NA BASHIR YAKUB -
Kuna tofauti kati ya gharama za kesi(costs), fidia (compesation),
na faini(fine). Gharama za kesi ni nje ya haya lakini pia ni nje ya kile
ulichoshinda. Kwasababu imeamriwa ulipwe fidia au imeamriwa ulipwe faini haimaanishi
hata gharama zinahesabika humohumo. Laa, hasha, kama ni fidia utalipwa,
kadhalika na gharama utatakiwa kulipwa.
Ukweli ni kuwa watu wengi huwa hawadai gharama za kesi . Mtu
akishaambiwa ameshinda basi. Kama imeamriwa alipwe pesa, au kama ni mali kama
ardhi imeamriwa arudishiwe, au ushindi mwingine wowote basi huondoka tu moja kwa moja bila kudai gharama
zake. Sasa yafaa ujue kuwa nje ya ushindi unaopewa na mahakama pia unatakiwa
kulipwa gharama zako za kuendeshea shauri/kesi.
1.GHARAMA ZA KESI NI
NINI .
Gharama za kesi ni yale matumizi yote halali uliyoingia
wakati ukishughulikia kesi/shauri husika. Hizi ni pamoja na nauli ulizokuwa
ukitumia kutoka nyumbani kwenda mahakamani kwa kipindi chote cha kesi/shauri
mpaka kuisha,pesa uliyomlipa wakili kama ulikuwa unawakilishwa na wakili, pesa
uliyotumia kumlipa wakili kuandaa nyaraka , pesa ya kuchapa(print),pesa ya kutoa kopi kwenye nyaraka mbalimbali ulizokuwa
ukiwasilisha mahakamani, na gharama nyingine yoyote ambayo uliingia wakati
ukifuatilia kesi/shauri.
Isipokuwa tu gharama hizo ziwe zile ambazo ni halali. Rushwa
na gharama nyingine za ajabu ambazo umeingia haziwezi kulipwa na ni makosa
iwapo ulifanya hivyo.
2. NANI HULIPA GHARAMA
ZA KESI/SHAURI.
Aliyeshindwa hutakiwa kumlipa aliyeshinda. Mfumo wetu wa
jumuia ya madola(common law) hakuna utaratibu wa kila mtu/upande kushinda(win
win situation). Badala yake kuna mfumo wa shinda shindwa(win loose situation).
Mmoja lazima atangazwe mshindi na mwingine mshindwa.
Kwahiyo yule aliyetangazwa kushindwa
anawajibika kumlipa gharama aliyeshinda.
Na haijalishi iwapo huyo aliyeshinda alikuwa mlalamikaji/mshitaki, au alikuwa
mlalamikiwa/mshitakiwa.Suala ni kwamba ameshinda basi alipwe gharama zake.
3. NANI ANAAMRISHA GHARAMA KULIPWA.
Hakimu au jaji aliyekuwa anasikiliza shauri/kesi husika ndiye
anayetoa amri ya kulipwa gharama. Isipokuwa wewe mlalamikaji au mlalamikiwa
unatakiwa kuomba gharama hizo. Na wakati wa kuomba kulipwa gharama ni wakati ule
kesi inapokuwa inaendelea.
Gharama hazitolewi moja kwa moja ispokuwa unaomba.
Na wakati wa kuomba ni huo wakati shauri/kesi inaendelea.
4. USHAHIDI KUWA
UMETUMIA GHARAMA.
Ni muhimu sana wakati kesi ikiendelea kuwa unaomba kupewa,na
kutunza risiti ya kila gharama unayoingia. Hata ukitoa kopi omba risiti ili ije
kuwa ushahidi wako wa gharama. Gharama ambayo huna risiti yake inaweza
kukataliwa. Hii husaidia pia kutotumia nafasi hiyo kumkomoa mtu ili alipe zaidi
hata kwa kile ambacho hukutumia.
Kwahiyo unashauriwa tangu siku ya kwanza
uapopokea wito wa kuitwa mahakamani, au siku ya kwanza kufungua kesi/shauri,
hakikisha kila hatua yako unakuwa na risiti ili uje kulipwa gharama zako.
5. WAKATI GANI GHARAMA
HULIPWA.
Gharama hulipwa mwishoni kabisa baada ya kesi/shauri kuisha. Gharama
haziwezi kulipwa kabla ya kesi/shauri kuisha kwasababu kabla ya hapo unakuwa
hujajua umetumia kiasi gani. Kesi haijaisha maana yake bado unaendelea kutumia
na hivyo huwezi kufanya majumuisho ya gharama.
Kwahiyo gharama italipwa
mwishoni kwakuwa hapo ndipo unapoweza kufanya majumuisho kuanzia mwanzo wa kesi/shauri
lilipoanza hadi mwisho lilipoisha,na kujua umetumia kiasi gani.
Ni vema sasa ufahamu kuwa nje ya kushinda na kuambiwa ulipwe
fidia, urudishiwe nyumba/kiwanja, au ushindi mwingine wowote, pia uwe
unakumbuka kulipwa gharama ambazo umeingia katika kushitaki au kujitetea.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment