NA BASHIR YAKUB -
Ni miaka mingi tangu kesi yako imefunguliwa mahakamani lakini haiishi.
Huelewi ni kwanini na kila siku ukienda ni tarehe juu ya nyingine.
Mwingine atakwambia kesi yangu ina miaka zaidi ya kumi
na bado haijaisha nk. Tatizo
hujui nini zaidi ya kupata kalenda kila
siku. Basi makala yataeleza hatua ambazo unaweza kuchukua kumaliza tatizo hili.
Aidha, Ibara ya 29(2 )
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka bayana kuwa kila raia wa
Tanzania ana haki ya kupata ulinzi wa sheria. Basi sio sawa ukimbilie
mahakamani kupata ulinzi wa sheria halafu usipate ulinzi huo hata baada ya
miaka mingi.
CHUKUA HATUA HIZI KAMA KESI YAKO IMECHELEWESHWA BILA SABABU ZA MSINGI.
( 1 ).Tafuta ushauri wa kisheria kutoka
kwa mwanasheria,hata wale wa msaada wa sheria. Utamwelezea ishu yako nzima na
wapi umekwama. Huyu atakusaidia kutambua kama imechelewa kwa makusudi, kwa
uzembe, au ni sababu tu za kisheria zimesababisha ichelewe.
Wakati mwingine kesi inaweza kuchelewa kwasababu za kisheria
ambazo ziko juu ya uwezo wa mahakama kuiharakisha kesi yako, kwa mfano
mapingamizi ya mara kwa mara, maombi ya mara kwa mara, upelelezi kuchelewa nk,
nk. Hii ndiyo sababu utamtafuta mwanasheria ili abainishe(identify) nini hasa
chanzo cha kukwama kwa kesi yako. Atakwambia kama umeonewa au sheria ndivyo
ilivyo.
( 2 ). Toa malalamiko yako kwa jaji au hakimu
anayesikiliza kesi yako. Usiogope kumwambia Jaji au hakimu kuhusu kuchelewa kwa
kesi yako.Kumwambia ni haki yako na hutaambiwa kuwa umekosea au umeidharau
mahakama.
Na unaweza kumwambia kwa njia
mbili, moja kwa mdomo, na pili kwa
kumwandikia barua.
Kwa mdomo utamwambia wakati wowote kesi itakapokuwa
ikiendelea mahakamani, baada ya kunyoosha mkono na kumuomba kuwa kuna jambo unataka
kumwambia, na kwa maandishi utaandika barua na kuipeleka masijala,au kwa karani
wake, au namna nyingine utakavyoelekezwa na wahusika pale mahakamani. Usitukane
wala kusema/kuandika maneno ya hovyo, eleza tu lalamiko la kesi yako kuchelewa
na utasaidiwa.
( 3 ). Kama hukupata msaada hapo juu, basi
peleka malalamiko yako kwa hakimu mfawidhi, jaji mfawidhi, au hata kwa msajili.
Hakimu mfawidhi ni hakimu kiongozi wa eneo la mahakama husika. Kwahiyo kama
kuna mahakimu wengi eneo lile la mahakama yeye ndiye kiongozi wao.
Na
utampataje/utamjuaje, ni kwa kuuliza tu. Uliza hakimu mfawidhi ni nani na mpe malalamiko
yako. Unaweza kufanya hivyo kwa mdomo/mazungumzo au kwa barua kama tulivyoona
hapo juu.
Wakati mwingine hakimu mfawidhi anaweza asiwe anakaa eneo la
mahakama bali yuko huko wilayani au pengine. Bado si tatizo, uliza na peleleza ujue alipo mfuate na mpe
malalamiko yako au mwandikie. Hii ni kwa wale ambao kesi zao zipo mahakama za
mwanzo, za wilaya na zile za hakimu mkazi.
Kwa wale ambao kesi zao zipo mahakama kuu, Jaji mfawidhi
ndiye kiongozi wa eneo husika na majaji wote wa eneo hilo anawaongoza yeye.
Unaweza kumpatia huyu malalamiko yako kwa njia ya mdomo/mazungumzo, au kwa njia
ya maandishi. Unampataje/unamjuaje, ni
kwa kuuliza tu.Uliza jaji mfawidhi ni nani ,na omba kuonana naye kwa mujibu wa
utaratibu wa pale ulivyo au mwandikie.
( 4 ). Kama hukupata msaada katika 3 juu,
basi peleka malalamiko yako kwa Jaji mkuu. Jaji mkuu ni mtumishi mkuu wa
mahakama, na yupo kuhudumia, na kutatua kero za watu ikiwemo ya kwako. Huyu sio
mfalme ambaye hawezi kufikika, laa hasha. Ni mtumishi na anawatumikia watu kama
wewe. Isipokuwa sikushauri uende kwake kabla hujapitia ngazi hizi zilizoelezwa
hapa juu. Yeye apelekewe tatizo sugu
ambalo limeshindikana huku kote.
Jaji mkuu ni mmoja Tanzania nzima na ofisi yake kuu ipo
mahakama ya rufaa kivukoni, Dar es salaam.
Naye unaweza kumwandikia barua au ukaomba miadi ya ana kwa ana.
Wakati mwingine unaweza kuwa unacheleweshwa na watu wa chini
na hawa viongozi waliotajwa humu hawajui. Wafuate watakusaidia.
Yumkini, usiende kwa
rais,waziri mkuu,waziri yeyote ,mkuu wa mkoa, wa wilaya ama mkurugenzi nk. Hawa
katu hawawezi kukusaidia kwakuwa hawawezi kuingilia kazi inayoendelea
mahakamani. Usipoteze mda chukua hatua sahihi. Hakuna nje ya hawa anayeweza kukusaidia.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment