NA BASHIR YAKUB -
( A ).NAMBA YA KESI.
Kesi ya Jinai Na. 22/1998, Mahakama kuu Mwanza , Mbele ya
Jaji Mlay.
( B ) WASHITAKIWA.
1. Kapteni Jumanne Rume Mweiru. Huyu
ndiye alikuwa Kapteni siku ya tukio, akiendesha toka Bukoba VIA kemondo Bay hadi
Mwanza.
2. Gilbert Mokiwa. Huyu alikuwa mkaguzi
wa meli, na ndiye alikuwa na wajibu wa kuikagua MV Bukoba.
3. Alphonce Sambo. Huyu alikuwa afisa
bandari Bukoba, na wakati meli inaanza safari yeye na wenzake waliratibu
safari.
4. Prosper Rugumila.Huyu alikuwa afisa
bandari kemondo ambapo MV Bukoba ilipitia ikitokea bandari ya Bukoba na kuongeza
abiria na mizigo.
( C ) KOSA
WALILOSHITAKIWA NALO.
Kuua bila kukusudia
kinyume na kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za
Tanzania.
( D ) MAELEZO YA KOSA.
Kuwa, tarehe 21 / 5 / 1996 majira ya saa 7 :30 asubuhi, eneo
la ziwa Victoria Mwanza washitakiwa kwa uzembe walisababisha meli ya MV
BUKOBA iliyokuwa ikitokea Bukoba
kuelekea Mwanza kupinduka na kuzama ,na hivyo kusababisha vifo vya watu 159.
( E ) MASHAHIDI UPANDE WA MASHTAKA.
Upande wa mashitaka ulileta mashahidi 32 wakiwemo ;
1. Kapteni Cleophas Magoge . Huyu saa 8
: 15 asubuhi,aliitoa MV VICTORIA bandarini Mwanza ilipokuwa inaendelea na
matengenezo na kulazimika kuiendesha
kuelekea kwenye eneo la ajali baada ya kuambiwa kuwa MV BUKOBA imezama.
Anasema alipofika eneo la tukio
aliiona MV Bukoba ikiwa kichwa chini miguu juu, huku mizigo hasa ndizi,watu, na
miili mingi ikielea majini. Na aliposogea karibu alimuona Kapteni wa MV
Bukoba mshitakiwa wa kwanza akiwa
ananing’inia juu ya meli iliyozama.
2. Shahidi mwingine ni Kapteni Mannase
Ephraim Kombo. Huyu anasema siku ya tukio alikuwa akiendesha MV BUTIAMA kutoka
Port Bell Uganda kuelekea Mwanza. Anasema saa 6 :00 za asubuhi aliingia kwenye
radio na kuwasiliana na bandari ya Mwanza kuwa atafika saa 9 : 00 asubuhi.
Anasema wakati akiwasiliana alisikia
Kapteni wa MV Bukoba naye akiwasiliana kuwa atafika mwanza saa 8 :00 asubuhi.
Anasema alifika bandari ya Mwanza saa 9:00am akashusha mizigo lakini MV Bukoba
iliyosema kufika saa 8:00am haikuwa imefika.
Anasema, baadae alimsikia MPANGALA
aliyekuwa muongoza meli siku hiyo akiiita MV Bukoba kwenye radio bila majibu. Anasema MPANGALA aliita
sana mpaka akaamua kutoka nje kutizama, na kwa mbali saana aliona kitu ambacho
hakukielewa. Alirudi ndani na kuchukua hadubini(binocular) kutizama tena, na
hapohapo alimsikia akiongea kwa mshtuko kuwa MV Bukoba inazama.
Anasema maramoja aliamua kuiendesha
MV BUTIAMA kuelekea eneo la tukio ambapo alikuta mitumbwi kadhaa ya wavuvi
ikiokoa watu, na aliona maiti nyingi, watu hai, na mizigo vikielea.
3. Shahidi mwingine ni meneja wa yard ya
meli Mwanza. Anasema siku 29 kabla ya kuzama yaani april MV Bukoba ilikuwa na matatizo ya kuyumba ambayo pia
yalithibitishwa na mashahidi wengine. Anasema, mtaalam kutoka Ubelgiji ambao
ndio waliotengeneza meli hiyo aliletwa kuchunguza tatizo hilo na aliifanyia majaribio
katika eneo liitwalo Karumo.
Mtaalam aligundua matatizo ya kuyumba
na akasema watatoa ripoti mwezi wa 7 /1996, lakini meli ikazama mwezi 5/ 1996
miezi miwili kabla ripoti kutolewa.Anasema lakini baada ya majaribio hayo kuanzia
tarehe 12 / 5 / 1996 meli ilifanya safari tatu, mbili Mwanza – Port bell Uganda
, na moja Mwanza – Kisumu Kenya, na ya nne ndio ilikuwa ya mwisho ya Mwanza-
Bukoba.
Anasema siku hiyo MV BUKOBA ilienda
Bukoba lakini haikuwa imepangiwa kwenda huko, na badala yake MV VICTORIA ndiyo
iliyokuwa imepangiwa kwenda Bukoba. Anasema MV Victoria ina uwezo wa kubeba abiria
1200, na tani za mizigo 250 wakati MV BUKOBA
ina uwezo wa kubeba abiria 400, tani za mizigo 85.
Anasema kwahiyo tiketi za abiria na
mizigo zilizoandaliwa huko Bukoba zilikuwa ni za MV Victoria kwasababu ndiyo ilitakiwa kwenda. Kutokana na
hitilafu za injini ikashindwa kwenda na ikabidi ibadilishwe na MV BUKOBA na
hivyo MV Bukoba ikafanya kazi ya MV Victoria.
4. Munaf Hussein Ibrahim Punja ni abiria
aliyenusurika katika hiyo ajali. Anatoa ushahidi kuwa alipanda meli saa 9:00 pm
bandari ya Bukoba na watu walikuwa wengi pamoja na mizigo. Anasema meli ilikuwa
inakwenda upande. Anasema walipofika Kemondo saa 10 ;00 usiku alishangaa
kuwaona David pamoja na Mutayoba ambao aliwaacha bandari ya Bukoba na hawakuwa
wamepanda meli.
Anasema aliwauliza kulikoni, wakamwambia
kuwa kule Bukoba bandarini walizuiwa kuingia kwenye meli kwasababu ilijaa
kwahiyo wakaamua kuchukua Taxi kuja kuisubiria Kemondo Bay. Anasema hapo
Kemondo walipanda na wakasafiri wote.
5. Zabron Kasindirano naye ni abiria
aliyenuurika. Anasema meli ilipofika Kemondo Bay alimuona shemeji yake Francis Justusi Kaganji na kushangaa
kwasababu walimuacha Bukoba. Anasema
alimuuliza amefikaje Kemondo akamwambiwa alipanda taxi baada ya kuzuiwa kupanda
bandari ya Bukoba.
Anasema saa 7 :00 asubuhi wakati wamekaribia kufika meli
ilianza kuyumba sana. Anasema alikuwa
amekaa na wanawake akawaambia wapande juu kuchukua “life Jacket” lakini
wakamcheka kuwa ni mwanaume muoga na
hivyo kwa hofu ya kutoonekana muoga naye hakuchukua tena Jacket.
Anasema haikupita
dakika 10 tokea aambiwe muoga meli ikapinduka, akatupwa kwenye maji karibia na
mkungu wa ndizi ambao aliushikilia mpaka akaokolewa, na kuwa wale wanawake
hakuwaona tena.
Mashahidi walikuwa wengi ila kwa kutaja ni wachache.
( F ) ILI WATUHUMIWA WAPATIKANE NA HATIA YALITAKIWA
KUTHIBITISHWA MAMBO YAFUATAYO.
1. Kwamba meli ilikuwa na matatizo ya
kiufundi(ya kuyumba) na wao hawakuyashughulikia/kuyajali au kuzingatia matatizo hayo.
2. Pili, waliijaza meli watu kuzidi uwezo wake.
3. Tatu, waliijaza meli mizigo kuzidi
uwezo wake.
MATATIZO YA KIUFUNDI.
-
Hii
ilishindwa kuthibitika kwasababu kwanza
hakukuwa na rekodi yoyote ya mafundi na wataalum akiwemo yule Mbelgiji, iliyozuia meli kuendelea kufanya kazi.
Hakukuwa na shaka kuwa meli ilikuwa na matatizo ya kuyumba ila haikuzuiwa
kufanya kazi.
-
Pili, hakukuwa na ushahidi wa kisayansi
ulioonesha kuwa matatizo ya kuyumba
ndiyo yaliyopelekea meli kuzama.
KUJAZA WATU KULIKO UWEZO.
-
Hii
nayo ilishindwa kuthibitika kwasababu hakukuwa na rekodi sahihi ya watu
waliongia kwenye meli. Baadhi ya vitabu vinaonesha 400, vingine 700, vingine
759 nk.
-
Pia idadi ya watu ilioneshwa kwa kuangalia tiketi
zilizouzwa. Hakukuwa na ushahidi wa kuonesha waliongia ndani ya meli yaani
waliosafiri walikuwa wangapi. Mashahidi nao wanathibitisha kuwa kununua tiketi
sio kusafiri, unaweza kununua tiketi halafu usisafiri. Kwahiyo ni vigumu kupata
idadi ya waliosafiri kwa kuhesabu tiketi zilizouzwa.
