NA BASHIR YAKUB -
Kawaida safu hii
huandika na kufafanua masuala mbalimbali ya kisheria na mahakama. Mara nyingi huandika kuhusu ndoa, mirathi,
makampuni, jinai, ardhi, na madai mengine kwa ujumla. Leo itakuwa tofauti
kidogo japo ni ndani ya tasnia ya sheria humohumo.
Nianze tu kwa kusema kuwa wakati taifa zima likifanya kazi
kufikia uchumi wa kati ambao ndio dira ya mihimili yote mahakama,bunge na
serikali, kuna jambo moja ambalo hatuwezi kulisahau. Jambo hili ni utumishi uliotukuka.
Hakuna ubishi, injini ya uchumi wa kati ni watumishi. Lakini ni aina gani ya
watumishi ambao ni injini ndilo litakuwa swali. Aina ya watumishi ambao
wanaweza kutufikisha huko ni wale wenye
moyo wa kazi, ari, uvumilivu, waelewa,na wale ambao utumishi kwao sio kazi tu
ya kusubiri mshahara mwisho wa mwezi,
bali pia huduma nzuri kwa watu.
Kote duniani ambako si
tu wamefikia uchumi wa kati tunaoulilia, bali pia wana uchumi wa juu kama
china, amerika, na nchi za ulaya wamefikishwa hapo na watumishi bora .
Waliowahi kufika huko wanajua ni namna gani watumishi wa huko wanavyotoa huduma.
Unaweza kudhani unahudunmiwa na ndugu yako wa tumbo moja.
Niseme tu kuwa watumishi
wa mahakama kuu ya Dar es salaam kitengo cha mawakili wameonesha mfano wa aina
hii. Ni aina ya watumishi ambao ukibahatika kuhudumiwa nao unahisi kweli
umepewa huduma. Hawatachoka kukupatia maelezo, hawatachoka kukuelekeza, na hata
ukitaka namba zao binafsi hukupatia, na endapo utapiga muda wowote kutaka
ufafanuzi utapewa bila kukaripiwa kama ambavyo imekuwa pahala pengine pa utumishi.
Ni muhimu sana, tena sana kumpatia sifa anazostahili yule ambaye amefanya vizuri. Kadhalika
kumuonya yule ambaye hajafanya vizuri. Tumekuwa tukipenda sana kukosoa na kulalamika huku tukiacha kusifia na
kusemea yaliyo mazuri. Hii ni desturi mbaya kabisa na inavunja moyo. Hata awe
Rais , Jaji mkuu au Spika na ukubwa wao wote, pale ambapo wanafanya mambo mazuri
badala ya kusifia tukakosoa tu, nao huwa tunawavunja moyo.
Nimefanya kazi za mahakama kwa muda mrefu kabla sijawa wakili
na baada. Nawajua watumishi mbalimbali wa ngazi za mahakama kama makarani, watunza
kumbukumbu, wapeleka nyaraka(process server), wahasibu, nk. Sio siri wengi
wamekuwa wakilalamikiwa sana na wananchi. Masuala ya mafaili kupotea ilishaacha siku nyingi mno kuwa habari ya kushangaza . Namkumbuka mhasibu
mmoja wa kike mahakama ya wilaya kinondoni . Alikataa kutukatia risiti za
malipo watu kama sita hivi akasema ana kazi nyingine na hivyo turudi kesho, na
badala yake akahamia chumba kingine akawa anapiga gumzo na wenzake. Na anafanya hivyo akijua kabisa kuwa unapokata risiti ndipo
unapohesabika kuwa umeingiza nyaraka mahakamani ndani ya muda.
Kwahiyo
usipopata risiti leo maana yake kwa mujibu wa sheria umeingiza nyaraka mahakamani kwa kuchelewa na
hivyo inaweza ikawa mwisho wa kesi yako, yaani umepoteza. Hawa ndio wengi wa
watumishi wetu.
Niwataje na kuwapongeza wawili tu kwa niaba ya wengine
kitengo cha mawakili mahakama kuu Dar es salaam. Rajab Kagame na Mwenzake ndugu
Bedson Mariba hongereni sana. Mnafanya kazi nzuri na nyie ni mfano wa kuigwa.
Mawakili na wananchi wengine ambao hupata
huduma yenu hapo ni mashahidi wa hili. Anayefanya vizuri sharti aambiwe
ili aongeze na aamshe ari kwa wengine.
Nimalize kwa kusema kuwa utumishi sio tu ni kazi bali pia ni huduma, basi yafaa tufanye kazi kwa kutoa huduma.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment