NA BASHIR YAKUB -
Umiliki wa ardhi hutolewa kwa masharti maalum. Kila aliyepewa
hati miliki anajua kuwa amepata hati hiyo kwa masharti ambayo anapaswa
kuyatekeleza. Wapo ambao hudhani kuwa ukishapewa hati na masharti basi ni
hivyohivyo tu huna la kufanya hata kama hujaridhika au hunufahishwi na masharti
hayo.
Hii ni fikra isiyo sahihi na sasa wapaswa kujua kuwa masharti katika
hatimiliki ya ardhi yanaweza kubadilishwa kwa maombi maalum. Masharti ni kwa
ajili ya maendeleo na kwa ajili ya maendeleo waweza kuomba kubadilishiwa
masharti/sharti la umiliki.
1.NI MASHARTI YAPI
HUWEKWA KATIKA HATIMILIKI.
Yapo masharti mengi. Kifungu cha 34 cha Sheria Namba 4 ya ardhi kimeeleza masharti ya hati miliki. Baadhi ya
masharti hayo huwa ni pamoja na matumizi kwa mfano, utaambiwa unapewa hati ya
eneo hili ni kwa ajili ya biashara tu, viwanda tu, hoteli tu,makazi tu,
nk.
Au utaambiwa unapewa umiliki wa ardhi kwa miaka 33, 66, au
99. Au utapewa sharti kuhusu ujenzi, kwa mfano utaambiwa eneo hili huruhusiwi
kujenga jengo lisilo la ghorofa, au eneo linaruhusiwa kujengwa jengo la chini
tu, au pajengwe jengo lisilo la kudumu nk, nk.
Haya ni baadhi ya masharti unayoweza kupewa wakati unapokuwa
ukipewa hati miliki.
2. UTARATIBU WA KUOMBA
KUBADILISHIWA MASHARTI.
Ndio, unaruhusiwa kuomba kubadlishiwa masharti au sharti
kulingana na mahitaji yako. Unaweza
kuomba muda wowote baada ya kupewa umiliki au wakati mchakato wa kupatiwa umiliki
ukiendelea. Utaratibu wake ni huu;-
( i )Utatakiwa kujaza fomu namba 27 ambayo inaeleza matumizi ya sasa na yale
mapya unayoomba kubadilishiwa. Fomu hii inapatikana kwenye kanuni za Sheria
namba 4 ya ardhi, za mwaka 2011, pia zinapatikana ofisi za ardhi, na kwa
wanasheria.
( ii ) Fomu hiyo itaambatanishwa na nakala
ya hati husika, picha za muombaji, na ada ya maombi ya kubadilisha.
( iii ) Itakuwa imesainiwa na muombaji au wakili wake.
( iv ) Itaambatana na risiti za karibuni za
malipo ya kodi za ardhi au jengo.
( v ) Pia utaambatanisha taarifa nyingine
yoyote ambayo unaweza kuombwa kuwasilisha
na mamlaka za ardhi.
( vi ) Maombi hayo yatapelekwa kwa kamishna
wa ardhi kwani ndiye mwenye mamlaka na mchakato huu.
3. KUKUBALIWA
MABADILIKO YA MASHARTI.
Unaweza kukubaliwa maombi au kukataliwa au kubadilishwa kwa kile ulichoomba. Endapo utakubaliwa basi kamishna atakutaarifu kwa taarifa maalum
kupitia anuani na mawasiliano uliyotumia kwenye maombi. Atakutakata kuwasilisha
kwake hati miliki halisi ili aingize
mabadiliko mapya na kutia muhuri wake. Pia atakutaarifu mabadiliko mapya ya
malipo ya kodi na tozo za ardhi kutokana na matumizi mapya.
4. ADHABU YA KUKIUKA
MASHARTI.
Kifungu cha 45 cha Sheria namba 4 ya ardhi kimesema kuwa
ukiukwaji wa masharti ya umiliki wa ardhi
utapelekea hati ya mmiliki kufutwa.
Kufutiwa umiliki ardhi maana yake ni kunyanganywa ardhi. Kwahiyo ni muhimu kuendana na masharti haya
na panapo tatizo au hitaji la kubadili sharti kwa ajili ya maendeleo basi omba
ubadilishiwe kuliko kujibadilishia matumizi bila kufuata taratibu jambo ambalo
linaweza kugharimu ardhi yako yote.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment