NA BASHIR YAKUB -
Ume;muuzia mtu kiwanja au nyumba. Mmeandika mkataba na
kuusaini tena mbele ya mwanasheria. Kwenye mkataba mmeweka vipengele vingi lakini kimojawapo kinahusu umaliziaji wa pesa
ya manunuzi. Hii ni kwasababu mnunuzi
amelipa kiasi kidogo na kiasi kingine ameahidi kwenye mkataba kukimalizia baada
ya muda fulani.
Mkataba umesainiwa na umekamilika. Mda umeenda na kufika ule
ambao mnunuzi alitakiwa kumalizia kiasi kilichobaki lakini bado haoneshi dalili za kumalizia kiasi
hicho. Umejaribu kumkumbusha mara kadhaa
lakini maneno yake ni yaleyale na pesa
halipi. Muda mlioahidiana sasa umepita
lakini bado mnunuzi hajamalizia hela
. Na pengine sasa hapokei hata simu au hujui aliko au anatoa majibu ya dharau au
yasiyoridhisha au vinginevyo.
Nini ufanye katika mazingira kama haya, zipi haki zako, ipi
hadhi ya mkataba wenu wa mauziano ambao uliusaini nk, nk. Tutaona hapa chini.
1.KUHUSU KUUZIANA NA
KUBAKI NA DENI.
Sheria haikatazi kuuziana ardhi na likabaki deni. Suala hilo
limeachwa katika hiari ya muuzaji na mnunuzi.Ni wao watakoamua kuhusu kulipa
hela yote au kulipa kiasi na kubaki na deni. Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba
kimesema mkataba ni halali ikiwa umefanywa
na wahusika timamu/kamili,huku wakiuziana kitu halali, na kwa masharti halali ya kisheria.
Basi madhali haya
yametimia jambo la kubaki na deni
halikatazwi kisheria.
2. KUSHINDWA KUMALIZIA
DENI.
Kushindwa kumalizia deni ndani ya muda ambao umeainishwa ndani ya mkataba kwa ufupi ni kuvunja
mkataba. Unapovunja sharti katika
mkataba ni umevunja mkataba. Basi kwa mazingira ya namna hii mnunuzi
anakuwa amevunja mkataba. Kifungu
cha 39
cha Sheria ya Mikataba kinasema kuwa
kushindwa kutekeleza yale yaliyokubaliwa katika mkataba ndio kufa kwa mkataba .
Kwahiyo ni vema mnunuzi ambaye hajamaliza ahadi yake ya
kimkataba kufahamu kuwa amevunja mkataba na hivyo ameua mkataba.
3. NINI UFANYE IKIWA PESA HAIJAMALIZIWA.
Ikiwa muda umepita na mnunuzi hajamalizia hela basi kifungu cha 73 cha sura ya 113 sheria Namba 4 ya ardhi kimekupatia majibu kuwa unaweza kufanya haya
;-
( a )Unaweza kurejea katika umiliki kwa amani bila
kupitia/kutumia mamlaka/taasisi yoyote( resume into possession peaceably).
Utakachotakiwa kufanya ni kumpa taarifa ya maandishi mnunuzi kuwa kwakuwa
ameshindwa kutekeleza ahadi iliyo kwenye mkataba basi narejea tena katika umiliki
wa shamba,kiwanja ,au nyumba yako.Na utarejea kweli.
( b ) Kurejea katika umiliki kwa kuitumia mahakama. Hapo juu
unarejea katika umiliki bila kuihusisha mahakama wakati hapa unaitumia mahakama
kurejea katika umiliki. Njia hii ya pili
unaweza kuitumia pengine kwakuwa mnunuzi ameshaanza kulitumia eneo na hivyo
ukaona ni vigumu kurejea katika umiliki bila nguvu ya sheria, au namna nyingine
ambayo unaona ni vigumu kuurejea umiliki kwa amani.
( c ) Unaweza kufungua shauri la madai ya hela ya kiasi
kilichobaki. Hapa unaamua kutorejea
katika umiliki lakini unachotaka ni kiasi kilichobaki tu umaliziwe na mambo
yaishe. Njia hii haipo kwenye sheria ya ardhi
bali sheria ya mikataba na katika madai ya kawaida.
( d ) Unaweza kumtafuta msuluhishi(mediator) kumaliza tofauti
zenu. Msuluhishi anaweza kuwa yule aliyetajwa katika mkataba wenu au yeyote
ambaye hakutajwa ambaye mtamridhia asuluhishe.Wakili, hakimu au jaji anaweza
kuwa msuluhishi mzuri kwa kumtumia kama mtu tu wa kawaida bila kutumia
utaratibu wa kawaida wa kufungua kesi.
( e ) Unaweza kusamehe deni kwa maandishi ikiwa utaona inafaa
kufanya hivyo. Haikatazwi kusamehe deni.
4. FIDIA.
Ikiwa utaamua kutumia njia yoyote hapo juu unaweza pia kudai fidia kama nyongeza ya hicho unachodai. Kifungu cha 73( 2) cha Sheria ya ardhi kimesema
hivyo. Fidia ni kwasababu huyu amevunja mkataba. Fidia ni nyongeza tu wala haipunguzi kile unachodai.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment