NA BASHIR YAKUB -
Yapo mambo tunatakiwa kuyazungumza mara kwa mara ili watu
wayaelewe. Moja ya mambo hayo ni hili la watu kudaiana hela hadi kufikishana polisi. Mtu binafsi,
Saccos au taasisi imekukopesha fedha, na hatimaye umeshindwa kulipa,
wanachokifanya ni kukupeleka polisi. Huko polisi ati unaandikishwa maelezo na wakati mwingine unatakiwa kusaini mkataba
mpya wa lini na namna gani utalipa deni.
Au wakati mwingine unawekwa ndani kabisa, au huwekwi
ndani ila siku ambayo umeambiwa kulipa ikifika hujalipa ati
askari anakupigia simu kukuuliza kwa nini hujalipa deni , na vitisho vya
kukukamata na kukuweka ndani, au wakati mwingine unakamatwa kabisa na kuwekwa
ndani.
Kwa ufupi haya yote ni makosa makubwa. Ni makosa kwa askari yeyote
ambaye ameamua kuchukua kesi ya aina hii, na ni makosa hata kwa yule anayedai
ambaye amekwenda kuripoti .
1.KUDAIANA HELA.
Masuala ya kudaiana hela ni masuala ya madai(civil). Polisi
hawahusiki kabisa na masuala ya madai. Polisi wanahusika na masuala ya jinai(criminal).
Kudai hela si masuala ya jinai hata kidogo. Masuala ya jinai wanayohusika nayo
polisi ni yale yote yaliyoorodheshwa katika Sheria ya Kanuni za adhabu, Sura
ya 16 ambayo ni kama kubaka,kuiba, kutukana, kulawiti,kupigana,
kuharibu mali , kujeruhi, rushwa, dawa za kulevya, uhaini, mauaji, kughushi, na
mengine yaliyo katika sheria nyingine mtambuka yanayofanana na hayo.
2. HATA KUWEKWA
CHINI YA ULINZI TU KWA MADAI YA HELA
HAIRUHUSIWI.
Kutoruhusiwa kwa polisi kujihusisha na masuala haya ya madai
ya kudaiana hela kumeelezwa kwa mapana. Si tu polisi hawaruhusiwi kukuweka
ndani kwa makosa kama haya bali pia hawaruhusiwi hata kukuweka chini ya ulinzi.
Kukuweka chini ya ulinzi ni kuzuia uhuru wako wa kutembea kwa namna yoyote ile,
hata kwa kukwambia hapo ulipo usitoke.
Katika kesi ya Rudolf v Athumani (1982) TLR 100 mahakama
ilisema kuwa ni kazi ya polisi pale
wanapoletewa mashtaka kuchambua ikiwa mashtaka
yaliyoletwa kwao ni madai au ni jinai
ili ikiwa ni jinai wayachukue na ikiwa ni madai waachane nayo na wamshauri
mleta mashtaka/malalamiko(informer) hatua sahihi za kuchukua.
Jaji Sammatta aliongeza kuwa polisi hawaruhusiwi kumweka mtu chini ya
ulinzi kwa makosa ya madai.
3. NINI UFANYE UKIFIKISHWA POLISI KWA MAKOSA
KAMA HAYA.
Ikiwa utafikishwa au kuitwa polisi kwa masuala ya kudaiana hela, waambie tu polisi kuwa haya
ni mashauri ya madai na nyie hamhusiki
na masuala ya madai kisheria. Lazima hili uwaambie wajue kuwa unalijua . Na usikubali kuingia makubaliano yoyote ya
kulipa/au kusaini labda uamue kwa hiari yako.
Kama utaona hawaelewi waambie wakupeleke mahakamani kwa kosa
hilo. Kwa uhakika hakuna wa kukupeleka mahakamani kwa kosa hilo. Labda
wakutafutie kosa jingine la kubambikiwa(maliciously) lakini si hili la madai ya
hela. Hakuna namna utafikishwa mahakamani na polisi kwa kosa hili, hakuna
namna.
Pili, ikiwa umewekwa chini ya ulinzi kwa makosa kama haya
basi unaruhusiwa kumfungulia shauri la madai ya fidia yule askari aliyekuweka
chini ya ulinzi pamoja na huyo mleta taarifa polisi/aliyeshitaki. Katika kesi ya Simon Chatanda v Abdul Kisomi
(1973),LRT,No 11 mahakama ilisema kuwa kumweka mtu chini ya ulinzi kwa
makosa ya madai ni makosa(wrongful confinement) na kuwa aliyewekwa chini ya
ulinzi anaweza kudai fidia kutoka kwa yeyote
aliyehusika akiwemo mtoa taarifa/aliyeshitaki.
Na tatu kwa wale mnaodai mnayo haki ya kufungua shauri la
madai mahakamani na sio kwenda polisi.
Ndio maana hujawahi kuona taasisi kubwa za fedha kama CRDB,NBC,NMB na nyingine
zikifungua kesi polisi kwa mtu wanayemdai aliyeshindwa kurejesha mkopo.
Hufungua madai mahakamani na sio polisi. Shida hii iko kwa watu binafsi
wanaokopesha, na taasisi ndogo ndogo za mikopo.
Hawa wanatakiwa kuacha hii tabia kwakuwa yule unayemdai anaweza
kukugeuzia kibao ukadaiwa fidia kubwa wewe na huyo askari wako unayemtumia.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment