NA BASHIR YAKUB-
Unaweza kukubali kosa polisi au popote kama serikali za
mitaa,sungusungu,nk na baadae kulikataa
kosa hilo uwapo mahakamani. Kitu hiki sio jambo la kushangaza na tayari sheria
ilishaweka mazingira ya jambo kama hili.
Makala haya hayalengi kuwaelekeza wahalifu mbinu bali kueleza
sheria inavyosema.
Wapo watu wengi ambao akiwa chini ya ulinzi wa polisi au wananchi
wenye hasira hujikuta analazimika au analazimishwa kukiri kosa. Na kwasababu ya
mazingira mtu hujikuta amekiri hata kama hakutenda ili kunusuru maisha yake kwa
wakati huo.
Lakini pia wengine huwa wamepigwa sana hasa huko mahabusu za polisi.
Ni katika mazingira ya namna hii ambapo mtu anaweza kukiri lakini baadae mahakamani
akakataa.
Hata hivyo nitoe angalizo na msisitizo kuwa si vyema kukiri
kama kweli hujatenda kosa, itokee tu katika mazingira magumu na ya kulazimishwa.
Hii ni kwasababu kunaweza kukawa na ugumu wa kujinasua katika kukiri huko mbeleni
mahakamani.
Aidha, yapo maamuzi mengi ya mahakama kuu na ya rufaa
yanayoongelea kukiri polisi na kukataa mahakamani ila tuangalie haya mapya katika kesi ya jinai namba 6/2017
kati ya JAMHURI dhidi ya MUHANGWA SIMON
mahakama kuu ya Bukoba chini ya Jaji I.C. Mugeta iliyotolewa maamuzi hivi
karibuni tarehe 25/9 /2019.
Katika kesi hii mtuhumiwa Muhangwa alikiri kosa la kuua mbele
ya polisi huko Biharamulo na akaandikishwa maelezo ya kukiri mbele ya hakimu wa
mahakama ya Mwanzo huko Biharamulo. Alipoletwa mahakama kuu mjini Bukoba kwa
ajili ya kusikilizwa kesi yake akakataa kuwa hajawahi kukiri.
Kawaida katika mazingira kama haya mahakama hujielekeza
katika misingi mikuu mitatu ambayo hutakiwa kuthibitishwa na upande wa
mashitaka ili kuonesha kuwa mtuhumiwa ameamua tu kubadilika lakini alikiri
kweli.
Upande wa mashitaka ndio wenye wajibu wa kuitosheleza mahakama kupitia
misingi hii kuwa mtuhumiwa alikiri japo sasa anakataa kuwa hakukiri.
Misingi hii ya mahakama nitaieleza ili ikusaidie ikiwa ikatokea ukalazimika kukiri na baadae
kukataa, uweze kujua wanaokushitaki wanatakiwa
kuthibitisha nini, au wewe uwahoji/uwaulize nini na katika lipi. Misingi
yenyewe ni kama ifuatavyo ;
MOSI, wanaokushitaki wawe na ushahidi mwingine unaojitegemea
unaoonesha kuwa kweli umetenda kosa(collaboration). Wasitegemee ushahidi huu wa
kukiri pekee kwasababu huo tayari umeishaukataa. Watafute ushahidi mwingine wa
kuusaidia huu kuonesha kuwa hata kama umekataa kuwa ulikiri bado kuna hili na
lile linakuingiza kwenye kutenda kosa.
Ni wajibu wako kuwahoji kuhusu uwepo wa
ushahidi mwingine tofauti na huu wa kukiri. Wakikosa basi kukiri kwako kunakosa
nguvu na hivyo kuleta uwezekano wa kuachiwa huru.
PILI, wanaokushitaki wathibitishe kuwa ulikiri bila
kulazimishwa. Hii ni kasababu kukiri kwa kulazimisha au kushawishiwa ni sawa na
kuwa hujakiri/hukukiri. Wathibitishe kuwa hakukuwa na kulazimishwa. Hapa pia na
wewe unayo kazi ya kufanya.
Kazi yenyewe ni kujitahidi kuonesha mazingira ya kulazimishwa
kukiri mfano alama za kipigo na mateso mwilini mwako, au mazingira ya hatari
kama kuzingirwa na wananchi wenye hasira, au kundi, na mazingira mengine
yanayofanana na hayo. Ukifanikiwa katika hili basi umefanikiwa kufuta kukiri
kwako na umekaribia kuachiwa huru.
TATU, wanaokushitaki wathibitishe kuwa ulichokiri ulikuwa ukimaanisha hicho na si vinginevyo. Kwa
maana kuwa kukiri kwako hakukulenga kitu kingine chochote bali lile kosa uliloshitakiwa nalo. Hii ni
kwasababu waweza kuwa ulikiri lakini hukuwa umeelewa kile unachokiri.
Ni kazi yao wanaokushitaki kuthibitisha
kuwa ulichokiri ulilenga kosa husika, lakini pia ni wajibu wako kama ulikiri bila
kuelewa kuonesha kuwa hukuwa umeelewa
unakiri nini au mazingira hayakuwa rafiki kukupa nafasi ya kuelewa ulichokuwa
unakiri.
Kwa ujumla wakishindwa kuthibitisha lolote katika haya matatu
niliyoeleza basi ni shaka la msingi katika ushahidi wao hata kama ulikuwa
umekiri yafaa mahakama ikubaliane na wewe
kuwa hukukiri na uachiliwe huru.
Mwisho, kukiri nilikoongelea hapa kunajumuisha maelezo
unayoandika polisi(cautioned statement),na yale yote unayoandika au kusaini
popote nje ya mahakama kabla kesi yako kuanza(extra judicial statement).Hivi
ndivyo sheria inavyotaka.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE. ” 0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
Asante !