-
Kitabu
cha uhakiki wa wasafiri ambacho hutumiwa na wakaguzi ndani meli inapokuwa
safarini ndicho kinaweza kuthibitisha waliosafiri
yaani waliokuwa ndani ya meli, na hivyo kujua kama ilizidisha au hapana. Hata
hivyo kitabu hicho nacho kilizama, na hivyo kukosa ushahidi wa kujua mpaka meli
inazama ilibeba abiria wangapi, na hivyo
kuweza kutambua kama walikuwa wamezidi ama hapana.Hii nayo ikafia hapo.
KUJAZA MIZIGO KUPITA
UWEZO.
-
Hii
nayo haikuweza kuthibitishwa. Hakuna rekodi Bukoba bandari kuwa zilipakiwa tani
ngapi ,na hakuna rekodi Kemondo Bay ziliongezwa tani ngapi. Unawezaje kusema
ilizidisha mizigo kwa ushahidi wa macho tu bila rekodi sahihi ya mizigo.Hii
nayo ikafa.
( G ) HUKUMU.
-
Kama
hakuna ushahidi kuwa ubovu wa meli ndio uliosababisha izame, kama hakuna
ushahidi kuwa meli ilipakia abiria wengi kuliko uwezo wake, kama hakuna
ushahidi kuwa meli ilipakia mizigo kuliko uwezo wake, nini kilichobakia zaidi
ya kuwaachilia huru washitakiwa wote wanne.
-
Mahakama
ikaona washitakiwa wote wanne hawana hatia , ikaamuru waachiliwe huru mara moja.
( H ) TUNAJIFUNZA NINI.
Ajali zote za majini, kuanzia hii ya
MV Bukoba, Spice Islanders Zanzibar, mpaka sasa Mv nyerere, nk, hadithi ni moja
tu, kuzidisha abiria na mizigo. Pamoja na hayo katika ajali zote hizi, hakuna
mtu unayeweza kumsimamisha akwambie idadi halisi kabisa,ile yenyewe ya watu
waliokuwemo na akakwambia. Huu ni ukweli. Hayupo, na narudia hayupo. Si mkata
tiketi, si mkaguzi anayesafiri na meli, si kapteni, si ofisa wa bandari, hakuna. Ndio maana utaona
inatajwa idadi ya waliokufa leo, kesho wanasema mwili mwingine umegunduliwa na
hivyo waliokufa idadi imeongezeka na kufikia kadhaa.
Hakuna mtu wa kukwambia waliosafiri
ni 100, walionusurika ni 50, tuna maiti 30, na hivyo sasa hivi tunafuta maiti
20 TU tufunge zoezi. Hakuna wa kutoa
takwimu kama hii. Ajali zikitokea tunakaa mwaroni tunasuburi chochote ambacho kitatemwa na ziwa ndicho tunachobeba
na kuongeza kwenye idadi. Ziwa lisipotema tunasema basi wameisha. Hatuwezi
kusema kwenye idadi yetu anakosa maiti mmoja na ndiye tunamtafuta kwasasa, katu
hatuwezi. Kweli dunia hii ya karne ya 21 hatuwezi hata kujihesabu hata kwa
kutumia vidole na vijiti ?, Kweli. ?.
Mbona huku kwenye usafiri wa anga
idadi iko wazi na inajulikana. Utaambiwa abiria waliosafiri,na sio waliokata
tiketi, bali waliosafiri ni 257, watumishi wa ndege(crew) ni 10, na hivyo waliokuwemo
jumla ni 267. Na inakuwa hivyohivyo
kweli hakuna kubabaisha. Kwanini
haiwi hivyo kwenye meli/vivuko. Leo ni
miaka 22 tangu MV Bukoba izame, nakuhakikishia hakuna wa kukwambia idadi halisi
ya waliofariki katika ajali hiyo, hayupo.
Leo ni miaka 7 tangu MV Spice
Islanders izame, nakuhakikishia hakuna wa kukwambia idadi halisi ya waliofariki
katika ajali hiyo, hayupo. Na leo nasema hakuna wa kukwambia idadi halisi
kabisa ya waliofariki kwenye kivuko cha MV Nerere, hayupo. Na huu ndio ukweli. Kadhalika katika meli zote hizo hakuna wa
kukupa idadi ya tani halisi ya mizigo iliyokuwemo bila kubabaisha, hakuna.
