Monday 17 September 2018

BODABODA,BAJAJI,TAXI KUSHINDWA KULETA HESABU NA KUKUSABABISHIA HASARA,NINI UFANYE KISHERIA.


Image result for BODABODA BAJAJI


NA  BASHIR  YAKUB -

Sio siri wengi waliowekeza kwenye biashara ya bajaji,bodaboda,taxi na hata daladala wamejuta kufanya hivyo. Wengi wameingia hasara na mambo hayakuwa kama walivyotarajia. Na niamini,waliomo leo kwenye hiyo biashara sio wale walioanza, bali ni wageni kwani walioanza walishaacha siku nyingi kuepuka kichwa kuuma.

Sasa yafaa tuzingatie mambo kadhaa ya kisheria ili kuona  namna gani unaweza kudhibiti biashara hii na hata ikikushinda isikushinde ukiwa mwenye kupoteza(looser).Katika kufanya hivyo tutizama mambo mawili, kwanza Mkataba, na pili Udhamini.

1.MKATABA.

Eneo la mkataba au makubaliano ni eneo muhimu  sana tangu unapowaza biashara hii. Mkataba ndiyo tafsiri ya uhusiano wako na huyo unayemkabidhi chombo. Popote, na wakati wowote mtakapotofautiana  rejea yenu ya kwanza ni mkataba. Mkataba ndio biashara yenyewe, na hivyo uimara wa mkataba utatambulisha uimara wa biashara,  halikadhalika udhaifu wa mkataba huenda ukawa ndio udhaifu wa biashara.

Na uimara wa mkataba ni sehemu kuu mbili. Kwanza mfumo, na pili maudhui/vipengele. Mfumo ni lazima mkataba uwe katika muundo mzuri wa sheria. Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba, Sura ya 345 kinasema mkataba  mzuri ni ule ambao umefanywa na watu stahili kufanya mkataba(partie’s competence), wenye hiari huru(free consent), wakibadilishana vitu halali(lawful object and consideration ), na kile wanachokubaliana kiwe hakijakatazwa na sheria nyingine yoyote. Kwahiyo mfumo mzuri wa mkataba utategemea haya.

Upande wa pili tumesema ni upande wa maudhui/vipengele. Hapa tunaongelea masharti(conditions/terms). Haya ni yale ambayo mnataka yatekelezwe. Hapa napo ni sehemu muhimu sana kwasababu panabeba lipi litakuwa likifanyika na lipi hapana. Hapa ndipo patakaposema hesabu ni kiasi gani, italetwa kila baada ya muda gani, nani atakabidhiwa, endapo isipoletwa kabisa au ikaletwa nje ya muda nini kitokee, chombo kitatunzwa vipi, nani atabeba uharibifu ndani ya chombo, kesi ya kuibiwa au kupotea inakubalika kwa misingi ipi nani atabeba hasara hiyo, endapo dereva akipotea nani atafutwe kwa niaba yake, nk,nk.

Hii ni sehemu huru ambayo  mipaka yake ni pale litakapoingizwa sharti lolote la kuvunja sheria nyingine ya Tanzania. Kama halipo, mtaweka sharti lolote na mbingu ndiyo itakuwa mpaka(sky is the limit).

2.   UDHAMINI.

Kwa dhati kabisa kama mtu anahitaji ajira/kazi kwenye chombo chako hakikisha  anaye mdhamini.  Alete mdhamini na kama hana atafute kazi kwingine asikutie kwenye majaribu. Sehemu ya VIII ya Sheria ya Mikataba,Sura yas 345 imeeleza habari ya udhamini na kufidia hasara(indemnity). Mdhamini ni mtu wa lazima kwenye makubaliano ya aina hii na hasa kwa namna biashara hii inavyoumiza kichwa. 

Kutakuwa na mikataba miwili, mmoja kati yako mwenye chombo na dereva, na pili kati yako mwenye chombo na mdhamini. Dereva ataleta mdhamini wake na wewe kazi yako itakuwa ni kumtathmini(asses) kama anafaa au hapana.

Aidha,mkataba wako  na mdhamini utaeleza wazi kuwa mdhamini atabeba hatia yote(full liability)  ya dereva pale ambapo kutatokea hasara, na/au dereva akapotea,na/au akapatikana lakini akawa hana uwezo  wa kufidia hasara, nk, nk.
Mdhamini awe ni mtu kuaminika, mwenye makazi  yanayotambulika, na awe mtu ambaye kweli anaweza kubanwa akafidia endapo litatokea la kutokea.

Aidha, mdhamini sio lazima awe mtu wa tatu(third party). Hata dereva mwenyewe anaweza kujidhamini ikiwa atakubali kuweka rehani mali yake yoyote isiyohamishika au inayohamishika ambayo utakuwa na uhakika kuwa italinda chombo chako. Huu ni utaratibu ambao umekuwa ukitumiwa na taasisi za fedha kuhakikisha kwamba haziingii hasara.  Na sisi wajasiriamali  wa hii biashara tukiuasili(adopt) utaratibu huu,tukautumia hakika utasaidia na hatutaingia hasara. Utapata usingizi, na utaepuka kurudishwa nyuma na watu ambao bado wako kwenye mchezomchezo, ambao bado  hawako makini(serious) na maisha.    

Kwa machache haya niseme kuwa kuna umuhimu wa kuyatilia maanani  yaliyosemwa humu,  ili sasa tukomeshe tabia ya kurudishana nyuma. Wale ambao tayari wameingia makubaliano lakini hawakufanya hivi bado hawajachelewa wanaweza kuitisha makubaliano mapya. Na wale ambao wanatarajia kuingia kwenye hii biashara basi itakuwa vema kwao walau wakifuata utaratibu huu.

Niseme tu kuwa biashara hii ni nzuri,yenye faida ila taswira yake imeharibiwa na  madereva walio wengi.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


1 comments:

  • Dennis Moyo, Mshauri wa masuala ya media says:
    9 February 2023 at 04:07

    Kweli kabisa. Kuingia mkataba ni rahisi. Lakini namna ya kum'bana pindi anapolega lega kutekeleza yaliyomo ndani ya mkataba ndo inakuwa kasheshe. Mdhamini ni kipengele muhimu sana kt Mkataba. Wengi tunachukulia poa tunapoingia mkataba wa mamilioni ya shilingi. Hadi pale machungu yanayoingia ndipo tunakumbuka umuhimu wa udhamini. Asante sana Mh. Bashiri Yakub.

Post a Comment