NA BASHIR YAKUB -
Ardhi iwe kiwanja au nyumba thamani yake hupanda pale
inapokuwa imepimwa. Kupima ardhi ni kurasimisha ardhi. Faida nyingi hupatikana
baada ya ardhi kuwa imerasimishwa. Baadhi ya faida ni kuwa ardhi hupanda
thamani yake, kuweza kupata mkopo kwa urahisi, ardhi kutumika kama dhamana
mahakamani, lakini kubwa ni kuwa na amani na uhakika wa ardhi yako kuwa eneo
ulilopo linaruhusiwa kisheria, sio eneo
hatarishi, sio eneo la miradi ya serikali, sio hifadhi ya barabara au barabara
nk.
Unakuwa na amani kuwa uko sehemu
sahihi na salama.
Kupima ardhi ni hatua inayopitiwa pale unapoelekea kupata
hati. Kila ardhi yenye hati imepimwa lakini si kila ardhi iliyopimwa ina hati.
UTRATIBU WA KUPIMIWA
ARDHI.
1.Kuandika barua ya maombi ni hatua ya
kwanza ambapo utatakiwa kumwandikia mkurugenzi wa halmashauri ukiomba kupimiwa
eneo lako. Hii ni barua ya kawaida ya kiofisi isipokuwa ieleze majina yako kwa
ukamilifu na ichambue anuani ya eneo ambalo linalotakiwa kupimwa kwa ukamilifu.Mkurugenzi
unayetakiwa kumwandikia ni yule wa halmashauri ambamo ardhi inayotakiwa kupimwa
imo. Kwa mfano kama ardhi iko wilaya ya kinondoni
basi mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya atakayeandikiwa barua.
Barua hiyo itaambatanishwa na nyaraka za umiliki wa eneo husika. Mara nyingi nyaraka hapa huwa ni
ile mikataba ya mauziano. Kadhalika,
barua yako inatakiwa kupitishwa serikali
za mitaa na kwa mtendaji kata.
2. Barua itakapokuwa imekidhi vigeo
basi itapokelewa kwa mkurugenzi na hapo mkurugenzi ataiwasilisha idara ya ardhi. Baruayako ya
maombi itakabidhiwa kwa afisa ardhi ambaye kazi yake kubwa itakuwa ni
kuthibitisha na kujiridhisha na umiliki wa ardhi ya mwombaji.
3. Baada ya kujiridhisha, afisa ardhi ataandaa na kujaza fomu namba SF 47 na kuiwasilisha
kwa afisa mipango miji.
4. Fomu na nyaraka vikishafika kwa
afisa mipango miji kazi yake kubwa ni kutizama iwapo eneo linaloombwa kupimwa
lina mchoro wa mipangomiji. Kama mchoro upo basi kazi nyingine ya afisa mipango
miji ni kusoma mchoro ule kuangalia kama eneo limepangiwa sawa na kile unachoomba.
Unaweza kuwa unaomba kwa ajili ya makazi kumbe eneo lilishapangiwa viwanda
tangu miaka ya huko nyuma pengine hata kabla hujazaliwa.
Maeneo yote yenye michoro huwa yamepangwa kwa ajili ya shughuli fulani mf, maeneo ya
makaburi, makazi, viwanda, maeneo hatarishi, dampo, miradi mbalimbali ya serikali,
viwanja vya wazi au vya michezo nk.
5. Afisa mipango miji akithibitisha
kuwa maombi yako yanaendana na mchoro husika
basi atairudisha ile fomu na SF 47 kwa afisa ardhi ikiwa na mapendekezo
ya maombi yako. Hapo afisa ardhi atajaza fomu SF 37 ambayo ndiyo maombi rasmi ya kuomba kupimiwa akiambatanisha na ushahidi wa mchoro wa mipango
miji unaoonesha eneo husika na vitawasilshwa
kitengo cha upimaji.
6. Hapo upimaji atateuliwa afisa
upimaji ambaye utaambatana naye mpaka eneo husika kwa ajili ya upimaji . Baada
ya hayo, ardhi yako itapimwa na hapo utaratibu wa kupimiwa utakuwa umekamilika
na hivyo kufungua mlango kwa hatua nyingine kufuata.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment