NA BASHIR YAKUB -
Ni muhimu kutahadharishana kuhusu jambo hili. Kitaalam jambo
hili huitwa “adverse possession”. Ni kanuni ya kisheria. Ni wakati ambapo mtu
au watu wanavamia ardhi yako, lakini baada ya muda wahesabika kuwa ni wamiliki
halali. Na wanatambuliwa hivyo na sheria na wewe mmiliki halisi unageuka na kuwa
mvamizi.
Lakini hoja kubwa hapa si lazima mtu awe mvamizi. Anaweza kuwa
mpangaji, au mtu anayekulindia eneo.
Lengo la hoja ni kutaka kuwatahadharisha
wamiliki ardhi hasa wale wanaowaacha
watu wawalindie maeneo au wanaowapa watu kukaa bure bila utaratibu maalum. Ifahamike kuwa si kosa
mtu kukulindia eneo na wala si kosa mtu kukaa bure kwenye eneo lako, ila ni
kosa tena kubwa kufanya hivyo bila utaratibu maalum wa kisheria.Na hapa ndipo
kugeukana kunapokuja.
Ni rahisi huyo mtu kukugeuka na wapo watu wamegeukwa, na kwa
kutumia kanuni hii na wameruhusiwa na mahakama kuwa wamiliki halali.
Kawaida sheria zetu za ardhi Tanzania zinatambua aina au
namna mbalimbali ambazo mtu anaweza
kupitia katika kupata ardhi kihalali. Moja ni kununua, pili kupewa zawadi, tatu
kurithi, nne kutwaa eneo lisilo na mwenyewe, tano ni hii ya kuingia katika eneo kama mvamizi ama
vinginevyo na baadae ukabadilika na kuwa mmiliki.
Namna zote hizi ni za kisheria na zinakubalika kama njia
halali za kupata na kumiliki ardhi.
1.WAKATI AMBAO MVAMIZI
ATATAMBULIKA KAMA MMILIKI.
Wote tunajua kuwa mvamizi ni yule mtu ambaye ameingia
kiharamu katika ardhi ya mtu mwingine. Ardhi inaweza kuwa nyumba, kiwanja au
shamba na vile vilivyomo. Kuingia kiharamu ni kuingia bila ridhaa ya mmiliki na
bila ya sababu za kisheria.
Lakini hata mpangaji au mtu uliyemuacha akulindie eneo anaweza
kuhesabika kama mvamizi katika kanuni hii iwapo wewe mmiliki utakosa ushahidi
wa maandishi au vinginevyo kuthibitisha kuwa ni mpangaji au ni mtu uliyemuacha
akulindie eneo.
Kesi ya Buckinghamshire cc v Moran [1990]
Ch 623(CA) imeeleza misingi ya kanuni hii ya mvamizi kugeuka
kuwa mmiliki. Kadhalika mahakama ya
rufaa katika rufaa namba 193/2016 kati ya The registered trustee of the holly spirit
sisters Tanzania VS January Kamili Shayo na wengine 136 nayo imeeleza
jambo na kuweka misingi yake.
Kesi hizi mbili zinaeleza kuwa
ikiwa mtu ataingia na kukaa kwenye ardhi
yako, iwe nyumba, kiwanja,shamba au vinginevyo kwa kipindi ambacho kinazidi
miaka 12 basi mtu huyo mvamizi atageuka kutoka hadhi yake ya uvamizi na kuwa
mmiliki halali.
Kwa msingi huu kumbe si salama
mtu au watu kuendelea kukaa katika eneo lake bila taratibu maalum
zinazotmbuliwa na sheria.
Hata hivyo hoja ya kukaa zaidi ya miaka 12
pekee haitoshi kuthibitisha umiliki bali pia mvamizi athibitishe pia kuwa wakati
anaingia hakuwa na ridhaa yoyote kutoka kwa mmiliki, mfano, hakuomba kukaa au
kutumia hiyo ardhi, au hakuwa mpangaji, pia athibitishe kuwa hakuwa na haki yoyote
kukaa humu mfano sio mtoto au mke wa mmiliki au hakuwa na haki nyingine, nk.
Tunachotaka kusisitiza ni kuwa tuwe makini na watu ambao wanakaa
kwenye maeneo yetu kwa mda mrefu na hata wapangaji wa aina hiyo pia.
2. NAMNA YA KUWEKA ARDHI YAKO SALAMA KUEPUKA KANUNI HII.
Kwanza, yeyote utakayempa
ardhi yako kwa ajili ya kulima, kufuga, kuishi ,kupanga au shughuli nyingine
yoyote, basi hakikisha mnaandika na kusaini na kuweka picha ikiwezekana na
mashahidi. Mara nyingi walinzi wa maeneo
hasa mashamba makubwa na viwanja wamekuwa wakigeuka.Unaweza kudhani sio rahisi
kufanyiwa hivyo na ni masikhara, lakini waliokutwa na haya wanajua nazungumzia
nini. Wapo wengi wametumia kanuni hii kuchukua maeneo ya watu. Na muda huo kama
hakuna maandishi mtu anakukataa kuwa hukumruhusu aingie bali aliingia
mwenyewe baada ya kukuta hamna mtu.
Pili, ni muhimu kuyawekea uzio
maeneo yetu kuepuka wavamizi. Kadhalika kuweka vibao hasa kwenye mashamba
vinavyokataza uvamizi kwa mfano kibao kinaweza kuandikwa “HAIRUHUSIWI KUINGIA
ENEO HILI BILA KIBALI MAALUM” nk.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment