NA BASHIR YAKUB -
Bubu yaani mtu asiyeweza kuongea anaweza kuwa shahidi mahakamani iwapo
ameshuhudia tukio. Kutokuwa na uwezo wa kuongea hakumwondolei sifa ya kushuhudisha
kile ambacho amekishuhudia. Ikumbukwe ushuhuda unatokana na na hatua ya mtu kuona, kusikia, kuhisi,
kugusa, au utambuzi wa tukio kwa namna
yoyote ambao umetokana na kiungo cha
mshuhudiaji.
Yumkini, bubu wengi hawasikii. Na tumeona hapo juu kuwa ushuhuda
ni pamoja na kusikia. Hata hivyo pamoja na kutosikia kwao bado wanavyo viungo
vingine vya mwili ambavyo wanaweza kuvitumia kushuhudia tukio. Viungo hivyo ni
pamoja na macho, mikono kugusa, ulimi kuhisi,akili katika utambuzi nk.
1. SHERIA KUHUSU BUBU SHAHIDI.
Kifungu cha 128( 1 )
cha Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 kinasema kuwa mtu ambaye hawezi kuongea(bubu) anaweza kutoa ushahidi wake
katika namna nyingine ambayo itaweza kuwa fanisi na ya kueleweka. Njia fanisi na ya kueleweka ni kama kupitia
maandishi/kuandika ikiwa anao uwezo wa kuandika, na kwa ishara ikiwa anao uwezo
wa kutumia ishara.
Wengi tunajua ishara kama njia kuu ya mawasiliano kwa bubu.
Basi hiyohiyo inaweza kutumika kwa bubu kutoa ushahidi.
2. HALI IKOJE KAMA HAKIMU/JAJI HAELEWI ISHARA YA BUBU.
Bubu anapotoa ushahidi wake kwa ishara panatakiwa pawepo mtu ambaye
atatafsiri ishara zile kwa maneno. Hata kamaHakimu/Jaji angekuwa na uwezo wa
kujua ishara za bubu bado mtu anayetafsiri anatakiwa kuwepo. Hii ni kwasababu
mahakamani hayupo hakimu tu. Bali wapo wapo wengine kama upande wa mashtaka ,
upande wa utetezi ambao wangependa kujua nini bubu anaongea katika ishara zake
ili wapate kumuhoji na kumuuliza maswali kuhusu kile alichoongea.
Hata hivyo mahakama ina hiari ya kupima kile ambacho
anafasiri mfasiri ili naye asije akapotosha
au kuingiza yake . Na kwa msingi huu ndio maana mahakama hailazimiki
kukubaliana au kubanwa na kile alichoongea/alichofasiri mfasiri.
Katika kesi ya HAMIS v REPUBLIC . 18 EACA. 217, dada wa bubu aliiambia mahakama kuwa yeye
anaelewa vizuri ishara za mdogo wake ambaye ni bubu na hivyo akasema atasaidia kutafsiri wakati mdogo wake
akitoa ushahidi.
Mahakama ilimruhusu atafsiri ushahidi wa mdogo wake. Lakini katika
hukumu mahakama ilisema kuwa imeukataa ushahidi wa bubu kwakuwa tafsiri iliyotolewa
dada yake ilikuwa haieleweki.
3. JARIBIO KABLA BUBU HAJATOA USHAHIDI.
Bubu hustahili kujaribiwa kabla ya kupokelewa ushahidi wake.
Jaribio hulenga kujua kama anajua alichokuja kufanya mahakamani na kama anao uwezo wa kujibu kile
anachoulizwa kwa usahihi. Jaribio hufanyika kwa kumuuliza maswali na kuona kama
anaweza kutoa majibu yanayoendana na maswali hayo(capability of giving rational
answers). Ikiwa ana uwezo huo basi
huchukuliwa kama shahidi kamili( competent witness).
Na kama hawezi kujibu sawa na kile anachoulizwa basi hawezi kuchukuliwa
kama shahidi kamili. Basi, hayo ni machache kuhusu bubu kuwa shahidi.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
Umetoa elimu nzuri lakini pia ni kusahihishe Kidogo mwanasheria msomi katika sheria za watu wenye ulemavu ziwe za kimataifa na kitaifa ni kosa kumuita mtu mwenye ulemavu jina la hilo tatizo lake hayo majina yamekuwa yenye kunyanyapaa mfano mtu asieweza kuongea kumuita bubu kama ulivyo ita juu ya title yako
Umetoa elimu nzuri lakini pia ni kusahihishe Kidogo mwanasheria msomi katika sheria za watu wenye ulemavu ziwe za kimataifa na kitaifa ni kosa kumuita mtu mwenye ulemavu jina la hilo tatizo lake hayo majina yamekuwa yenye kunyanyapaa mfano mtu asieweza kuongea kumuita bubu kama ulivyo ita juu ya title yako