NA BASHIR YAKUB -
Ni muhimu ukiwa na kesi ya ardhi ambayo kwa maoni yako
unahisi mahakama haiwezi kutoa haki inavyostahili bila kulitembelea na kulijua eneo
la mgogoro(Locus in Quo) kuiomba itembelee. Sheria iko wazi na inakuruhusu
wewe kuiomba mahakama kutembelea eneo la mgogoro ili kushuhudia hicho unachotaka
iamini. Na hii haijalishi upo pande gani wa kesi, uwe mlalamikaji ama
mlalamikiwa kila upande unayo haki ya kuomba kutembelea eneo la mgogoro.
Hatua hii ni muhimu sana kwasababu itatoa picha na mwanga wa
kile ambacho unakiongelea. Itatoa taswira na ushahidi wa dhahiri. Wakati
mwingine waweza kushindwa kueleza jambo vizuri
pengine kutokana na jiografia ya eneo lenyewe, kwakuwa si rahisi
kuelezeka ama sababu nyinginezo. Lakini kwa mahakama kufika na kuona mazingira,
basi kila kitu kitajieleza chenyewe.
Hata hivyo, huwezi kuomba mahakama itembelee eneo la mgogoro
kama kesi ipo hatua ya rufaa. Hii ni kwasababu hatua ya rufaa ni hatua ambayo sheria
hairuhusu ushahidi mpya kutolewa. Kwahiyo kama unahitaji kuomba jambo hili ni
vema uliombe mapema kabisa kule kesi ilipoanzia.
Kwa mahakama za ardhi kesi inaweza kuwa imeanzia baraza la
ardhi la kata, au imeanzia baraza la ardhi la wilaya, au imeanzia mahakama kuu.
Popote itakapokuwa imeanzia unayo haki ya kuomba mahakama itembelee eneo la mgogoro
ili iweze kujiridhisha katika kile unachosema.
Aidha, sio migogoro yote ya ardhi inahitaji kutembelewa na
mahakama. Mgogoro kama umenyooka una ushahidi na mashahidi wa kuweza
kuthibitisha na kila jambo likaeleweka, basi hamna haja ya kuomba kutembelea. Lakini
ikiwa kwa mtazamo wako unaona kuna jambo hata likielezwa haliwezi kueleweka mpaka
mahakama ifike na kuona basi utaomba.
Unapoomba mahakama nayo itapima na kuona iwapo kuna umuhimu
wa kufanya hivyo ama hapana, bali kila kitu kinaweza kuishia ndani ya mahakama.
Katika kutoa uamuzi wa kutembelea ama hapana mahakama itaongozwa na misingi ya sheria
iliyowekwa ikiwemo ile iliyoelezwa katika kesi ya Evelyn Even Gardens NIC LTD and
the Hon.Minister , Federal Capital Territory and Two Others, No.FCT/HC/CV/1036/2014;Motion
No. FCT/HC/CV/M/5468/2017 .
Misingi ni pamoja na;-
Kama kutembelea eneo kutawezesha kuondoa
mashaka juu ya kinachobishaniwa, Kama mgogoro unahitaji utambuzi wa mipaka,
majirani na ukubwa au kiwango cha eneo,na
Kama ubishi unahusu hali halisi ya eneo, na jingine lolote ambalo
mahakama itapima na kuona linafaa kuisukuma itembelee.
Misingi hii pia imeelezwa katika kesi ya MARTIN MGANDO vs MICHAEL .F.
MAYANGA , Rufaa Namba 93/2019, chini ya Jaji Bahati.
Nisisitize tu kwamba mahakama inaweza kuamua yenyewe(sua
moto) kutembelea eneo la mgogoro bila kuombwa na mtu yeyote. Hata hivyo
ni muhimu wewe uliye kwenye kesi mlalamikaji ama mlalamikiwa kuwa wa kwanza
kulianzisha hili ikiwa unaona ni la muhimu. Hii ni kwasababu wewe ndiyo mwenyue
kesi ambapo matokeo mabaya ama mazuri yanakuja kwako. Kwa leo yatutoshe haya.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment