Na Bashir Yakub.
Wiki iliyopita niliandika kuwa ujenzi wa fensi pekee kwenye
kiwanja sio maendelezo halisi kwa mujibu wa kanuni mpya za sheria ya ardhi
tofauti na tulivyozoea. Leo tena tunatizama Sehemu ya (iii) kanuni ya 7 ya
kanuni mpya kanuni za Sheria ya Ardhi kupitia tangazo la serikali namba 345 la tarehe 26/ 4
/ 2019.
Kanuni ya 7(1) inasema kuwa mwenye kiwanja/shamba ambalo
halijaendelezwa au lenye maendelezo hafifu,endapo ataomba mkopo na kuweka
rehani ardhi hiyo, atatakiwa ndani ya miezi sita tokea siku alipoweka rehani,
apeleke taarifa kwa kamishna wa ardhi kuonesha ni namna gani pesa yote au sehemu ya pesa alizokopa
zimetumika katika kuendeleza ardhi husika.
Kutokana na kanuni hii maana yake ni kuwa ardhi unayokopea
inatakiwa kuwa imeendelezwa au kama haijaendelezwa basi kiasi cha pesa
unachopata kupitia mkopo lazima kitumike kuendeleza ardhi hiyo uliyotumia
kukopea bila kujali umekopa hela ili kuzifanyia nini. Na hii ni kwa ardhi zenye
hatimiliki. Mwenye ardhi atatakiwa ndani ya miezi sita tokea kuweka ardhi yake rehani apeleke taarifa
maalum kwa kamishna wa ardhi kuonesha ni namna gani hela yote au sehemu ya hela
aliyoipata ilivyotumika kuendeleza ardhi aliyoweka rehani.
MFANO, una kiwanja chenye hatimiliki, lakini hakijaendelezwa(un-developed)
au kimeendelezwa lakini maendelezo hafifu(under-development) kama kujenga fensi
tu, au kijumba kibovu cha mlinzi nk.Sasa unaomba mkopo benki wa Tsh milioni 50 na
rehani yako ni kiwanja hicho. Benki wao watatizama na kuona kuwa kiwanja
unachoweka rehani hakijaendelezwa au kina maendelezo hafifu.
Watakueleza sharti hili la sheria mpya kuwa aidha ukiendeleze
halafu ndio uje kwao kuchukua mkopo au wakipokee hivyohivyo kama rehani lakini
kuwe na makubaliano maalum kuwa ndani ya miezi sita kiasi kutoka hiyo milioni
50 wanayokupatia itatumika kuendeleza kiwanja, na wao hilo watalisimamia
kuhakikisha linafanikiwa kwakuwa bila kiwanja kuendelezwa mkopo utakuwa batili
na wao watapoteza.
Kama utakubali utapata mkopo kama utakataa hautapata mkopo
kwasababu bila hivyo mkopo utakuwa batili kwa mujibu wa mabadiliko haya ya sheria.
Hivi ndivyo itakavyokuwa.Tafsiri kwa ujumla wake ni kuwa ardhi ambayo haijaendelezwa
au ina maendelezo hafifu kama kujenga fensi nk. haiwezi tena kutumika kukopea
hata kama ina hatimiliki.
Aidha, kama benki wataamua kukupatia mkopo kwa masharti
ya kuendeleza basi ndani ya miezi sita
tokea upokee mkopo huo ni lazima kupelekwa taarifa maalum kwa Kamishna wa ardhi
kuonesha ni namna gani mkopo huo umetumika kuendeleza ardhi iliyowekwa rehani,
na hii ni hata kama mkopo huo unatoka kwa mafungu(installment).
Pia, hii yote haijalishi unakopa ili hizo hela ukazifanyie
nini. Hata kama unataka kununua gari, au kufungua biashara, sharti ni kuwa kiasi
cha hela kitoke kuendeleza ardhi. Kazi itabaki kwako umekopa kiasi gani, kiasi
gani utumie kuendeleza ardhi, kiasi gani kitabaki kwa ajili ya biashara zako,
na kama hilo kwako litawezekana ukarudisha hela ya watu ikiwa salama baada ya
kuikata kata hivyo.
Zaidi, taarifa ya namna pesa ilivyotumika kuendeleza eneo
itakuwa katika fomu maalum ambayo imeanzishwa na sheria hiyo fomu namba 551.
Mwisho udanganyifu wowote katika mchakato huu ni jinai inayoweza
kukupeleka jela kwa kifungo kisichozidi miaka miwili au faini, au vyote viwili
kwa mujibu wa kanuni ya 9.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE. ”. 0784482959,
0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment