NA BASHIR YAKUB -
Nakala ya hukumu ya mahakama huhitajika pale kesi au shauri
linapokuwa limefika mwisho. Kwa lugha nyingine maamuzi ya mahakama ndiyo hukumu
ya mahakama. Hapa ndipo tunapojua nani ameshinda na nani ameshindwa. Nani
anastahili kulipwa au kukabidhiwa mali fulani na nani hastahili. Kadhalika nani
anastahili kufungwa na nani anastahili kuachiwa huru. Yote haya na mengine
mengi ndiyo yanayojenga kitu kinachoitwa
hukumu.
1.UMUHIMU WA NAKALA YA
HUKUMU.
Mara nyingi wale ambao hawakuridhishwa na maamuzi ya mahakama
kwenye hukumu hutaka kukata rufaa. Rufaa ni malalamiko yanayopelekwa mahakama
ya juu zaidi yakilalamikia hukumu au maamuzi yaliyotolewa na mahakama ya chini. Rufaa hufunguliwa na mtu
ambaye hakuridhika na kile kilichoamuliwa. Kwahiyo hata wewe kama unayo kesi
ambayo tayari imetolewa hukumu na hukuridhishwa
na kile kilichoamuliwa basi unayo haki ya msingi ya kukata rufaa.
Na huna haja ya kuhofu kama unazo sababu za msingi na za kisheria.
Waweza kuwa umeshindwa mahakama ya chini lakini ukaibuka mshindi mahakama ya
juu ambako umekata rufaa.
Hata hivyo, huwezi kukata rufaa bila kuwa na nakala ya
hukumu. Na hapa ndipo linapojitokeza suala la kupata nakala ya hukumu kwa
wakati na bila kucheleweshwa. Narudia huwezi kukata rufaa ikiwa hujapata nakala
ya hukumu kutoka mahakama iliyotoa uamuzi.
2. HASARA ZA KUCHELEWA
KUPATA NAKALA YA HUKUMU.
Ikiwa lengo lako ni kukata rufaa basi yafaa ujue kuwa rufaa
zote huwa zina muda wake. Zipo za siku 45,za siku 30 nk. Muda huo unahesabika
tokea siku hukumu iliposomwa. Ni ndani ya muda huo ambapo unatakiwa kukata
rufaa. Nje ya muda huo huruhusiwi na unakuwa umepoteza haki hiyo.
Sasa wakati mwingine muda huo waweza kuisha ukiwa bado unashughulikia
kupata nakala ya hukumu. Ni hapa
tunapotakiwa kujua la kufanya ili kuepuka kadhia na mazingira hatari kama haya.
3. KUCHELEWA KUPATA NAKALA YA HUKUMU.
Unaweza kuchelewa kupatiwa nakala ya hukumu kwasababu
mbalimbali. Moja ni kutokuomba kwako kupatiwa nakala ya hukumu. Kesi au shauri
linapoisha yafaa mara moja uombe kupatiwa nakala ya hukumu. Katika mada
nyingine nitaeleza utaratibu wa kuomba nakala ya hukumu. Kwahiyo kumbe waweza
kuchelewa kuipata kwasababu hukuiomba.
Pili, waweza kuchelewa kuipata kwasababu ya uwezo na ufanisi
wa mahakama husika. Nakala ni lazima iwe
imechapwa na imesahihishwa vizuri. Ukosefu wa vitendea kazi kama kompyuta
laweza kuwa tatizo la kuchelewa kupata hata kama uliiomba kwa wakati.
Tatu, uchache wa watumishi/makarani wachapaji ambapo huwa na
mizigo mingi na hivyo huchapa kazi moja moja kwa awamu jambo ambalo laweza
kukuchelewesha ukisubiri kazi yako ifikiwe.
Nne,uzembe wa wachapaji
na wakati mwingine huwa ni makusudi ili kujenga mazingira ya kupozwa(rushwa).
4. NINI UFANYE IWAPO NAKALA YA HUKUMU IMECHELEWESHWA.
Jambo la kwanza, kesi au shauri linapoisha hakikisha siku
hiyohiyo au inayofuata umeandika barua ya kuomba nakala ya hukumu. Hii
itakusaidia kwani hata ukichelewa kukata
rufaa ukapitwa na mda utasema mimi niliomba nakala mapema kwahiyo kuchelewa sio
makosa yangu.
Pili, ikiwa unaona makarani au wachapaji wanakuchelewesha
bila sababu au huelewi ni namna gani wanavyoshugulikia suala lako tafuta muda muone hakimu aliyetoa hukumu na
mpe maelezo yako na namna ambavyo hujapatiwa
nakala hiyo. Au waweza kumuona hakimu mfawidhi. Hakimu mfawidhi ndiye kiongozi
wa mahakama husika. Ukiuliza hakimu mfawidhi ni nani utaoneshwa na hapo utampatia
malalamiko yako. Hivi ndivyo unavyoweza kuepuka kupoteza haki hii.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment