NA BASHIR YAKUB-
Kifungu cha 265 cha Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai kinataka kesi zote za jinai mahakama
kuu ziendeshwe kukiwa na usaidizi wa wazee wa baraza, kadhalika kifungu
cha 7 cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu kinataka hivyo kwa upande wa
mahakama za mwanzo.
Kifungu cha 177cha Sheria ya Ushahidi kinaruhusu wazee wa baraza kuuliza
maswali mashahidi wakati wa kesi. Huku Kifungu
cha 290 cha Sheria ya Ushahidi kikiruhusu
Wakili na wahusika katika
kesi(parties) kwa maana ya mshitaki na
mshitakiwa kuhojiana maswali.
Tumeona kifungu cha 177 kikiruhusu wazee wa baraza kuuliza maswali
wakati tukiona hiki cha 290 kikiruhusu Wakili pamoja na mshitaki na mshitakiwa
kuhojiana maswali. Kisheria kuna tofauti ya kuhoji maswali(cross examine) na kuuliza maswali(ask or put questions).
Na tofauti ni hiyo kuwa katika vifungu hivi wazee wa baraza
wameruhusiwa kuuliza, wakati mawakili na wahusika wa kesi wakiruhusiwa kuhoji.
Kuhoji ni kuuliza maswali ya kumchanganya shahidi, maswali ya
mitego, maswali yaliyo nje na muktadha wa kesi ili kumvuta shahidi,na maswali mengine ambayo
hayajanyooka. Hata maswali yaliyonyooka yanaruhusiwa pia katika kuhoji. Anayehoji(cross
examine) ana uwanja mpana wa kuhoji chochote. Kwake mbingu ndio mpaka wa kuhoji.Huku
ndiko kuhoji.
Wakati kuuliza kwa mujibu wa tafsiri ya kifungu cha 177 Sheria
ya Ushahidi ni kuuliza maswali yaliyonyooka tu na kuepuka swali lolote lenye
lengo la kumchanganya shahidi. Ni maswali yanayolenga kupata ufafanuzi tu katika
kile alichosema shahidi.
Hii ndiyo tafsiri iliyotolewa na majaji watatu wa mahakama
ya rufaa Jaji Msoffe,Rutakangwa, na Bwana katika rufaa namba 147/2008 kati ya MATHAYO
MWALIMU na MASAI RENGWA dhidi ya JAMHURI.
Ni makosa wazee wa baraza kuvaa joho la uwakili au joho la
mshitaki na mshitakiwa na hivyo kuanza kuhoji maswali. Hii imekua kawaida sana
hasa mahakama za mwanzo ambapo wazee wa baraza wamekuwa wakihoji kufikia hatua
ya kupandisha jazba kana kwamba naye ni
mhusika katika kesi.
Lakini pia wamekuwa wakihoji watuhumiwa katika staili ya
uwakili. Yote haya ni makosa.
Iwapo jambo kama hili limekukuta basi hii inaweza kuwa sababu
ya rufaa kuwa hukutendewa haki kwa kuhojiwa na wazee wa baraza.
Wazee wa baraza
wanatakiwa kubaki na kazi yao ambayo ni kuuliza,kushauri(opinion) huku kazi
uwakili ya kuhoji na ile ya kuamua ya uhakimu/ujaji kuwaachia wenyewe. Wakati mwingine
watuhumiwa hufokewa na wazee wa baraza. Hii si sawa na yafaa ifahamike hivi ilivyoelezwa
humu.
Kitu ambacho unaweza kufanya kama wewe ni mtuhumiwa na mzee
wa baraza akakuhoji, au kupaza sauti kwa ukali yafaa umueleze kuhusu wajibu
wake na uiombe mahakama iyaandike na kuyaingiza kwenye kumbukumbu hayo uliyomueleza.
Na usisitize yaandikwe kweli kwakuwa iwapo utapatikana na hatia hayo yanaweza
kuwa sababu yako ya rufaa.
Mwisho, mahakama ya rufaa katika kesi niliyotaja hapo juu imeshauri
muda wa wazee wa baraza kuuliza maswali. Sio wakati wote watauliza maswali bali
katika muda maalum. Mahakama ya rufaa imependekeza wazee kuuliza maswali mwishoni
kabisa baada mawakili kufunga kumhoji shahidi(re-examination) au kama hakuna mawakili
baada ya mshitaki na mshitakiwa kumaliza kuulizana maswali.
Wasiulize muda wowote au kumuingilia na kumkatiza shahidi wakati
akieleza au akijibu Swali. Wasubiri wanaohojiana wamalize ndipo waje kuuliza. Tuyazingatie
haya.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE. ” 0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment