NA BASHIR YAKUB -
Wapo watumishi wa umma ambao wameachishwa kazi kwasababu
mbalimbali na wanahisi kuwa pengine haki haikutendeka lakini hawajui la
kufanya. Basi waelewe la kufanya lipo na ni rufaa. Na wengine wanajua kuwa ni
rufaa yumkini wasijue rufaa yenyewe inakatwa kwa utaratibu upi. Nitaeleza hapa,
lakini kwanza tujue nani mtumishi wa umma anayeongelewa hapa.
1.NANI MTUMISHI WA
UMMA.
Sheria namba 8 ya 2002, Sheria ya Utumishi wa Umma ,
iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Namba 18 ya 2007 imemueleza mtumishi wa umma. Kifungu
cha 3
kinasema kuwa mtumishi wa umma ni yule anayefanya kazi katika ofisi yoyote
ya umma. Ili uelewe vizuri mtumishi wa umma anayeongelewa katika sheria hii na
katika makala haya ni yule
mfanyakazi/mwajiriwa wa serikali.
Kwahiyo watumishi wa bunge, maafisa wa mahakama, na wafanyakazi wa taasisi/kampuni
binafsi taratibu hizi za rufaa zinazoelezwa
humu haziwahusu.
Tunaongelea watumishi wa serikali kuu, za mitaa, mashirika ya
umma, idara na taasisi zote zilizopo chini ya serikali tukiondoa wale wa uteuzi
japo nao wanaongozwa na sheria hii.
2. HAKI YA RUFAA.
Unapokuwa umesimamishwa kazi rufaa ni haki yako ewe mtumishi.
Rufaa sio kuonesha ukorofi, sio kuwa mjuaji, sio kupingana na serikali, na sio
kukosa utiifu. Rufaa ni haki kama zilivyo haki nyingine za mshahara, likizo,
nk. Usiogope kukata rufaa kwani hata huyo aliyekusimamisha kazi naye akisimamishwa
anakata rufaa.
Kifungu cha 25( 1 ) (b) cha Sheria ya utumishi wa umma ndicho
kinachoeleza haki hii.
Kadhalika kwenye barua yako ya kuachishwa kazi au siku ya kusimamishwa, yafaa na ni haki
uelezwe haki hii ya rufaa.
3. KUSHUSHWA CHEO NAKO
KUNAKATIWA RUFAA.
Rufaa sio kwa ajili ya kusimamishwa kazi tu. Kifungu hichohicho
cha 25 cha Sheria ya Utumishi wa Umma kinasema rufaa pia inaweza kukatwa iwapo
umeshushwa cheo , au mshahara wako
umepunguzwa. Kwahiyo haki ya rufaa kwa mtumishi ni pana na haikomei kwenye
kusimamishwa kazi pekee.
4. RUFAA INAKATWAJE?.
Rufaa ni maelezo mazuri yenye hoja za kimazingira, yaani kile
kilichotokea(facts), yakisaidiwa na hoja za kisheria(point/s of law). Na
itakuwa katika mfumo wa maandishi. Itakuwa na sehemu kuu tatu,yaani kichwa, hoja na hitimisho.
Kichwa chaweza kuwa “RUFAA YA KUPINGA KUSIMAMISHWA KAZI”.
Hoja, Utaeleza kile kilichotokea/
unacholalamikia kwa maana ya yale
maeneo(areas/aspects) unayohisi kuonewa, na kisha utaeleza sheria zinasemaje,
au sheria zipi zilikiukwa wakati ukiwajibishwa.
Ni kitu ambacho unaweza kuandika na wala huna haja ya kuhofu.
Ni maelezo ya namna ulivyoonewa + Sheria zinasemaje au sheria zipi zimevunjwa. Pia taratibu za kukuwajibisha, mfano
kutosikilizwa kabla ya kuadhibiwa,
kupewa mda kidogo wa kujitetea, kutoitwa kwenye kikao cha nidhamu nk, nayo ni
maelezo ambayo unaweza kuingiza eneo hili la hoja.
Hitimisho. Hapa utaomba maamuzi ya awali ya kufutwa kazi
yabatilishwe na rufaa yako ikubaliwe/ishinde, utaomba urejeshwe kazini, kisha utaandika jina lako, nafasi yako (uliyofutwa/cheo),
na utaweka namba yako ya simu.
5. RUFAA IPELEKWE WAPI.
Ukishaandaa rufaa sheria inakutaka kuipeleka tume ya utumishi
wa umma. Ofisi zao kwasaasa zipo pale Ubungo Plaza kwa Dar es salaam. Hiyo ni
kwa mujibu wa kifungu cha 25 (1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma.
Pia unapokuwa umeandaa yale maelezo yako ya rufaa yafaa
nakala uipeleke kwenye mamlaka/ofisi iliyokuwajibisha/iliyokufuta kazi. Hii ni
kwa mujibu wa kanuni ya 61( 1 ) Kanuni
za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003.
6. MUDA WA KUKATA
RUFAA.
Kanuni ya 61( 1 )
Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003
inasema kuwa rufaa inatakiwa
kukatwa ndani ya siku 45 tokea siku yalipotolewa maamuzi ya kufutwa kwako
kazi. Utehesabu siku 45 na ndani mwake uwe umekata rufaa.
7. KUCHELEWA KUKATA RUFAA.
Kanuni ya 61( 4 )
Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003 inasema kuwa mtumishi aliyechelewa
kukata rufaa ndani ya muda wa siku 45 rufaa yake inaweza kupokelewa ikiwa tu
anazo sababu za msingi za kuchelewa.
Hivyo basi, unapokuwa umechelewa na kupitwa na muda unachotakiwa
kufanya ni kuandaa maelezo ya kuchelewa kwanza kabla ya maelezo ya rufaa. Utaeleza
kwanini umechelewa na kama una ushahidi wa sababu za kuchelewa utaambatanisha
kwenye maelezo yako. Kisha utaeleza rufaa yako kama ilivyoelekezwa hapo juu.
Maelezo yakuchelewa na maelezo ya rufaa yanakuwa ni maelezo
kwenye nyaraka moja isipokuwa unaanza kueleza kuchelewa kwako na kuomba rufaa
yako ipokelewe nje ya mda, kisha kwenye nyaraka hiyohiyo unatoa hoja zako za
rufaa kama ilivyoelekezwa hapa juu. Halafu unasaini na kupeleka kwa ajili ya mawasilisho.
8. VIAMBATANISHO VYA RUFAA.
Rufaa yako inatakiwa iambatanishwe(annexeture/s) na nakala ya maamuzi ya kufutwa kwako kazi.
Barua ya kufutwa kazi ndiyo maamuzi ya kufutwa kazi ambayo nakala yake(kopi) unatakiwa
kuambatanisha nyuma ya maelezo yako ya rufaa. Pia kama unavyo vielelezo
vingine(exhibit/s) vinavyosimamia hoja
zako navyo waweza kuviambatanisha. Kwahiyo ni muhimu kupewa barua ya kufutwa kazi
mara tu unaposimamishwa.
9. USUBIRI MAJIBU YA RUFAA BAADA YA MUDA GANI ?.
Kanuni ya 62( 2 )
Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003, inasema kuwa ndani ya siku 90 tokea
siku ilipopokelewa rufaa unapaswa kupokea majibu ya rufaa hiyo. Hivyo ikifika
muda huo na ukaona kimya yafaa ufuatilie hukohuko ulipopeleka ili kujua kulikoni.
10. HAKI ZAKO NI ZIPI IKIWA
RUFAA YAKO IMESHINDA ?.
Kifungu cha 25( 1 ) ( e ) cha Sheria ya Utumishi wa Umma
pamoja na Kanuni ya 60( 6 ) Kanuni za
Utumishi wa Umma vinasema iwapo rufaa itashinda basi mtumishi aliyekuwa
amefukuzwa atahesabika kama ambaye hakuwahi kufukuzwa. Maana yake haki zote za mishahara
muda uliosimama, haki za likizo, na mengine utastahili kupata ikiwemo kurejea
kazini mara moja.
11. NINI UFANYE RUFAA YAKO IKISHINDWA.
Bado unakuwa na nafasi ya rufaa ikiwa tume itaamua kuwa rufaa yako
imeshindwa. Kifungu cha 25( 1 ) ( d ) cha Sheria ya Utumishi wa Umma pamoja na
Kanuni ya 60( 5 ) Kanuni za Utumishi wa
Umma vinasema kuwa , mtumishi ambaye hakuridhishwa na maamuzi ya tume ya rufaa
anaweza kukata rufaa tena kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Rais ndiye mkuu wa
watumishi wote na maamuzi yake yatakuwa ni ya mwisho na hakutakuwa na rufaa nyingine
tena isipokuwa sasa ukiamua kubadilisha mwelekeo/upepo na kwenda mahakamani.
Haya ndiyo ya msingi kuhusu rufaa ya mtumishi wa umma.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment