NA BASHIR YAKUB -
Watu wengi wamekuwa wakijiuliza ikiwa mmoja wa wanandoa aliyepelekea
ndoa kuvunjika kama anastahili mgao wa mali. Mfano,mwanamke katika ndoa
anaanzisha chokochoko makusudi ili ndoa ivunjike apate mgao wa mali aendelee na
maisha yake. Au mwanaume kwa tabia zake mbaya za ulevi au kutokuwa
mwaminifu anapelekea ndoa kuyumba hadi
kuvunjika kabisa. Je kwasababu amesababisha matatizo na ndiye chanzo cha tatizo
mpaka ndoa kuvunjika anastahili mgao wa mali ?.
Mara nyingi tumeeleza kuhusu ndoa kuvunjika na misingi ya
kugawana mali ambayo imewekwa na sheria hususan Sheria ya ndoa. Kifungu cha 114
cha Sheria ya ndoa kwa ujumla kinaeleza misingi ya kuzingatia wakati wa
kugawana mali ndoa inapovunjika. Lakini kifungu hichohicho kifungu kidogo cha 2(b)
kinaeleza kwa umahsusi kuwa kitu kikubwa ambacho kinapaswa kuzingatiwa wakati
wa kugawana mali ni mchango wa kila mwanandoa katika kupatikana kwa mali husika.
Yaani ni swali la mwanandoa amechangia nini mpaka hii mali imepatikana.
Tafsiri ya mahakama kuhusu mchango wa mwanandoa katika
kupatikana mali ni pamoja na mchango wa pesa, mchango wa kazi(nguvu), pia kazi
za nyumbani ambazo mara nyingi hufanywa na mwanamke kama kufua, kupika, kulea
watoto, kutunza nyumba nazo zinahesabika ni mchango katika kupatikana mali
ambazo zitachumwa na mwanaume moja kwa moja huko kazini anakoenda.Hii ni tafsiri
katika rufaa namba 9 ya 1983, TLR 32 katika
kesi maarufu ya Bi Hawa, ikifuatiwa na utitiri wa tafsiri nyingi kama hizo
kutoka mahakama kuu na ya rufaa. Huu ndio msimamo wa sheria na haya tumeyarudia
mara nyingi.
Swali kuu la mada ni ikiwa aliyeleta chokochoko mpaka ndoa
kuvunjika kama naye anastahili kupata mgao wa mali, au asipate kabisa kwakuwa
ndiye aliyeleta ugomvi, au apate kidogo. Mahakama kupitia kesi ya ROBERT ARANJO
v ZENA MWIJUMA ( ) [1985] TZHC 5; (14 March 1985); 1984 TLR 7 (TZHC) itatujibia
swali hili. Katika kesi hii mkata rufaa ambaye ni mwanandoa ndugu Robert Aranjo
alikata rufaa mahakama kuu ikiilalamikia mahakama ya mwanzo na ya wilaya kwa kumpatia mke wake robo ya mali kama mgao wake wakati
mwananmke huyohuyo ndiye aliyesababisha ndoa kuvunjika baada ya kuamua kuondoka
mwenyewe nyumbani kwasababu anazozijua yeye.
Kwahiyo ndugu Robert aliamini kuwa
mwanamke huyo hastahili mali aliyopewa kwakuwa yeye ndiye sababu ya kuvunjika
kwa ndoa.
Jaji Maina(kama alivyokuwa), alitoa uamuzi kuwa suala la nani
amesababisha ndoa kuvunjika halina uhusiano wowote na suala la nani anatakiwa
kupata nini. Alisema kuwa katika mambo yanayozingatiwa wakati wa kugawana mali pale
ndoa inapovunjika swali la nani amesababisha ndoa ivunjike halina nafasi.
Alisema kinachozingatiwa na kuangaliwa ni kile kilichoelezwa katika kifungu cha
114 cha Sheria ya ndoa ambacho ni pamoja na mchango wa mwanandoa katika
kupatikana kwa kila mali husika.
Kwahiyo kwa wale waliotaka kujua kuhusu hatima ya waanzilishi
wa chokochoko katika ndoa basi hili liko hivi. Suala la nani ameanzisha ugomvi
haliangaliwi wakati wa kugawana mali. Aidha, suala hili linaweza kuangaliwa
katika mazingira mengine kwa mfano zinapokuwa zinajadiliwa sababu zilizopelekea
ndoa kuvunjika, na katika masuala ya fidia kwa mwanandoa, lakini si katika
kugawana mali. Kwahiyo hivi ndivyo
ilivyo.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE. ”. 0784482959,
0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment