NA BASHIR YAKUB -
Mtu mmoja anadai yeye amenunua kiwanja, na mwingine naye
anadai amenunua kiwanja hichohicho. Na wote hawa wawili kila mmoja anadai kuwa
ameuziwa kiwanja na mtu huyohuyo mmoja, na wote wana nyaraka za mauziano zenye
jina na sahihi za huyohuyo muuzaji.
Maelezo yote katika makala haya yatakuwa yanarejea misingi ya
sheria katika maamuzi ya mahakama kuu katika kesi ya JOVENT CLAVERY RUSHAKA NA DEVOTA
YIPYANA MPONZI dhidi ya BIBIANA
CHACHA,Land Case No. 303/2016. Makala haya yanahusu pia nyuma na
mashamba.
1.NANI MNUNUZI HALALI
KATI YA WAWILI.
Ni hivi, pale ambapo watu wawili wameuziwa kiwanja kimoja
kutoka kwa mtu mmoja basi mmiliki halali anakuwa yule aliyenunua wa kwanza. Suala
la msingi iwe tu kuwa yule aliyenunua wa kwanza awe alinunua kwa kufuata
utaratibu wa kisheria.
Ikithibika kuwa mnunuzi wa kwanza ana ushahidi wa kununua kwa
kufuata utaratibu wa kisheria basi yeye ndiye anakuwa mmiliki halali. Na hapa hata
kama baada yake kuna wanunuzi wengine kumi, bado yeye atabaki kuwa mnunuzi
halali na mmiliki halali.
Kwa msingi huu, wale waliomfuatia katika kununua watakuwa si
wanunuzi halali na hawatakiwi kudai umiliki wa kiwanja hicho. Ni muhimu kueleza
hili kwa uwazi ili watu waelewe na waache kuwa wanagombana.
2. KWANINI MNUNUZI WA
PILI HAWI HALALI.
Mnunuzi wa pili au mwingine yeyote anayemfuatia hawi halali
kwasababu hadhi ya umiliki(good title) aliyokuwa nayo muuzaji anakuwa
ameishaipoteza kwa kumuuzia yule wa kwanza. Kawaida unapokuwa na mali unakuwa
na hadhi ya umiliki(good title), hadhi ambayo unaweza ukaitoa kwa kuiuza,
kuitoa zawadi, au kuirithisha. Hadhi hiyo ukishaitoa kwa njia yoyote kati ya
nilizosema hapa kwa mtu mwingine unakuwa umebakiwa huna kitu. Maana yake ukiitoa
kwa njia ya kuuza,huna kitu tena cha kuuza baadae, labda kiwe kingine na sio
kilekile. Kwahiyo akija mtu wa pili naye ukamuuzia kitu hichohicho maana yake
umemuuzia kitu ambacho huna, na wewe mnunuzi wa pili umenunua kitu kutoka kwa
mtu ambaye hana. Tafsiri rahisi anakuwa amekuuzia hewa.
3. NAMNA YA KUTAMBUA
MNUNUZI WA KWANZA.
Namna pekee ya kujua nani mnunuzi wa kwanza na ni aliyefuatia
ni kwa kila mmoja kuonesha mkataba wake wa mauziano na kutizama tarehe. Tarehe
iliyotangulia ndiyo ya mnunuzi wa kwanza na tarehe zinazofuatia ni za wanunuzi
wengine waliofuata.
Mashahidi walioshudhudia nao ni muhimu kuthibitisha hili.
Lakini hawa ili wathibitishe ni lazima kuwe na mkataba wa mauziano. Hii ni
kwasababu sheria inakataza kununua ardhi bila maandishi. Ardhi ikinunuliwa bila
maandishi ni sawa na kusema haijanunuliwa. Kwa hiyo mashahidi watakuja kuthibitisha
tarehe iliyo katika maandishi. Hivi ndivyo
tunavyojua nani aliyetangulia kununua.
4. NINI AFANYE MNUNUZI WA PILI.
Haki aliyonayo mnunuzi wa pili au mwingine yeyote aliyefuatia
ni haki za aina mbili. Kwanza ni haki ya
madai ya pesa yake ya manunuzi kwa ukamilifu pamoja na fidia kutoka kwa muuzaji
aliyeuza mara mbili. Hili anaweza kulidai kawaida au akaitumia mahakama na atapata haki hiyo.
Haki ya pili ni kumfungulia jinai ya utapeli mtu huyohuyo
aliyeuza mara mbili. Hapa muuzaji anaweza kukabiliwa na adhabu ya kifungo,
faini, pamoja na fidia. Aidha aliyeuziwa
mara ya pili anaweza kuamua kuchukua hatua hizi zote mbili kwa pamoja, yaani
akamfungulia madai akidai kurudishiwa hela yake pamoja na fidia, na wakati huo
huo akamfikisha polisi kwa ajili ya kesi nyingine ya jinai kwa ajili ya adhabu
ya kifungo nk. Kwahiyo atachagua kuchukua mojawapo au zote mbili kwa pamoja.
Pamoja na hayo, kama inawezekana kufanya mazungungumzo na
huyo muuzaji kurudisha hela yako pamoja na fidia za usunbufu basi ni bora zaidi.
Na wakati mwingine aliyetapeliwa anaweza kufidiwa kwa kupewa kiwanja kingine
ikiwa ataridhika nacho.
5. HALI IKOJE KAMA
MNUNUZI WA PILI AMESHATAFUTA HATI MILIKI KWA JINA LAKE.
Mfano nyote mliuziwa kiwanja ambacho hakijapimwa, lakini yule mnunuzi wa pili tayari akajiwahi na
kutafuta hatimiliki, na yule mmiliki wa kwanza akabaki tu na mkataba wa
mauziano. Na tunajua pengine hatimiliki ina hadhi kubwa kuliko mkataba wa
mauziano.
Hali hii haibadilishi msimamo wa sheria katika hili. Bado
mnunuzi wa kwanza mwenye mkataba wa mauziano
anaendelea kuwa mmiliki halali dhidi ya mnunuzi wa pili mwenye hati miliki. Kwa
maana hiyo hatimiiliki yake haimsaidii chochote katika hili.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment