NA BASHIR YAKUB -
Yapo mambo ambayo kwa mujibu wa sheria sio kujipatia mali kwa
njia ya udanganyifu. Hata hivyo polisi kwenye vituo vyao wamekuwa wakilazimisha
mambo hayo kuwa kosa hilo la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu kwasababu
wanazozijua wao, mojawapo ikiwa ni mchongo kutoka kwa mlalamikaji.
Masuala ya watu kudaiana hela ama migogoro ya ardhi kama mtu mmoja kuwauzia watu tofauti ardhi
moja si masuala ya polisi, na wala si makosa ya kujipatia pesa ama mali kwa
njia ya udanganyifu.
Tumesema mara nyingi kuwa, mamlaka ya polisi ni kushughulikia masuala ya jinai tu. Masuala ya
kudaiana hela ni masuala ya madai na sio jinai. Kwa msingi huu yapo nje kabisa
ya mamlaka yao. Masuala ya kudaiana hela yanaongozwa na sheria ya mikataba Sura
ya 345, pamoja na Sheria nyingine za fedha na rehani, wakati masuala ya migogoro
ya ardhi yanaongozwa na Sheria namba 4 na 5 za ardhi, Sheria ya Usajili wa
ardhi na nyinginezo mtambuka.
Kwahiyo makosa haya na mengine yanayofanana na haya hayawezi kuitwa
ya kujipatia mali ama fedha kwa njia ya udanganyifu. Mara nyingi makosa haya
yamekuwa yakipelekwa huko kwenye kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu kwa
makusudi ili kumkomoa mtu ili awekwe ndani nk.
Vifungu vya 301, na
302, vya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, vinaelezea kosa la kujipatia mali
kwa njia ya udanganyifu kumaanisha ujinai. Mfano wa makosa ya kujipatia mali
ama fedha kwa njia ya udanganyifu ni wale wanaotuma SMS au kupiga simu na kusema
umejishindia kitu fulani na hivyo utume hela ili upate kitu hicho, na pesa kweli
zikatumwa kwake, huku jambo hilo sio kweli. Fedha hiyo itakuwa imepatikana kwa njia udanganyifu.
Au mtu anakwambia lete hela nikuletee mali fulani au
nakuagizia japan huku akijua sio kweli. Fedha hizo akizipokea na asilete
alichoahidi zitakuwa zimepatikana kwa njia ya udanganyifu. Mifano kama hiyo ndiyo
ya kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.
Aidha, tunasisitiza tena kuwa masuala ya kudaiana hela, au
ugomvi wa ardhi hayaingii kwenye jinai ya kujipatia pesa/mali kwa njia ya
udanganyifu, bali ni madai. Na hivyo, ni kosa kabisa askari yeyote katika kituo
chochote kujihusisha na masuala ya madai, labda iwe kwa ushauri. Kama askari
atachukua masuala haya ili awashauri au awapatanishe hiyo itakua ni sawa. Ila
kama atayachukua ili afungue jalada la kesi hilo ni kosa.
Mahakama kuu ya Tanzania imeshatoa maamuzi mengi kuelezea
jambo hili na moja ya maamuzi ya hivi karibuni ni katika Madai ya Rufaa
Namba 23/2017 kati ya RIBENT RWECHUNGURA vs PONSIAN MUTAYABARWA ambapo
Jaji KAIRO alisema ni makosa
mgogoro wa ardhi kufunguliwa polisi.
Sehemu husika ambapo yafaa upeleke masuala hayo ni mahakamani
moja kwa moja. Ukiulizia mahakamani au ukampata Wakili utaelekezwa utaratibu mzima
wa hapo mahakamani.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment