NA BASHIR YAKUB -
Warithi halali ni pamoja na
watoto wa marehemu na wake/mke wake halali. Kanuni ya 31 Sheria ya Wosia(1963),Tangazo
la Serikali Namba 436/1963 inazitaja
sababu 3 ambazo mtoa wosia anaweza kuzitumia kumnyima mrithi halali haki ya urithi
kama ifuatavyo ;-
MOSI, ikiwa mrithi amezini na mke wa mwenye kutoa
wosia. Mathalan, mtoto wa kiume amezini na mke wa baba yake.
PILI, ikiwa mrithi amejaribu kumuua au amemshambulia
au kumdhuru mtoa wosia au amefanya hivyo kwa mke wa mtoa wosia.
TATU, ikiwa mrithi bila sababu za msingi
hakumtunza mtoa wosia katika shida ya
njaa au ugonjwa.
Ipo sababu nyingine ya kuwa
mrithi ameharibu mali ya mtoa wosia, lakini sheria inasema sio sababu ya
kumnyima bali apewe halafu kile alichoharibu kikatwe kwenye mgao wake.
Basi, nje ya hizo sababu huwezi
kumnyima mrithi halali urithi. Haijalishi mali ni zako, watoto ni wako na kila
kitu ni chako. Na hii ni kwasababu WOSIA ni zao la sheria na hivyo kuandaliwa
kwake, kuhifadhiwa kwake, na kutekelezwa kwake ni lazima kufuate sheria. Wosia
sio suala la matakwa ya mtu 100% kama wengi wanavyojua, bali matakwa ya sheria
kwa karibia 100%.
HATUA 2 ZA KUMNYIMA URITHI
MRITHI HALALI.
Ikiwa ni halali kwa vigezo hivyo
hapo juu kumnyima mrithi halali urithi basi mtoa wosia kabla hajafanya hivyo ni
lazima atekeleze haya mawili ;-
KWANZA, awe amempa nafasi ya kujitetea mrithi anayelenga
kumnyima. Hata hivyo, hili si lazima kwa mujibu wa maamuzi katika kesi ya PAULO
FERDINAND vs F. BIGUTU(1968) HCD Na. 29. Anaweza kumpa nafasi ya
kujitetea kabla hajafa au asimpe.
PILI,ikiwa ataamua kumnyima/kuwanyima ni LAZIMA wosia uwe
umeeleza sababu za kwanini mrithi/warithi wamenyimwa. Hii ni lazima kwa mujibu
wa kanuni ya 34-39 ya Sheria ya Wosia(1963),Tangazo la Serikali
Namba 436/1963. Ni lazima mtoa
wosia/marehemu awe ameeleza katika wosia wake sababu za kwanini fulani na fulani ameamua kuwanyima.
Nini matokeo ikiwa mtu/watu
wamenyimwa urithi katika wosia na sababu hazikuelezwa.
Kanuni ya 38 ya Sheria ya Wosia(1963),Tangazo la Serikali Namba 436/1963 inatujibia . Inasema
kuwa ikiwa mrithi halali amenyimwa urithi katika wosia, na wosia huo haukueleza
sababu ya kumyima au umeeleza sababu lakini zisizokuwa za msingi, kwa maana si
zile zinazotajwa na sheria(tulizoona hapo juu), basi wosia huo UNAVUNJWA.
Nini matokeo ya kuvunjwa kwa
wosia.
Kanuni hiyohiyo inasema kwamba wosia
unapovunjwa basi mali zote zinaanza kugawiwa
upya kama vile ambavyo marehemu angekuwa
amefariki bila kuacha wosia.
Ni upi utaratibu wa kugawa mali
upya kama marehemu hakuacha wosia.
Kama marehemu alikuwa mkristo Sheria
ya Urithi ya India ya 1865 ( Indian Succession
Act 1865) itatumika kugawa mali zake. Ambapo kwa mujibu wa kifungu cha
27 cha sheria hiyo mgao utakuwa hivi ;-
MOSI,kama mume amefariki
na akaacha mjane na watoto basi moja ya tatu ( 1/3) ya mali zote za
marehemu zilizo kwenye mirathi anatakiwa
apewe mke wake(mjane). Mbili ya tatu( 2/3)
ya mali hizo zote itaenda kwa watoto wake wote.
PILI, kama hakuna watoto walioachwa na marehemu katika familia husika lakini kuna mjane,mali ya marehemu hugawanywa
katika mtindo ambao ndugu hupewa nusu (1/2), na mjane hupewa nusu ya mirathi ya marehemu(1/2). Hii
ni sawa kwa sawa. N.k., n.k…………
Kama marehemu alikuwa
mwislamu basi sheria
ya kiislam(Quran na Hadith)
vitatumika kugawa mali zake.
Kadhalika, kama marehemu hakuwa
mwislam wala mkristo bali mtu wa mila basi sheria ya kimila ya THE
LOCAL CUSTOMARY LAW (DECLARATION) ORDER 1963 itatumika kugawa mali zake
sambamba na taratibu za mila za kabila/koo
yake.
Nani ana mamlaka ya kugawa mali
upya.
Kanuni ya 39 ya Sheria
ya Wosia(1963) inatujibia kuwa wana ukoo wanaweza kufanya hiyo kazi
kama kuna maelewano, au mahakama yenye mamlaka.
Nisisitize kuwa WOSIA au MIRATHI
ambayo haikufuata au haikurandana na sheria inavyotaka ni BATILI. Na zaidi, ni kweli mali ni zako, watoto ni wako, na kila
kitu ni chako ila zingatia kuwa WOSIA na taratibu za MIRATHI sio zako, ni za sheria
na lazima utii, au ujiandae WOSIA wako
kutofuatwa baada ya kifo chako.
MWISHO lakini si kwa umuhimu, makala haya hayamlengi
yeyote au tukio lolote lililotokea katika jamii yetu hapo nyuma, hivi karibuni,
au hapo baadae.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE. ”. 0784482959,
0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment