NA BASHIR YAKUB -
Wapo watu wana matatizo na wanahangaika kupata msaada wa bure
wa kisheria lakini hawajui waanzie wapi,wafanye nini ili kupata huduma hii. Taratibu
zipo, na unaweza kupata wakili wa kusimamia kesi yako bure bila malipo kupitia
utaratibu wa msaada wa kisheria. Unaweza kupata uwakilishi huu katika kesi zote yaani zile za jinai pamoja
na zile za madai.
Tunapoongelea za jinai tunamaanisha zile kesi za kuua,kubaka,
kupiga,kutukana nk, na tunapoongelea kesi za madai tunamaanisha zile za ardhi kugombea mali,
mirathi, ndoa, mikopo,watoto malezi, talaka, nk.
Kwahiyo pote kwenye jinai na madai unaweza kupata uwakilishi
wa bure wa Wakili. Utasimamiwa kesi yako mwanzo hadi mwisho bila kuhitaji
kulipa gharama yoyote. Na msaada wa kisheria unaweza kuwa wa uwakilishi kwa
maana kuwa wakili utakusimamia mahakamani au unaweza kuwa wa ushauri tu bila
kuhusisha mahakama au vyote kwa pamoja.
Lakini yafaa tufahamu kuwa sio watu
wote wanaweza kupata msaada huu. Makala yataeleza utaratibu wa kupata msaada wa
kisheria bure halikadhalika ni watu wa aina gani wanaweza kupata msaada huu.
1.WANAOSTAHILI KUPATA
MSAADA WA KISHERIA BURE.
i)Watu wasiojiweza kabisa kifedha.
ii) Wanawake.
iii)Wazee.
iv)Walemavu.
v) Watoto.
vi)Wagonjwa wasiojiweza.
Hata hivyo kwa wanawake, walemavu,wagonjwa wasiojiweza, na
wazee bado nao sifa ya kutokuwa na uwezo wa kifedha inatizamwa. Haimaanishi
kila mwanamke,mzee,mgonjwa au mlemavu anastahili msaada wa kisheria wa bure.
Sifa ya kutokuwa na uwezo kifedha ni sifa kuu inayoangaliwa. Isipokuwa kwa
watoto hata kama mzazi au mlezi ana uwezo, bado mtoto anaweza kupatiwa msaada
huu kwakuwa kinachoangaliwa ni maslahi ya mtoto mwenyewe wala sio ya mzazi ama
mlezi.
2. UTARATIBU WA KUOMBA MSAADA WA KISHERIA.
Utaratibu utategemea kama tatizo lako ni madai au jinai.
i)Madai.
Ikiwa ni madai kwa
mfano masuala ya ardhi, mirathi,ndoa, watoto, nk utatakiwa kutafuta vituo vya
misaada ya kisheria. Vituo hivi ni zile asasi(NGO) zisizo za serikali
ambazo hutoa misaada ya kisheria. Kila
mkoa zipo na hutofautiana mkoa hadi mkoa.
Kama hujui zilipo basi waweza kwenda eneo la mahakama na hapo
utauliza wapi nitapata shirika la msaada
wa kisheria na hapo utaelekezwa. Pia unaweza
kuuliza makao makuu ya wilaya kwani
orodha ya mashirika huwa ipo hapo pia . Zaidi, unaweza kuuliza kwenye ofisi za
mawakili wa kujitegemea ili uelekezwe mashirika ya msaada yalipo. Na kwa wanaojua
kutumia mtandao, humo pia unaweza kutafuta ukapata. Maeneo haya utapata majibu
sahihi ya wapi yalipo mashirika ili usaidiwe.
Ukilipata shirika husika basi watakupa utaratibu wao lakini zaidi huwa ni kujaza fomu maalum na
kuleta barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa inayokutambulisha na
kuelezea hali yako ya kiuchumi. Taratibu nyingine ni za kawaida na hapo
utapata ushauri wa kisheria bure au wakili wa kukuwakilisha bure bila malipo
yoyote.
ii) Jinai
Sura ya 21 ya Sheria ya Msaada wa Kisheria katika Jinai ndiyo
hueleza utaratibu wa msaada wa sheria katika jinai. Kifungu cha 3( 1 )
kinaeleza makosa ya jinai ambayo unaweza kuombea msaada wa kisheria kuwa ni
yale ambayo adhabu zake haziko chini ya
kifungo cha miaka 15, adhabu za kifo, maisha, adhabu ya kuondolewa ndani ya nchi,
na sifa nyingine zilizotajwa hapo juu mwanzoni awali.
Utaratibu wa kupata msaada hapa kama huna uwezo ni kuomba kwa
hakimu husika au jaji kuwa unaomba kupata msaada wa uwakilishi kwasababu huna
uwezo. Muombe huyuhuyo hakimu au jaji anayesikiliza kesi yako. Na unaweza
kumuomba mda wowote hata mara ya kwanza tu unapofikishwa mbele yake. Yeye
anajua ni utaratibu gani afuate ili upate wakili wa kukuwakilisha bure bila malipo
yoyote.
Na usiogope kumuomba hakimu/jaji kwani kufanya hivyo ni haki
yako, na takwa la kisheria na wala sio kosa au ujuaji(much know).
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment