NA BASHIR YAKUB -
Hapo awali niliandika
namna sheria isivyowaruhusu viongozi
wa serikali za mitaa
(watendaji kata, wenyeviti wa mitaa,wajumbe, na ule uongozi wote wa huko
chini) kuandaa na kusimamia
mauzo na manunuzi ya nyumba au viwanja, kwa ujumla ardhi.
Nikasema kuwa kitu hicho hakiruhusiwi
katika sheria na wanaofanya
hivyo wako katika makosa
makubwa.
Nikasema zaidi kuwa, na asilimia kumi wanayowatoza ni makosa
na ndio maana hailipwi kwenye akaunti ya serikali bali mkononi au utapewa
risiti za kuchana kwenye daftari badala ya EFD, wizi mtupu.
Leo tena tutizame kama unaweza kuruhusiwa kubadili jina la
ardhi kutoka kwa aliyekuuzia kwenda kwenye jina lako mnunuzi ikiwa ulisimamiwa
na serikali za mitaa katika manunuzi hasa ardhi iliyopimwa.
Sheria Namba 4 ya 1999, Sheria ya Ardhi kifungu cha 62( 1)
kinasema kuwa kila nyaraka(document) yoyote ya ardhi iliyosajliwa ambayo
itatumika katika mauzo,rehani,zawadi,kurithi,
au pango ni lazima iwe katika mfumo wa fomu maalum.
Kifungu hiki kinaturejesha
katika kanuni za ardhi za mwaka 2001 ili kuziona fomu zinazohusika katika
manunuzi ya ardhi na mahitaji yake.
Fomu ya kwanza ni fomu namba 38 ambayo ni sawa na mkataba wa
mauzo(contract for disposition). Fomu hii inalazimisha kuwa ni lazima iwe imegongwa muhuri wa Wakili au kushudiwa na wakili.
Fomu ya pili ni namba 35 ambayo kisheria ni nyaraka ya
kuhamisha umiliki(transfer of right of occupancy).Fomu hii nayo inatoa ulazima
wa kuwa imeshuhudiwa na kugongwa muhuri wa Wakili pande mbili, yaani upande wa
mhamisha umiliki/muuzaji, na upande wa mpokea umiliki/mnunuzi.
Maana yake ukipeleka nyaraka(documents) za ununuzi wa ardhi
uliosimamiwa na kusainiwa na serikali za mitaa bila ushuhuda wa wakili kwa
lengo la kubadili jina hazitapokelewa. Iwe umezipeleka ardhi ya wilayani au
wizarani kote hazitapokelewa kwasababu zitakuwa hazijakidhi mahitaji ya
kisheria.
Aidha, kwenye sheria nilizotaja hapo juu hakuna popote alipotajwa
serikali za mitaa. Kwa waliowahi kuwatumia serikali za mitaa halafu wakaenda
kuhamisha umiliki (transfer) wanajua namna walivyorudishwa. Serikali za mitaa hawaruhusiwi
na nyaraka hizi za kisheria hazijaweka sehemu yao ya kusaini au kugonga mhuri. Wakili ni mtu pekee anayetajwa na sheria hizi.
Kazi kubwa ya serikali za mitaa katika ununuzi wa ardhi ni
kumtambulisha muuzaji ikiwa mnunuzi ataamua kwa hiari yake kuwatumia kutaka
kumjua muuzaji huyo. Au wakati mwingine mnunuzi atawahusisha ikiwa atahitaji kujua historia ya eneo husika.
Hata hivyo
hatua hizi zote za kuwahusisha ni hiari na sio takwa la kisheria. Mnunuzi au
muuzaji anaweza kuamua kuwahusisha au asiwahusishe.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment