NA BASHIR YAKUB -
Walioshitakiwa
walikuwa 13, SP Christopher Bageni, ACP Abdallah Zombe, ASP Ahmed Makele, PC
Noel Leornard, WP 4593 Jane Andrew, CPL Nyangerela Moris, PC Michael Shonza,
CPL Abeneth Saro,DC Rashid Mahmoud Lema, CPL Emmanuel Mabura,CPL Felix Sandys
Cedrick , CPL Rajab Hamis Bakari, na CPL
Festus Philipo Gwabisabi.
Kwanini wameshitakiwa watu wote hawa halafu mtu mmoja
ndiye aliyepatikana na hatia na akahukumiwa kunyongwa, tutaona hapa.
Kwa kumbukumbu kesi hii ilianzia mahakama kuu ya Tanzania
mbele ya Jaji Massati JK. Wakati upande wa mashtaka ukifunga kesi
yao mahakama ikawaondoa watuhumiwa
watatu PC Noel Leornard, CPL Nyangerela
Moris na CPL Felix Sandys Cedrick kwa
kuwaona hawana kesi ya kujibu na hivyo ikaona hakuna haja ya kuwataka kujitetea
na kuendelea kuwa katika kesi.
Kwahiyo wakabaki 10 ambao sasa walikutwa na kesi ya
kujibu na hivyo kesi ikaendelea na hao 10 ikiwemo Bageni. Wakati wameanza
kujitetea mmoja wao hao 10 DC Rashid Mahmoud Lema alifariki na hivyo kesi yake
ikaishia hapo na sasa idadi ikabaki 9.
Mwisho wa kesi hapo
mahakama kuu Jaji Massati aliwaachilia huru watuhumiwa wote 9 waliokuwa
wamebaki kwa kuwaona hawana hatia. Moja ya hoja kubwa ya kuachiliwa kwao huru
ilikuwa kwamba kati ya wote hao 9 waliobaki katika kesi hiyo hakuna hata mmoja
kati yao iliyefyatua risasi na kuua.
Ikumbukwe aliyefyatua risasi na kuua ni CPL Saad
ambaye hakuwahi kufikishwa mahakamani baada ya kutoroka mapema liliposanuka. Kwahiyo
mahakama kuu iliona kutokuwepo kwa CPL Saad ili atiwe hatiani kwa kuua au
amtaje mtu mwingine aliyempa amri ya kuua ili wote wahukumiwe kwa kosa moja,
iliona ni udhaifu ambao unatosha kuwaachilia watuhumiwa wote 9, na iliwaachilia
wote huru.Kwa ufupi iliona hakuna kinachowaunganisha na mauaji zaidi ya tu kuwa
walikuwa kwenye tukio.
Serikali/Jamhuri haikuridhishwa na uamuzi huo na hivyo
ikakata rufaa mahakama ya rufaa ikipinga hukumu hiyo dhidi ya watuhumiwa wote 9
walioachiliwa. Rufaa ikasajiliwa kwa namba 358/2013. Rufaa ilipangwa kwa majaji
watatu Jaji Luanda, Jaji Mjasiri na Jaji Kaijage.
Wakati rufaa inapangwa kusikilizwa serikali/Jamhuri ikawafutia rufaa watuhumiwa
watano WP 4593 Jane Andrew, CPL Emmanuel
Mabura, PC Michael Shonza, CPL Abeneth Saro na CPL Festus Philipo Gwabisabi.Kwahiyo kwenye idadi ya wale 9 wakabaki wanne ACP
Abdallah Zombe, SP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makele na , CPL Rajab Hamis
Bakari.Hivyo rufaa ya mahakama ya rufaa ikaendelea na hawa wanne.
Rufaa ilisikilizwa na mwisho mahakama ikawaondoa
watatu ACP Abdallah Zombe, ASP Ahmed
Makele na , CPL Rajab Hamis Bakari kuwa
hawana hatia na ikawaachilia huru, ikabaki na mmoja SP Christopher Bageni
ambaye ilimkuta na hatia na ikaamuru kunyongwa kwake hadi kufa.Kumbuka mahakama
kuu ilimwachilia huru. Ni mahakama ya rufaa iliyobadilisha maamuzi haya kutoka
kuachiliwa huru hadi kunyongwa.
KWANINI BAGENI
ANYONGWE NA WENZAKE WAACHILIWE HURU.
Mahakama Kuu.
Kumbuka mahakama kuu ilimuachilia Bageni kwasababu kuu
mbili. Kwanza siye aliyefatua risasi, na pili yule aliyefyatua risasi CPL Saad
hakufika mahakamani kumtaja Bageni kuwa ndiye aliyemuamrisha kupiga risasi ili wote wawe na hatia sawa.
Hii ni kwasababu kwa mujibu wa Kifungu cha 22 cha
Kanuni za Adhabu aliyetenda kosa kama vile CPL Saad alivyopiga risasi, na
aliyeamrisha(saidia) kutendwa kosa wote hatia yao ni moja. Kama ni kunyongwa ni
wote na kama ni kifungo ni wote.
Kwa msingi huu mahakama kuu haikumuona Bageni
akifyatua risasi kwasababu sio yeye aliyefyatua risasi na hivyo upande huo akaondolewa, lakini pia haikumuona
akiamrisha risasi kufyatuliwa kwasababu aliyefyatua hakuwapo mahakamani kumtaja kuwa ndiye aliyemwamrisha kufyatua na
hivyo upande huo pia nako akaondolewa.
Mwisho akaonekana haingii popote kwenye
kosa basi akaachiliwa huru.
Mahakama ya
Rufaa.
Mahakama ya rufaa haikukubaliana na uchanganuzi huo wa
mahakama kuu na hivyo ilimuona Bageni
ana hatia. Ilisema ni kweli Bageni siye aliyefyatua risasi, lakini kifungu cha
22 cha Kanuni za Adhabu kuhusu kutoa kwake amri kinamuingiza hatiani.
Ilisema kwamba
ushahidi wa kimazingira unathibitisha wazi kuwa alitoa amri. Ushahidi wenyewe wa kimazingira uliionwa na
mahakama ya rufaa ni kama ifuatavyo ;
KWANZA, katika askari wote waliokuwa
kwenye tukio yeye ndiye aliyekuwa na cheo kikubwa kuliko wote na hivyo yeye
ndiye aliyekuwa kiongozi wa amri zote
katika matukio yote yaliyotokea eneo hilo hata pasingekuwepo na shahidi
wa kusema alimuona anatoa amri.
PILI, walipokuwa wamewakamata
wafanyabiashara waliouliwa katika barabara ya SAM NUJOMA yeye ndiye
aliyeamrisha msafara wa magari mawili Defender na Pajero kuelekea msitu wa
PANDE(ushahidi
wa mtuhumiwa wa 4 CPL Rajab Hamis Bakari ).
TATU, mtuhumiwa wa 4 CPL Rajab
Hamis Bakari anasema walipofika msitu wa PANDE Bageni alishuka kwenye gari
akamuachia radio call . Wakati amekaa ndani ya gari akiwa amebaki na
dereva kwa jina FRANK alisikia kupitia radio call aliyoachiwa milio
ya risasi. Ikabidi ashuke kuelekea Bageni alikoelekea.
Alipowakaribia alimuona CPL
Saad akiwa anamalizia kumpiga risasi mfanyabiashara wa mwisho,wengine wakiwa
wameshauliwa wamelala chini huku Bageni akiwa amesimama anatazama.
NNE, baada ya wafanyabiashara kuuliwa,
ni Bageni aliyeamuamrisha dereva SGT James kubeba maiti na kuzipeleka Muhimbili(ushahidi
wa mtuhumiwa wa 4 CPL Rajab Hamis Bakari na Sgt James ).
Kwa mazingira haya mahakama ya rufaa ikaona kwa vyovyote
vile hata kama CPL Saad hayupo mahakamani kumtaja Bageni kuwa ndiye aliyetoa
amri ya kuua, bado mazingira yote yanaonesha yeye ndiye aliyetoa amri na hivyo
kuwa na kosa sawa na CPL Saad aliyekimbia.
Zaidi, mahakama
ya rufaa ikazingatia haya kwa Bageni ;
MOJA, kwanini Bageni aamrishe
wafanyasbiashara kupelekwa huko mbali kote PANDE tena kwenye msitu ambako hakuna nyumba wala kituo cha polisi. Nia
ya kuwapeleka huko ilikuwa nini hasa. Jibu likawa ni mpango wa kuwadhuru tu
bila shaka.
MBILI, Bageni alisema kuwa walikuwa
wakijibizana kwa risasi na marehemu
maeneo ya Sinza kwenye ukuta wa Posta. Ushahidi na mashahidi wote
akiwemo shahidi wa 20 Kisa Mohammed mlinzi wa ukuta huo wa posta alithibitisha
kuwa hakuna majibizano yoyote ya risasi yaliwahi kutokea eneo hilo. Swali
lilikuwa uongo huo ulitungwa kwa lengo lipi.
TATU, Bageni alionesha makasha tisa ya
risasi na kusema kuwa makasha hayo yalitokana na risasi zilizotumika katika
majibizano na wafanyabiashara waliouliwa maeneo ya Sinza. Wakati ushahidi wa
mtuhumiwa wa 4 CPL Rajab Hamis Bakari unaonesha kuwa makasha hayo yalitokana na
risasi zilizofyatuliwa hovyo hewani maeneo ya Bunju na zilifyatuliwa na CPL Saad na DC Rashid na baada ya kufyatuliwa Bageni aliwaamrisha wamkabidhi makasha hayo ambayo ndiyo aliwasilisha mahakamani. Swali
kwa mahakama ni lengo la kufyatua risasi
hovyo hewani na kuchukua makasha lilikuwa
ninini.
Kwa kuzingatia haya na hayo niliyotangulia kueleza
mahakama ya rufaa ikapigilia msumari kuwa Bageni si tu alitoa amri ya kuuliwa
wafanyabiashara bali pia aliandaa mazingira ya ushahidi ili kukwepa mkono wa
sheria.
Kwa shahidi hizi mahakama ya rufaa ikafuta uamuzi wa mahakama kuu wa
kumuona Bageni hana hatia, na ikatangaza uamuzi mpya wa kumkuta na hatia ya kuua
kwa kukusudia na hivyo kuamuru anyongwe hadi KUFA.
BAGENI AOMBA
UAMUZI WA KUNYONGWA KWAKE KUREJEWA.
Hii ndo ile ya juzi ambayo mlisikia. Basi ni hivi, mahakama
ya rufaa ndiyo mahakama ya mwisho katika kutoa maamuzi. Hakuna rufaa nyingine
baada ya maamuzi yake inakuwa imetosha na imetosha. Umeridhika, hukuridhika
uamuzi ukitoka hapo biashara imekwisha.
Hata hivyo, Sheria Mamlaka za Rufaa, Sura ya 141
kifungu cha 4(4), pamoja na Kanuni za Mahakama ya Rufaa zaMwaka 2009 , Kanuni ya 66(1)( a ) ( b ) zinatoa nafasi ya mwisho kwa mtu ambaye
hakuridhika na maamuzi ya mahakama ya rufaa kuomba MAREJEO hapohapo mahakama ya
rufaa.
MAREJEO ni maombi ya kuiomba mahakama ileile iliyotoa hukumu kupitia tena
maamuzi yake ili kujiridhisha na nukta kadhaa ambazo muombaji atakuwa
ameziainisha. Utaiomba mahakama chini ya majaji wengine tofauti na
wale waliotoa uamuzi wa kwanza kurejea tena na kuangalia vile vitu ambavyo
unadhani umeonewa.
Kesi ya BABU SEA nayo ilifikia hatua hii lakini
ikashindikana.Kwa Mawakili wanajua kuwa hii ni hatua isiyowezekana siku zote
labda iwe vinginevyo.
Kwahiyo hukumu
mliyoisikia juzi ni matokeo ya MAREJEO yaliyoombwa na Bageni ambayo ni namba
63/2016 chini ya majaji wengine watatu Jaji Mugasha, Jaji Wambali, na Jaji Kerefu.
Bageni alikuwa na hoja kuu mbili za kurejea, kwanza
kuwa hakupewa nafasi ya kusikilizwa na
pili kuwa mahakama ya rufaa wakati inasikiliza rufaa yake iliibua vitu vipya
ambavyo havikuwa sehemu ya kesi kule mahakama kuu.
Kwa ufupi majaji hawa walimsikiliza hoja zake kupitia
kwa wakili wake Gaudiosus Ishengoma, na wakasikiliza hoja kinzani kutoka upande
wa serikali/Jamhuri uliowakilishwa na Wakili Ladislaus Komanya na kusema kwamba
Bageni hana hoja za msingi na anacholalamikia hakina mashiko.
Kwa uamuzi huu majaji hawa Jaji Mugasha, Jaji Wambali,
na Jaji Kerefu wakakubaliana na uamuzi wa majaji wa mwanzo wa mahakama
hiyohiyo Jaji Luanda, Jaji Mjasiri na
Jaji Kaijage kuwa Bageni anastahili kunyongwa hadi KUFA. Hivi ndivyo SP
Christopher Bageni alivyobaki peke yake kati ya watu 13 alioshitakiwa nao.
Kwa kumbukumbu tarehe 14 / 1 / 2006 wafanyabiashara
wanne wa madini Ephraim Sabinus Chigumbi,Sabinus Chigumbi, Juma Ndungu na
Mathias Lunkombe waliuliwa na kuporwa madini na fedha taslim walizokuwa nazo katika
msitu wa PANDE Kinondoni Dar es salaam, mauaji yaliyotekelezwa na watuhumiwa
waliotajwa humu kwa kisingizio kuwa wafanyabiashara hao ni majambazi.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE. ”. 0784482959,
0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment