NA BASHIR YAKUB.
Kusimamishwa na trafiki barabarani, na ukawa huna leseni
mfukoni kwa muda huo sio kosa. Mwambie huyo trafiki kuwa hilo sio kosa. Sheria
inatutaka kutembea na leseni
tunapoendesha vyombo vya moto, lakini pia haisemi kuwa utakapokuwa hauna
pale unapoombwa na trafiki basi ni kosa.
Tunaongelea Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168. Wapo watu
wameandikiwa faini kisa wameombwa leseni wakasema hawana, au wakasema wamezisahau majumbani. Hawa
waliotozwa faini katika mazingira kama haya wameonewa. Na wanastahili
kurudishiwa fedha walizotoa haraka.
Ni kweli kifungu cha 77 cha Sheria ya Usalama Barabarani kinamtaka
kila mwendesha chombo cha moto kutembea na leseni barabarani. Ni kweli askari anayo mamlaka kumsimamisha mwendesha
chombo cha moto. Na ni kweli pia kuwa askari anayo mamlaka ya kumtaka mwendesha
chombo cha moto aoneshe leseni yake.
Lakini sio kweli hata kidogo kuwa
mwendesha chombo cha moto asipoonesha leseni kwa wakati huo basi tayari
ametenda kosa. Sio kweli.
Kifungu cha 77(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani kinasema
kuwa mtu hatatiwa hatiani, kwa maana ya kulipa
faini au kuandikiwa kosa au kuadhibiwa na chombo chochote ikiwamo mahakama, kwasababu
tu hakubeba, au hakutoa/kuonesha leseni
pale alipotakiwa kufanya hivyo, isipokuwa ana siku tatu za kutoa au kuonesha
leseni hiyo tokea siku hiyo
aliposimamishwa.
Tafsiri iko wazi kuwa unaposimamishwa, ukaombwa kuonesha leseni,
ukawa huna kwa mda huo, unazo siku tatu mbele za kutakiwa kuleta na kuonesha.
Anachotakiwa kufanya askari sio kukuandikia kosa, laa hasha, bali ni kukutaka
umuoneshe leseni hiyo ndani ya siku tatu tokea siku hiyo. Ukishindwa kufanya
hivyo ndani ya siku hizo hapo ndipo linaweza kuwa kosa.
Watu wasionewe. Wapo askari wengine pia hawajui hizi sheria. Hawa
sisi madereva tuwaelimishe.Unaweza kudhani askari anakuonea kumbe naye hajui. Kwahiyo kazi unayo wewe kuhakikisha unamweleza
huyo askari kuhusu kifungu hiki na namna kinavyotaka. Wewe ndiye mtetezi wa kwanza
wa haki yako kabla ya kutetewa na mtu mwingine.
Na kama itatokea ukaandikiwa
adhabu kwa lazima kwa kitu kama hiki, basi unayo haki ya kukataa kulipa na
kuomba kufikishwa mahakamani ili sheria ikatafsiriwe.Mwambie “sitalipa nataka
sheria ikatafsiriwe mahakamani”. Kukataa
kulipa sio kosa au ukorofi na hivyo huna haja ya kukhofu.Kukataa kulipa ni haki
katika haki ulizonazo ukihisi umeonewa. Na kama umeshalipa au ulilipa huko nyuma katika mazingira ya
jambo kama hili na unao ushahidi basi unayo haki ya kudai hela uliyolipa.
Unaweza kuidai huko ulikotozwa au mahakamani.
Sheria imetoa ahueni hii ikizingatia mazingira ya ubinadamu. Huwezi
kila unapoamka asubuhi ukakumbuka leseni. Huwezi kila unapokuwa na safari
ukakumbuka leseni. Safari nyingine ni za ghafla na za kushtua, mfano kuitiwa msiba,ugonjwa,matatizo
kazini,bila kusahau msongo/stress za ada na kodi. Atapata wapi muda wa
kukumbuka leseni mtu huyu.
Mwingine amebadilisha nguo na hivyo leseni kubaki kwenye nguo
iliyovuliwa, mwingine amebadilisha gari na hivyo leseni kubaki kwenye gari
jingine. Na mazingira mengine kama hayo. Zote hizi ni dharula za kibinadamu
zilizowafanya watunga sheria kuweka muda wa siku tatu kwa ajili ya kutoa au kuonesha leseni.
Basi wote tubadilike, madereva na askari wasimamia usalama
barabarani.Dereva asiwe mkorofi, kadhalika askari asimwonee dereva.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment