NA BASHIR YAKUB -
Tokea April mwaka huu 2018 utaratibu wa kusajili kampuni
umebadilika. Ni tofauti kabisa na ambavyo tulizoea.Hata hivyo, yapo mambo
ambayo yamebaki vile vile kama awali, kadhalika yapo mengi pia yaliyobadilika.Tutapitia
utaratibu wa awali kidogo na huu mpya.
UTARATIBU WA AWALI.
a ) Ulikuwa unatakiwa kuandika barua kuuliza jina unalotaka kutumia
kama jina la kampuni iwapo lipo au
hapana. Kama lipo ungetakiwa kuleta jingine, na kama halipo ulikuwa unapewa
ruhusa ya kulitumia katika usajili.
b ) Ulikuwa unatakiwa kuandaa waraka na
katiba ya kampuni(article and memorandum of association). Zilikuwa zinatakiwa
kwa uchache angalau nakala nne.
c ) Ulikuwa unatakiwa kupakua fomu namba
14(a) na 14( b ) kutoka kwenye mtandao wa BRELA, au kuzifuata fomu hizo hapohapo
BRELA ambapo ungetakiwa kuzijaza kisha kuzisaini.
d ) Kisha ulikuwa unatakiwa kubeba hizo nakala za waraka na
katiba ya kampuni, pamoja na hizo fomu zilizojazwa na kuzipeleka BRELA mnazi mmoja jengo la ushirika kwa ajili ya
usajili.
e ) Huko BRELA, baada ya kuzipitia na
kuona hazihitaji masahihisho sasa ungepewa ruhusa ya kulipia ambapo malipo
yalikuwa yakifanyika kupitia benki ya CRDB.
f ) Baada ya hapo ungetakiwa kusubiri kipindi cha wiki moja au
wiki na sikukadhaa, au wiki mbili ili
uweze kupatiwa cheti rasmi cha usajili
wa kampuni(certificate of incorporation).
UTARATIBU MPYA.
a ) Hitaji la kwanza kabisa katika utaratibu mpya ni lazima uwe
na kitambulisho cha taifa. Sio kile cha mpiga kura bali kile cha NIDA. Hiki ni
lazima. Na si lazima tu kwa yule anayetaka kufungua kampuni, bali lazima kwa
yeyote ambaye atakuwa mwanahisa katika kampuni(shareholder), au ataandikwa(subscribe)
kama mkurugenzi katika kampuni.
Kwa ufupi yeyote anayeingia kwenye nyaraka za kampuni ambazo zinatakiwa
kuwasilishwa BRELA kwa ajili ya usajili wa kampuni ni lazima awe na
kitambulisho hiki.
Lakini pia tokea mabadiliko haya yafanyike, muamala wowote
unaotakiwa kuufanya kuhusiana na kampuni
mathalan kubadili jina(name change), kubadili aina ya kampuni, kubadili
wakurugenzi, kuongeza au kupunguza wanahisa au hisa, mrejesho wa mwaka(annual
return), kuuliza hadhi ya
kampuni(official search) nk, lazima uwe na kitambulisho hiki.
b ) Lazima ufungue akaunti au mtu
mwingine mwenye akaunti akusaidie kukusajilia. Usajili wa sasa unafanyika
kwenye mtandao kupitia akaunti iliyofunguliwa na mhusika anayehitaji kufungua
kampuni.
Kufungua akaunti unaingia kwenye WEBSITE ya BRELA humo utaona maelekezo ya kufungua akaunti ambayo kimsingi
sio yenye utata(complicated). Kufungua akaunti ni rahisi sana sharti kubwa ni uwe tu na kitambulisho nilichoeleza hapo juu
kwenye “a”.
c ) Ukishakuwa na akaunti basi utaSCAN
waraka na katiba ya kampuni(memorandum & article of association) ,
kadhalika uta SCAN fomu zote zilizojazwa taarifa husika, utajaza taarifa za
ziada kwenye mtandao kwenye akaunti yako kisha utatuma BRELA.
d ) Ada za usajili sasa unalipia kwa njia ya mtandao wa
simu tigopesa, Mpesa Airtel Money nk, au
benki ukitaka iwe hivyo.
e ) Muda wa kusubiri usajili nao umepungua ambapo kama kila kitu
kimefanyka vizuri unaweza kusubiri chini ya wiki moja ili upate cheti cha
usajili wa kampuni(certificate of Incorporation).
f ) Cheti cha usajili nacho kikiwa tayari kinatumwa moja kwa
moja kwenye akaunti yako, na wewe hukohuko uliko utakichapa(print) na kuanza
kukitumia bila kuhitaji kwenda BRELA kukifuata kama ilivyokuwa awali.
Ada, masuala ya uandaaji wa nyaraka na kuzijaza taarifa,
kuzisaini ikiwa ni pamoja na kuzigonga mihuri ya wakili yamebaki vilevile.
Kubwa lililobadilika ni hitaji jipya na kitambulisho cha taifa, na usajili
kupitia mtandao kutoka mfumo wa usajili wa ana kwa na(physical/manual).
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment