NA BASHIR YAKUB -
Kampuni zote, ziwe kubwa au hata zile zenye watu wawili au zile
za familia huwa na wakurugenzi wake(Directors). Kampuni ikiwa na watu wawili
utakuta hao hao ndio wanahisa na haohao ndio wakurugenzi. Basi yote ni sawa na
inaruhusiwa kisheria.
Hata hivyo, kampuni hiyo hata kama ni ya watu wawili au ya
familia mke na mme ama vinginevyo, mkurugenzi yeyote katika hiyo kampuni
haruhusiwi kufungua kesi kwa niaba ya kampuni. Anaweza kufungua kesi kama yeye
binafsi kwa kutumia jina lake lakini si kwa niaba ya kampuni na kwa kutumia
jina la kampuni.
Kwa mfano kampuni inaitwa MECCO CO. LTD. Hawezi kufungua kesi
kwamba MECCO CO. LTD inamshitaki fulani yaani MECCO CO. LTD vs SHABAN. Hataruhusiwa
kutumia jina la kampuni namna hiyo. Hii ni hata kama kampuni imetendewa kosa fulani
ambalo kampuni ni lazima ishitaki. Bado hataruhusiwa kufanya hivyo. Na hii ni
kwa maafisa wote wa kampuni wakiwemo wanahisa,mameneja, katibu wa
kampuni(company secretary), mwanasheria wa kampuni na afisa yeyote yule wa kampuni.
Kitu pekee chenye mamlaka ya kushitaki kwa niaba ya kampuni
na kwa kutumia jina la kampuni ni maamuzi ya bodi ya kampuni(Board Resolution).
Maamuzi haya ya bodi hufanywa na wakurugenzi wa kampuni kwa niaba ya kampuni na
baada ya kupata ridhaa ya wanahisa.
Kama hakuna maamuzi ya jumla ya bodi ya wakurugenzi ya
kampuni (Board Resolution) ya kuamua
kampuni kushitaki basi mkurugenzi yeyote, ama mwanahisa, ama afisa yeyote wa
kampuni hawezi hata kidogo kushitaki kwa niaba, na kwa jina la kampuni.
Katika maamuzi ya mahakama kuu yaliyotolewa na Jaji
Maghimbi tarehe 6/3/2020 katika kesi ya ardhi No. 147/2018 kati ya Evarist
Steven Swai na Msafiri Enterpises Co. Ltd
vs The Registered Trustee of Chama cha Mapinduzi na wengine wawili,
mahakama kuu imeifuta kesi iliyofunguliwa na mkurugenzi wa kampuni kwa niaba ya
kampuni kwasababu ya kutokuwa na Maamuzi ya jumla ya bodi ya wakurugenzi(Body Resolution).
Mahakama imesema kuwa,hata kama kampuni husika inaonekana
kuwa ni ya familia, na kuwa mkurugenzi aliyefungua kwa niaba ya kampuni kuonekana
ndiye pia mwenye hisa kubwa katika kampuni hiyo kuliko wote, bado hana mamlaka
ya kufungua kesi kwa niaba na kwa kutumia jina la kampuni kama hana Maamuzi ya
jumla ya Bodi ya Kampuni(Body Resolution).
Mahakama imesisitiza kuwa alitakiwa kwanza aitishe kikao cha
wakurugenzi, wakae na watoe maamuzi kwa kuandaa nyaraka ya maamuzi ya bodi ya wakurugenzi(Body
Resolution) ambayo itakua inampa mamlaka, na kuridhia kampuni kushitaki. Kinyume
cha hivyo ni kosa ambalo adhabu yake ni kesi kufutwa,kulipa gharama, ama
vinginevyo.
Katika uamuzi huu mahakama haikuwa inatoa uamuzi mpya bali maamuzi ya namna hii ndio msimamo wa
mahakama na sheria kwa mda mrefu na hapa
ilikuwa ikisisitiza tu msimamo wake.
Sababu za kutoruhusu kila mkurugenzi,ama mwanahisa, ama afisa
mwingine kushitaki kwa niaba ya kampuni bila Maamuzi ya bodi, ni kuondoa uwezekano
wa kila mmoja kutumia jina la kampuni kushitaki jambo ambalo linaweza kuitia
hasara kampuni, lakini pia kuepuka kutumia jina la kampuni vibaya,kuepusha
kuiingiza kampuni kwenye migogoro isiyoisha nk.
Kwa wenye makampuni ambao wanahitaji kushitaki kwa kutumia
majina ya kampuni,hasa makampuni madogo ya wajasiriamali ambayo pengine kwao
hili ni geni, yawapasa wakae kikao cha wakurugenzi, wapitishe maamuzi ya
jumla(Body Resolution) ya kuruhusu kampuni kushitaki, na maamuzi hayo yawe
katika maandishi/nyaraka maalum iitwayo,”COMPANY/DIRECTORS BODY RESOLUTION”.
Nyaraka hiyo ni lazima iambatanishwe kwenye mashtaka(Plaint)
ili wakati kesi inafunguliwa iwe ushahidi kuwa maamuzi ya kampuni kushitaki
yalipitia hatua hii muhimu kisheria.
Basi tufanye hivyo.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment