NA BASHIR YAKUB -
Nakala ya hukumu ni haki yako ikiwa ulikuwa mhusika katika
kesi au shauri. Unakuwa mhusika katika kesi au shauri pale unapokuwa mshitaki
au mshitakiwa, mlalamikaji au
mlalamikiwa, au mhusika mwingine mwenye maslahi. Hapa ndipo unapohesabika kuwa mhusika katika
kesi au shauri na hapa ndipo unapokuwa na haki ya kuomba kupatiwa nakala ya hukumu.
Makala yaliyopita yalieleza kuwa nakala ya hukumu ni muhimu
hasa ukitaka kukata rufaa au kuchukua hatua zaidi , lakini pia ni muhimu kama
nyaraka ya kumbukumbu kwa ajili ya kesho, pia ni muhimu kwa ajili ya utekelezaji
wa kile kilichoamuliwa. Leo tuone mfano
halisi wa barua ya maombi ya nakala ya hukumu kama ulivyo hapa chini ;-
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, 24 / 5 / 2018
S.L.P..............................
Dar es salaam.
YAH ; MAOMBI YA KUPATIWA NAKALA YA
HUKUMU.
Nilikuwa mlalamikiwa katika shauri namba
13 la mwaka 2018, ambalo
limetolewa hukumu tarehe 22 / 3 / 2018, mbele ya Mhe. Kijana Mponela. Ninaomba
kupatiwa nakala ya hukumu kwa kumbukumbu
au hatua zaidi.
Wako
Mti Mkavu
( aliyekuwa mlalamikiwa ).
0717600900
Sahihi...............................
Barua itakuwa nyepesi na fupi hivyo. Na
inaweza kuwa imeandikwa kwa mkono au imechapwa. Lakini ni nzuri zaidi ikiwa imechapwa
kama uwezo upo.
Pia unaweza kutumia hii hii ila ukabadilisha
tu taarifa(copy&paste).Kwenye anuani imeandikwa kisutu lakini wewe utaweka
anuani ya mahakama iliyotoa hukumu yako na mkoa/wilaya ilipo, tarehe utaweka ya
kwako, kichwa kinaweza kubaki hivyohivyo, na kwenye maelezo utabadilisha
kutokana na taarifa za kesi/shauri lako. Mwisho utaweka jina lako,namba ya simu
pamoja na sahihi yako.
Kumbuka utakapoandika barua hii
hakikisha unatoa kopi na unakuwa na nakala mbili. Moja itabaki mahakamani na
moja utakwenda nayo ili wakugongee muhuri wenye tarehe wa kuthibitisha kwamba
wamepokea. Hiyo iliyogongwa muhuri urudi nayo kwa ajili ya kumbukumbu na hatua
za baadae.
Hiyo iliyogongwa muhuri ambayo umerudi
nayo ndiyo itakayokusaidia pale utakapokuwa umechelewa kukata rufaa na kupitwa
na muda. Na muda umekupita kwasababu ulikuwa
ukiisubiria mahakama kukamilisha kuchapa/kuandaa nakala yako ya hukumu. Basi hiyo
nakala iliyogongwa muhuri ni kwa ajili hii na ni muhimu sana tena sana kubaki nayo.
Barua ya kuomba nakala ya hukumu utaiwasilisha katika mahakama
ileile ambayo iliamua kesi au shauri lako.Gharama zake ni bure kwasasa kwa maelekezo ya jaji mkuu. Hakuna
malipo.
Maelezo mengine kuhusu nakala ya hukumu kwa ujumla,umuhimu wa
kuiomba na hasara za kutoiomba yalielezwa katika makala yaliyopita.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment