NA BASHIR YAKUB -
Huna haja ya kuvutana na mtu kuhusu iwapo wewe ni baba wa
mtoto au hapana. Nimesema baba kwasababu wasiwasi wa aina hii mara zote upo kwa
wanaume. Kuwa fulani ni mama wa fulani karibia mara zote hapana utata.
Basi wapo wanaopenda au ambao wangependa kufanya vipimo vya
vinasaba(DNA) kuthibitisha kama ni wazazi kweli ama hapana. Nitaeleza utaratibu
mzima hapa kutokana na Sheria ya Usimamizi wa Vinasaba vya Binadamu ya 2009,Sura
ya 73.
1.NANI ANAWEZA KUPIMWA
DNA.
Yeyote ambaye anahitaji kujua kuhusu uhalali wa uzazi wake
anaweza kupima DNA. Upimaji huu hauna umri. Hata hivyo DNA si kwa jili ya
masuala ya kuthbitisha uzazi tu, bali
hutumika hata katika masuala ya ushahidi na upelelezi.
2. NANI ANA
MAMLAKA YA KUOMBA DNA KUPIMWA.
Si kila mtu anaweza
kuomba kupima DNA. Hata kama mwenye
uhitaji ni wewe lakini bado huna mamlaka
ya kuomba kupima DNA. Kifungu cha 25(2) cha Sheria niliyotaja hapo juu kinawataja
wafuatao kuwa na mamlaka ya kuomba DNA kupimwa. Kinamtaja hakimu ambapo kuna
kesi/shauri fulani linaendelea, Wakili, afisa ustawi wa jamii, afisa polisi
mwenye cheo zaidi ya inspector,daktari, na mkuu
wa wilaya.Hawa ndio wenye mamlaka(Requesting Authority).
Kwahiyo wewe ukiwa na shida ya DNA unaweza kumuona mmoja kati
ya hawa ili aandae maombi ya kupima DNA na kuyapeleka kunakostahili.
3. MAOMBI YA DNA YANAPELEKWA WAPI.
Kifungu cha 24 cha Sheria ya Usimamizi wa Vinasaba kinaitaja maabara ya Vinasaba vya
binadamu ya Mkemia Mkuu wa serikali kuwa
na Mamlaka ya kupima DNA. Pia kinazitaja na maabara nyingine ambazo zitakuwa na
leseni maalum ya kupima DNA kuwa na mamlaka hayo.
Kwahiyo maombi ya DNA yatapelekwa moja kati ya sehemu hizo
mbili.
4. NANI ANAPELEKA
MAOMBI NA KUFUATILIA MAJIBU.
Wahusika waliopimwa DNA(sample source) hawaruhusiwi kupeleka
wala kufuatilia majibu ya DNA. Maombi na Majibu ya DNA yatapelekwa na
kufuatiliwa na hao niliowajataja hapo juu katika 2 ambao ndio wenye mamlaka ya kuomba DNA
kupimwa.
Hawa ndio watapeleka maombi na ndio watachukua majibu na
kuwasomea wahusika.
5. MAOMBI YA KUPIMA DNA YANAKUWAJE ?.
Kifungu cha 26(1) cha Sheria hiyo kinasema maombi ya kuomba
DNA kupimwa yatakuwa katika mfumo maalum wa maandishi. Yataeleza muombaji na
cheo chake, yataeleza wanaotakiwa kupimwa DNA na sahihi zao,yataeleza DNA
ipimwe katika nini na nini, yataeleza sababu
za kupima DNA,yatakuwa na kiapo kuwa majibu hayatatumika kwa shughuli
nyingine tofauti na iliyoombwa, na yatasainiwa na muombaji ambaye ni wale niliowataja
katika 2 juu.
6. ADA YA KUPIMA DNA NI KIASI
GANI.
Malipo yapo. Na mpaka disemba 2018 makala haya yalipoandikwa
ada ni Tshs 100,000/=( laki moja tu) kwa kila mtu. Kawaida DNA ya kutambua
uzazi(parentage) hupimwa watu watatu. Mama, baba na mtoto. Kwahiyo kila mmoja
ni laki moja na hivyo watatu ni laki tatu.
Nani anatoa hiyo hela, anaweza kuwa yule anayehitaji kuthibitisha kwamba yeye ni mzazi halali, au yakawa ni maelewano ya wahusika, au
kutokana na maelekezo ya mahakama.
7. DNA INAPIMWA KATIKA NINI NA NINI.
Kifungu cha 29(1) cha sheria hiyo kinaeleza maeneo ambayo DNA
inaweza kupimwa kuwa ni kwenye mate, damu, mkojo, ute ute wa sehemu za siri,
nywele,haja kubwa,ngozi,mifupa,meno,mbegu za kiume,unyayo na sehemu nyingine
ambayo mhusika atakuwa amegusa,kukanyaga au kuwepo au alama yoyote ya uwepo
wake.
Basi yatutoshe haya kwa leo kuhusu DNA ya kutambua iwapo
umzazi wa fulani ama hapana.
0 comments:
Post a Comment