Sasa unaweza kujiuliza tunakabiliwa
na tatizo gani hasa, hatujui hesabu hizihizi
za kuhesabu 1-10 na.....,ni wazembe, ni wasiojali,ni wapuuzi, ni watu
ambao bado tunaishi maisha ya ujima,ni watu wa aina gani hasa. Watu ambao ulaya,
America na uchina wameanza kugawana maeneo mwezini ili wachimbe madini ya PLAGIOCLASE
sisi hatuwezi hata kuhesabiana
kwa hesabu ya darasa la kwanza.Tuseme nini hiki kama sio janga. Na
hakuna shaka kushindwa kuhesabiana ndiyo sababu ya ajali za majini . Hatuna ajali
ya majini ambayo idadi ya watu ilikuwa
sawa(capacity). Zote idadi ilizidi.
Tizama pale feli kigamboni. Vinafanya
kazi vivuko vitatu kwa kupishana na wote
tiketi mnachukua sehemu moja. Kama kinazama kivuko kimoja pale(mungu aepushie
mbali) nani anaweza kusema idadi ya
waliokuwemo. Kwasababu hata tukisema tuhesabu tiketi bado hutopata jibu
kwakuwa tiketi za kupanda kivuko
chochote kati ya vitatu zinakatwa sehemu mmoja, hivyo huwezi kujua aliyekata
tiketi amepanda kivuko kipi kati ya vitatu.
Lakini tizama watu wanavyoingia
kwenye kivuko. Geti likifunguliwa mpaka
mtu mwenyewe aseme kimejaa sana siingii, vinginevyo watu wote mlioko kwenye
banda la kusubiria mtaingia. Kivuko hiki kinabeba watu wangapi kwani. Kikija
kidogo wanaingia haohao, kikija kikubwa wanaingia haohao, Looh.Mwanzoni
nilifikiri kwakuwa safari ya feli - kigamboni ni ya karibu sana basi sio rahisi
kutokea janga, lakini MV Nyerere imenifunza mengi.
Hoja ni kwamba, kama huwezi kujua na ukawa na idadi halisi ya waliosafiri
maana yake huwezi kudhibiti
upakiaji unaozidi uwezo wa chombo. Kwanini, kwasababu unajua chombo kinahitaji
kupakia wangapi, lakini hujui wanaoingia huwa ni wangapi.Na hapa ndipo yalipo
majanga.
Sasa tubadilike, yatoshe tuliyofunzwa
na ulimwengu. Tunahitaji mifumo mizuri ya kuratibu upakiaji wa abiria na mizigo
katika vyombo vya majini. Uratibu unaanza na nani anawajibika na nini, vifaa
vya kutambua watu wanaoingia kusafiri, na sio mashine za kukatia tiketi tu, usimamizi wa kiwango cha juu kwenye vituo vya
meli na vivuko, kuondoa rushwa meneo hayo,mfumo wa uongozi katika bandari na
meli unaoanisha kwa uwazi wajibu wa kila mfanyakazi.
Isiwe kama ya MV Bukoba
kapteni anasema, ni chief officer, chief officer anasema ni 1st
officer, 1st officer anasema ni marine surveyor, marine surveyor
anasema port officer, yaani unakosa hata awajibike nani katika nini
mpaka mwisho watu wote wanaachiwa huru. Mfumo mzuri wa nani anawajibikia nini.
Watu wa marine wachukue semina ya usimamizi wa abiria na mizigo kwenye viwanja
vya ndege. Hakuna dhambi umakini uleule unaotumika kwa abiria na mizigo kwenye
viwanja vya ndege ukatumika maeneo ya bandarini kwasababu pote zinabebwa roho
za watu. Kwanini huku ionekana tahadhari kubwa ya abiria na mizigo wakati huku hakuna, na wanaobebwa wote ni
watu. Tusipofanya hivyo tukaendelea na uenyeji enyeji wetu huu, tujiwekee
guarantee ya kupokea misiba ya majini kila baada ya kipindi fulani.
Narudia tena tatizo lipo kwenye upakiaji,
soma ripoti zote za ajali za meli ni abiria na mizigo kuzidi. Hapa ndipo
tunatakiwa kushughulika napo. Yanitoshe haya kwa leo.
MWANDISHI WA MAKALA HII NI WAKILI
WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA NA MAHAKAMA ZA CHINI YAKE ISIPOKUWA MAHAKAMA YA
MWANZO, NA MCHAMBUZI WA MASUALA YA SHERIA NA SIASA. +255 784 482 959.
Hongera xana msomi, kwa uchambuzi wa kitaalamu na wenye kuelewekaa, makala hii inaonyesha uzalendo wako hakika huu ndio uzalendo,ujumbe huu ukiwafikia wa lengwa twaweza kuondoa tatizo. Hongera xana bro
Wapumzike kwa amani waliopoteza maisha yao katika ajali ya mv bukoba