa zimepita. Madalali wengi akishapewa kazi na benki ama taasisi nyingine
ya mikopo kwa ajili ya kunadisha, basi anaanza kazi ya kuuza hapo hapo,au baada
ya mda mchache.
Kifungu cha 12((2) and (3) cha Sheria ya Madalali Wanadishaji
sura ya 227 kinasema kuwa hakuna ruhusa kwa dalali yoyote kuuza nyumba ama
kiwanja cha mtu mpaka mtu huyo awe amepewa taarifa ya siku 14, na siku hizo ziwe
zimeisha.
Kumbe tunaona kuwa haitoshi tu kumpa mtu taarifa ya siku 14, bali pia hizo siku 14 alizopewa
ni lazima ziwe zimeisha. Maana yake tunahesabu siku 14 tangu ulipopokea
taarifa,na baada ya huo mda ndo tunasema zimeisha. Kuuza kunaweza kuanza siku ya 15, siku ya 14
kamili dalali hawezi kuuza nyumba yako.
Nasisitiza eneo hili kwasababu baadhi ya madalali wamekuwa na
tabia ya kutoa hiyo notisi ya siku 14, lakini kabla ya muda huo kuisha anauza nyumba/kiwanja. Hili ni kosa na kama hilo
limetokea kwako basi uuzaji huo ni batili na hautambuliwi na sheria.
Katika kesi ya DOSCA DIDON KARANJA vs TPB BANK PLC, NAMIC
INVESTMENT LTD na HAIDARI MOHAMMED HARIRI, Madai ya Ardhi Namba 64/2015,
Dosca alipewa notisi ya kuuza tarehe 14 August 2015 na tarehe 16 August 2015,
yaani siku mbili baadae, dalali akauza nyumba yake.
Dosca alifungua kesi mahakamani kulalamikia baadhi ya mambo
likiwemo hili. Mahakama kuu ilitoa hukumu kuwa, hata kama alikuwa anadaiwa na
benki na ameshindwa kurejesha marejesho,bado mauzo ya nyumba yake yalikuwa batili
na haramu. Kwa msingi huu akarejeshewa umiliki wa nyumba yake.
Kwahiyo ni muhimu ukalijua hili ili haki iweze kutendeka. Ni vigumu sana haki
yako kutendeka kama wewe mwenyewe hujui hata hiyo haki kama unayo.Nimeandika
mara nyingi kuwa kudaiwa au kushindwa kurejesha hakuna uhusiano wowote na
kusigina haki za mdaiwa. Mdaiwa ana haki nyingi na lazima zizingatiwe anaposhindwa
kurejesha.
Moja ya tatizo la taasisi za mikopo ni kuwapa wakopaji
limkataba kama kitabu, lenye kurasa nyingi,lililoandikwa kwa kiingereza kigumu
cha kisheria, kiasi kwamba hata kama unajua kiingereza bado lugha iliyo kwenye
likitabu hilo itakutatiza tu. Jambo ambalo hata kama zimeelezwa haki za mkopaji
mle ndani, si rahisi kuzijua na
akajifunza. Ingekuwa ni vyema zaidi mkopaji pamoja na semina za matumizi ya pesa
ya mkopo, lakini pia akafundishwa haki zake hasa wakati atakaposhindwa
kurejesha.
Kifungu nilichotaja hapo awali cha 12((2) and (3) cha Sheria
ya Madalali Wanadishaji Sura ya 227, kinasisitiza kuwa haitoshi tu kumpa mdaiwa
notisi ya siku 14, bali pia notisi hiyo iwe katika lugha inayoeleweka, na yasiwe
tu maandishi katika karatasi, bali pia namna nyingine za kumjulisha zitumike.
Kwahiyo wadaiwa yafaa
myajue haya ili muwe na uwezo wa kuchukua hatua stahiki.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment