NA BASHIR YAKUB -
Unakuta umefungua shauri la ndoa, inaweza kuwa maombi ya talaka,mgawanyo
wa mali ,malezi ya watoto au vyote. Wakati huo ambapo kesi haijaanza, au
imeanza lakini haijaisha, unahisi au umeona mali za ndoa ambazo pengine zinatakiwa
kugawanywa zikiwa katika hatari ya
kuuzwa, kugawiwa,kuharibiwa,au kubadilishwa umiliki. Unaona kabisa shauri likija
kuisha patakuwa hamna kitu au kitakuwepo kidogo. Nini ufanye kisheria katika mazingira
kama haya ili kuokoa mali hizi, ili usije kukosa haki yako kesi ikiisha. Hiki
ndicho kitakachozungumzwa hapa.
Kitu unachotakiwa kufanya kimeelezwa katika kifungu cha 138( 1 ) cha Sheria
ya Ndoa. Kifungu kinasema pale ambapo mtu ataona kuna hatari ya mali
kuuzwa,kuharibiwa au kupotezwa kwa namna
yoyote ile basi atakuwa na haki ya kuomba mahakama itoe zuio la muda kumzuia
mtu yeyote kuuza,kubadili umiliki,kuharibu,kutoa zawadi au kufanya kitu kingine
chochote chenye lengo la kuathiri mali hizo.
Kitu hiki pia kimeelezwa mara nyingi na mahakama kuu pamoja
na mahakama ya rufaa katika kesi mbalimbali mojawapo ikiwa ni hii ya ELIZABETH
GIKENE vs JOHN ZAKHARIA GIKENE shauri la ndoa namba 5/2004.
Kwahiyo utakachofanya,kwanza kama shauri liko mahakama ya
wilaya, ya hakimu mkazi, au mahakama kuu na unaye Wakili anayekuwakilisha basi
mwambie kuhusu huo wasiwasi wako wa dalili za kupotezwa kwa mali lakini pia
muombe mfanye utaratibu wa zuio hili. Bila shaka mtakubaliana kuhusu hilo.
Pili,kama shauri liko katika mahakama nilizotaja hapo juu
lakini hauna Wakili anayekuwakilisha basi ni muhimu kumtafuta wakili yeyote
umweleze wasiwasi wako na umuombe akuandalie maombi ya zuio hili ili uzuie mali
wakati shauri la msingi likisubiriwa kuisha. Mtaelewana kuhusu hili na mtafanya
kama mlivyoelewana. Maombi haya ni lazima umtafute Wakili hata wa kukuandikia
tu halafu wewe ukaenda mwenyewe mahakamani, kwasababu mtu ambaye sio Wakili sio
rahisi kuandaa maombi haya.
Zaidi, kama kesi iko mahakama ya mwanzo hapa huna haja ya wakili
wala kuandaliwa maombi rasmi bali utamueleza hakimu anayesikiliza shauri lako kwa
mdomo kuhusu wasiwasi wako wa mali
kuharibiwa na utamuomba atoe zuio la muda mali zisiguswe mpaka shauri la msingi
liishe. Kama utaweza unaweza kumtajia hata kifungu cha sheria nilichotaja hapa juu pamoja na hiyo kesi
niliyoweka ambavyo kwa pamoja vinaruhusu maombi haya ya zuio. Kama utashindwa
basi mwambie tu bila kumtajia kifungu, atatoa msaada.
Mara nyingi tatizo hili la kuharibiwa mali wakati shauri
likiendelea limekuwa likiwakumba zaidi wakina mama. Anapofungua shauri kuomba
talaka au mgawanyo wa mali basi mwanaume
huanza kuuza baadhi ya mali au kuzibadilisha umiliki ili wakati shauri linaisha
mali ziwe zimeisha ili mwanamke asiambulie kitu, au kwa lengo kuwa ikifikia
ushahidi kila mali itakayotajwa na mwanamke kuwa ni ya ndoa akatae kuwa sio
yake au ilishauzwa.
Hata wanaume nao hukumbwa na tatizo hili lakini zaidi ni wanawake.
Basi hili lisikupe tabu tena kwakuwa dawa yake ndiyo hii. Na kwa taarifa mali
ikizuiwa na mahakama isiuzwe na mtu akaendelea na uuzaji au kuiharibu basi adhabu
yake ni kifungo miezi sita jela kwa kuidharau mahakama, lakini pia yule
aliyenunua anakuwa amepoteza hela yake kwakuwa amenunua mali ambayo imezuiwa na
mahakama na hivyo batili. Basi tuchukue
hatua.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE. ” 0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment