NA BASHIR YAKUB -
Nimeona mara nyingi ambapo marehemu alikuwa mkristo halafu
warithi wake, au ndugu, jamaa wanaamua kufungua mirathi katika mahakama za
mwanzo. Yatupasa kujua kuwa, pale ambapo marehemu alikuwa mkristo hairuhusiwi
kisheria kufungua mirathi yake katika mahakama yoyote ya mwanzo. Iwe ya mjini
au kijijini, madhali ni mahakama ya mwanzo basi inakosa mamlaka ya kimirathi
kwa marehemu mkristo.
Na hili ni katika namna zote, yaani pale marehemu anapokuwa
ameacha wosia au hajaacha. Madhali tu alikuwa ni mkristo basi usifungue
mahakama ya mwanzo.
Mahakama za mwanzo ni zile ambazo zipo kila kata vijijini
au mijini, na ni rahisi tu kuzijua kwani hata ukiuliza utaambiwa, na nyingine
zina mabango kabisa “MAHAKAMA YA MWANZO YA..........”
Kwenye masuala ya mirathi tunazo sheria za aina mbili, zile
za kiutaratibu (procedures), na zile zinazoelekeza mgawanyo wa mali yaani nani
apate nini(substantive laws). Hizi zinazoelekeza nani apate nini nazo ziko aina
kuu tatu. Na kila sheria katika hizi tatu inasimamia kundi lake. Kundi
linalosimamiwa na sheria moja haliwezi kutumia sheria ya kundi jingine. Na kila
sheria ni tofauti na nyingine katika namna ya kugawa mali.
Ya kwanza katika
hizi tatu ni sheria iitwayo Sheria ya Urithi ya India ya Mwaka 1865(The Indian
Succession Act), ya pili ni sheria iitwayo Sheria ya Amri za Mila ya Mwaka
1963(The Customary Law(Declaration)Order, na ya tatu ni Sheria ya Kiislam
ambayo ni Qur-an na Hadith/Sunnah.
Sheria ya Urithi ya
India ni maalum kwa ajili ya Wakristo,wakati
Sheria ya Amri za Kimila ni maalum kwa watu wa mila ambao sio waislam wala
wakristo, na Sheria ya Kiislam ni maalum kwa ajli ya Waislam. Kwahiyo kisheria
unatakiwa kuandaa mirathi yako kutokana na sheria yako. Na mirathi inaanza
tangu unapoandaa wosia na kuishia pale usimamizi au mali za marehemu
zinapogawanywa.
Hivyo kama ni wosia uwe na
sifa zinazokubalika katika sheria ya kundi lako, na usijiandikie tu kwani itakuwa
kinyume na sheria na itabatilishwa. Kadhalika kwa wale wanaofungua mirathi
wafungue mahakama ambayo imekubaliwa katika sheria ya kundi lao, na usifungue tu
unavyojisikia.
Pia nilitaja Sheria za
kiutaratibu(procedures) ambazo
baadhi ni Sheria ya Mahakama za
Mahakimu(The Magistrate Court Act), na Sheria
ya Mirathi sura ya 352,(PAEA).
Kuhusu wakristo kutofungua mirathi yao mahakama za mwanzo ni
kuwa, Jedwali la 15 kipengele cha 1(i) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu
kinasema kuwa mahakama ya mwanzo itakuwa na mamlaka katika masuala ya mirathi
iwapo sheria inayotumika katika mirathi hiyo ni sheria ya kiislamu au Sheria ya
Mila. Kwa maana ya kifungu hiki ni kuwa mahakama ya mwanzo inatumika katika mirathi
ambayo marehemu alikuwa muislam ama marehemu alikuwa mtu aliyeishi kimila. Marehemu
aliyekuwa mkristo mahakama hii haiwezi kutumika.
Aidha, mahakama inayotumika kwa marehemu mkristo ni Mahakama Kasimu ya Wilaya(district delegate) kwa
mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria ya
Mirathi sura ya 352. Mahakama Kasimu ya
Wilaya utaipata popote ilipo mahakama ya wilaya ya kawaida. Ni vyema ukafika
hapo ukasema nataka kufungua mirathi utaelekezwa utaratibu au uwasiliane na
mawakili.
Kadhalika makundi yote ya waislamu,wakristo na watu wa mila wanaruhusiwa
kuitumia mahakama kuu kwa shughuli za mirathi kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha
Sheria ya Mirathi Sura ya 352 kwakuwa ina mamlaka ya jumla.
Basi ni muhimu kwetu kuyazingatia haya ili kuweza kusimamia mirathi kwa uhalali. Msimamizi wa
mirathi anakosa uhalali na anahesabika si msimamizi wa mirathi, na kama amegawa
mali ugawaji unakuwa haramu iwapo hakufuata utaratibu wa sheria.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment