NA BASHIR YAKUB -
Ni fomu namba 3 katika kanuni za Sheria ya usajili wa ardhi .Inatokana
na kifungu cha 38 cha Sheria ya Usajili wa Ardhi Sura ya 334. Fomu hii kazi yake ni kuombea hati mpya ya ardhi baada ya ile uliyokuwa nayo mwanzoni kupotea.
Hati, sawa ilivyo kwa vitu vingine vyote inaweza kupotea, kuibiwa au
kuharibiwa. Mazingira ya matukio haya yote yameandaliwa majibu na sheria za
ardhi. Fomu hii namba 3 ni rasmi kwa
waliopoteza hati na hivyo kutaka kupata
hati mpya.
Fomu hii hutakiwa kujazwa na mhusika yaani yule ambaye jina
lilikuwa linasomeka kwenye hati iliyopotea. Kama lilikuwa likisomeka jina la
kampuni basi wale waliokuwa wamesaini ile hati iliyopotea awali ndio wasaini na
kujaza fomu hii. Anaweza kuwa mkurugenzi wa kampuni ama katibu wa kampuni.
Msimamizi wa mirathi pia anaweza kujaza na kusaini fomu hii
ikiwa jina lililo kwenye hati iliyopotea ni la mtu ambaye sasa ni marehemu. Isipokuwa
sasa kwa msimamizi wa mirathi ni lazima awe na fomu za kuthibitisha kuteuliwa
na kuthibitishwa na mahakama kuwa msimamizi wa mirathi. Ikiwa msimamizi wa mirathi
ni zaidi ya mmoja basi wote watajaza
fomu hii ya kuomba hati mpya na watasaini .
Yafaa tujue kuwa kabla hujajaza fomu hii ni muhimu ukawa tayari
umetafuta na kupata taarifa ya
kupotelewa(lost report) kutoka kituo cha polisi. Taarifa ya Kupolewa si tu ni muhimu, bali pia ya lazima kwani ndio itakayoambatanishwa
kwenye hii fomu ya kuomba hati mpya. Msajili wa hati hawezi kujua kama kweli
umepotelewa na hati kama hakuna taarifa hii.
Na ni ushauri kuwa kitu cha kwanza unachotakiwa kufanya unapopotelewa na
hati ni kutoa taarifa polisi na kupata taarifa rasmi ya kupotelewa.
Basi unapokuwa umejaza fomu ya kuomba hati mpya, na
umeambatanisha taarifa ya kupotelewa, peleka nyaraka hizo kwa msajili wa hati.
Mamlaka za ardhi zina vitengo vingi, ila kitengo rasmi kinachohusika na maombi
haya ni ofisi ya msajili wa hati. Kwahiyo peleka hapo nyaraka zako. Msajili wa
hati anaweza kuomba taarifa nyingine zaidi za uthibitisho kuhusu kupotelewa
kwako. Anaweza kuomba kiapo au vinginevyo ili kujiridhisha. Hicho atakachoomba
utatakiwa kukiwasilisha ili maombi yako
ya hati mpya yaweze kukubaliwa.
Fomu husika ya kuombea hati mpya ina maeneo makuu mengi.
Kwanza, ni kichwa ambacho huandikwa “maombi
ya kuomba hati mpya”. Pili, kuna sehemu
ya picha. Picha kwa maana ya paspoti size moja ambayo itakaa upande wa kulia wa
fomu husika. Kimsingi picha zinatakiwa kuwa tatu kwakuwa fomu zitatakiwa kuandaliwa tatu pia ili kila
fomu ipate picha moja. Hata kujaza na kusaini
kama ilivyoelekezwa hapa juu itakuwa ni hivyohivyo fomu tatu zote.
Fomu ina sehemu ya mtu kueleza jina lake lile lililokuwa likitumika
kwenye hati ya awali pamoja na anuani
yake. Kuna sehemu ya kueleza kuwa hati imepotea hali kadhalika maelezo ya namna
ambavyo imepotea. Pia yapo maelezo ya kiapo kwenye hiyo fomu kuwa ni kweli hati
imepotea na haijawekwa sehemu nyingine yoyote kwa makusudi mengine. Mwisho tarehe
ya kujaza fomu na sahihi ya muombaji/waombaji. Kisha itashuhudiwa na
Wakili. Wakili atasaini na kugonga
mhuri.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment