Wednesday 23 January 2019

KUENDESHA GARI SPIDI NDOGO BILA SABABU ZA MSINGI NI KOSA KISHERIA.

Image result for KUENDESHA SPIDI

NA BASHIR  YAKUB -

Wapo watu wanaojua kuwa kuendesha gari kwa mwendo mdogo ndio ustaarabu na ndio jambo zuri linalopendwa sana na sheria.  Yeyote mwenye mawazo  ya aina hii amekosea sana. Kifungu cha 56 cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya  `168 kinakataa dhana hii. Kifungu hicho kinasema kuwa  “dereva wa gari au teela  ambaye bila sababu za msingi ataendesha kwa mwendo mdogo(low speed)  ambao utaelekea kuwasababishia watumiaji wengine wa barabara usumbufu au utawasababishia usumbufu, atakuwa ametenda kosa na panapo hatia yake atatakiwa kuadhibiwa kwa kulipa faini”.                             

Maneno bila sababu za msingi hapo juu humaanisha kuwa  kama itatokea mtu anaendesha kwa mwendo mdogo  basi kuwepo na sababu za  msingi za kufanya hivyo na hapo ndipo anaweza kukwepa kuingia katika kosa hili. Sababu za msingi zaweza kuwa foleni kubwa na hivyo huwezi kuongeza mwendo, unaendesha ndani ya msafara rasmi unaotambulika kisheria, maelekezo ya vibao  na alama za usalama za eneo hilo yanakuelekeza kuendesha kwa mwendo huo, ubovu wa barabara ambao haukuruhusu kwenda mwendo mkubwa, barabara imezuiwa na waandamanaji au halaiki(population)  nyingine ambayo haikuruhusu kwenda haraka.  

Ubovu wa gari unaweza kuwa sababu ya kutembea taratibu  lakini sio sababu ya msingi. Sheria hii inaelekeza gari likiwa bovu kutokuendeshwa barabarani kwa maana ya kuwekwa pembeni ili kulirekebisha au kutafuta namna nyingine.
Kwahiyo usiwasababishie watu usumbufu barabarani kwa kudhani kuendesha mwendo mdogo ndio uendeshaji mzuri na bora. Askari wa usalama barabarani anayo mamlaka ya kukusimamisha na kukutoza faini kwa kuendesha mwendo mdogo bila sababu za msingi. 

Unakuta msururu wa magari yanayotembea taratibu, unadhani mbele kuna tatizo kumbe kuna mtu anatembea mwendo wa kinyonga.  Akisumbuliwa kwa honi anadhani wanamwonea yeye ndiye yuko sahihi zaidi kwakuwa anaendesha mwendo mdogo.  Hili ni kosa unaweza kupiga hata simu polisi ukaomba msaada wa kukamatwa na kuadhibiwa kwa mtu wa aina hii.

Aidha, ifahamike kuwa vibao/alama za barabarani ndizo mwongozo mkuu wa kiasi cha mwendo wa kuendesha. Kwahiyo hatua ya kwanza ni kuhakikisha unafuata alama hizi za mwendo zilizoko barabarani. Pale ambapo hazipo basi haifai kuendesha mwendo mkubwa sana wala mwendo mdogo sana. Ni kutumia mwendo wa kati kwa kati.
Mwendo kasi pekee ndio umekuwa ukipigiwa sana chapuo kama kosa, lakini kumbe hata mwendo wa polepole nao unaweza  kuwa kosa.

Ni ukweli usio na ubishi kuwa mwendo mdogo pasipostahili unaweza kukusababishia wewe mwenyewe ajali au ukawasababishia watumiaji wengine ajali.
Basi, ilikuwa ni muhimu hili nalo kujulikana ili wale wenye imani zao kuwa kwenda polepole ndio utiifu wajue kuwa sio kweli. Na pengine siku nyingine wakiadhibiwa wasione wameonewa.
Yatutoshe hayo, fuata sheria acha kuwasababishia watu usumbufu.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA  JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com









1 comments:

Post a Comment