NA BASHIR YAKUB -
1.UKAZAJI WA HUKUMU NI
NINI.
Ukazaji wa hukumu ni hatua inayochukuliwa na mtu aliyeshinda
kesi/shauri kwa kuiomba mahakama kumlazimisha mtu aliyeshindwa katika
kesi/shauri kufanya au kutekeleza kile ilichoamua dhidi yake/mshindwa. Kawaida
mtu akishindwa kesi/shauri mahakama huwa inatoa maagizo mbalimbali. Mathalan,
agizo la kulipa hela, agizo la kurudisha nyumba au mali fulani, agizo la
kubomoa, agizo la kuondoka katika pango au katika nyumba,kiwanja fulani, agizo la
kujenga, agizo la kulipa fidia, faini, gharama n.k. Maagizo yako ya aina nyingi inategemea na shauri na
shauri.
Hivyo basi, ukazaji hukumu/utekelezaji huwa ni kulazimisha agizo
aumaagizo ya aina tuliyoona hapo juu
yaweze kutekelezwa kama ilivyoamriwa.
2. NI WAKATI GANI HUKUMU HUTAKIWA KUKAZWA.
Kwa ujumla mahakama inapotoa hukumu basi yule aliyeshindwa mara
moja au ndani ya muda aliopewa kama amepewa,hutakiwa kutekeleza kile
kilichoamuliwa kwa hiari yake. Aliyeshindwa akikataa kutekeleza kile
kilichoamuliwa kwa hiari yake basi ni wakati huu ambapo suala la kukaza/kutekeleza hukumu kwa njia
mahakama huja.
Kwa maana nyingine mtu
aliyeshndwa akiamua kwa hiari yake kufanya yale aliyoagizwa na mahakama basi
suala ukazaji wa hukumu haliwezi kuwepo.
3. UMUHIMU WA KUZUIA HUKUMU KUKAZWA.
Sababu za msingi zinazoweza kupelekea kuzuia hukumu kukazwa ni
pamoja na sababu kuwa umekata rufaa na hivyo ukazaji wa hukumu usimame ili rufaa
yako isikilizwe kwanza, sababu nyingine ni iwapo kesi imeendeshwa bila wewe
kujua au kuwepo isipokuwa umeshtukia tu watu wanakuja kukaza hukumu, sababu
nyingine ni iwapo una maslahi katika
mali inayokaziwa hukumu kwa mfano ni mali ya ndoa na hukuwa na taarifa na
kilichoendelea, ni mali yako lakini
inataka kuuzwa au kutumika kutekeleza hukumu kwa kesi ambayo sio yako na
pengine hukuwahi kujua uwepo wake, nk.
4. KUZUIA UKAZAJI WA HUKUMU.
Ukazaji wa hukumu unazuiwa kwa njia ya mhusika kupeleka
maombi ya faragha(chamber application) mahakamani. Mleta maombi/mlalamikaji atakuwa yule anayezuia ukazaji wa hukumu na
mjibu maombi/mlalamikiwa atakuwa yule
anayekaza hukumu. Kadhalika ataunganishwa dalali wa mahakama(court brocker)
aliyeteuliwa kukaza hukumu kama yupo, na wengine ambao watakuwa ni muhimu
kuunganishwa ili kutekeleza azma.
Maombi ya kuzuia ukazaji wa hukumu yatafunguliwa katika
mahakama ambayo imetoa hukumu husika. Pia maombi haya yanaweza kupelekwa chini
ya hati ya dharula ikiwa utekelezaji wa hukumu umeshaanza au ikiwa unaona kuwa
uchelewaji wowote unaweza kupelekea utekelezaji kufanyika kabla hata maombi
yako ya kuzuia hayajasikilizwa na hivyo kukusababishia hasara na usumbufu. Hati
ya dharula husaidia maombi kusikilizwa haraka kuliko ilivyo kawaida.
Maombi ya kuzuia ukazaji au utekelezaji wa hukumu yataambatana
na kiapo cha muombaji yakieleza sababu za msingi na za kisheria za kwanini
hukumu isitekelezwe. Na watu wa aina mbili wanaweza kufungua maombi haya.
Kwanza mhusika kwenye hukumu hasa yule aliyeshindwa, na pili mtu yeyote mwenye
maslahi katika mali inayotaka kutumika
kutekeleza hukumu ambaye alikuwa mhusika
katika shauri lililoisha au hakuwa mhusika, na pia kuwepo sababu za msingi kuwa
si halali mali hiyo kutumika kutekeleza hukumu.
Maombi haya yakishapokelewa mahakamani yatapangiwa hakimu au
jaji wa kuyasikiliza. Na baada ya kusikilizwa inaweza kuamuliwa kuwa
utekelezaji/ukazaji wa hukumu usitishwe kwa muda kupisha rufaa au vinginevyo,
au kuwa sio halali kutumia mali hii kukazia hukumu na hivyo kuiondoa mali iliyokuwa
inatakiwa kutumika kukaza hukumu katika mchakato huo.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment