NA BASHIR YAKUB-
Unaweza kuwa wewe, ndugu yako,rafiki au jamaa yako ameunganishwa katika kesi ya mauaji.
Aghalabu, daktari anasubiriwa kutoa ushahidi mahakamani kuhusu sababu za kifo
cha marehemu. Na ni ushahidi huo wa daktari utakaokuondoa katika kesi hiyo ya mauaji au utakuingiza katika kesi hiyo
na hivyo kutiwa hatiani na kuadhibiwa.
Lakini sio daktari tu bali wenye kesi wote ambao ushahidi
wake unahitaji mtaalam(expert) kuthibitisha mfano mkemia, mtaalam wa muandiko
na sahihi, mtaalam wa biashara , mtaalam wa DNA nk.
1.USHAHIDI WA DAKTARI.
Kifungu chac 47 cha Sheria ya Ushahidi kinaruhusu kutumika na
kukubalika kwa ushahidi wa mtaalam( expert). Mtaalam ni pamoja na daktari.
2. MAMBO 6 MUHIMU UNAYOTAKIWA KUJUA.
A ).
Kabla daktari au mtaalam mwingine yoyote hajaanza kutoa ushahidi wake ni
ni muhimu sana athibitishe kwa ushahidi kuwa yeye ni mtaalam kweli (expert) kwa
hicho anachotaka kutolea ushahidi. Usikubali akaanza kueleza kabla ya kuthibitisha utaalam.Mtake
athibitishe hilo kwanza.
Utaalam unathibitishwa kwa taaluma(professional). Kama ni
daktari na mtaalam wa eneo fulani la tiba ,mfano mifupa, moyo, nk, aoneshe
cheti cha taaluma katika eneo hilo. Halikadhalika kwa wataalam wengine nao wanatakiwa
kufanya hivyo. Kama hawezi kuthibitisha hilo basi hiyo ni faida kwako kwakuwa
ushahidi wake ni wa kutia shaka.
Na hapo haijalishi mtaalamu(expert) huyo ameletwa na nani.
Awe ameletwa na polisi, PCCB, au idara nyingine yoyote. Msimamo huu ulitolewa
na mahakama katika kesi ya MUHAMMED
AHMED V REPUBLIC(1957)E.A. C.A 523.
B ). Daktari au shahidi yoyote mtaalam,
asiwe tu mtaalam wa vyeti, bali awe mwenye ujuzi wa uzoefu wa kazi husika. Kwa
mfano, daktari au mtaalam ambaye amemaliza chuo, ana cheti lakini hajaajiriwa
wala kuwahi kuifanyia kazi taaluma yake popote hawezi kuitwa mtaalam mwenye
uwezo(competence) wa kutoa ushahidi wa kitaalam.
Hakikisha unahoji
uzoefu katika taalum husika(practice) . Kama hana sifa hiyo basi ni
faida kwako kwani ushahidi wake ni wa mashaka. Lakini ni baada yako kulihoji hili, ili liingie katika kumbukumbu za
mahakama. Huu ni msimamo wa mahakama katikas
kesi ya GATHERU s/o NJAGWARA v R(1954)E.A.C.A 384.
C ). Hata kama kinachotolewa ushahidi
kinajulikana kwa kila mtu, bado anayetakiwa kukitolea ushahidi ni mtaalam.
Kwa mfano katika kesi ya
SALUM HARUNA v R (1968)HCD 37, askari alitoa ushahidi kuwa
alichomkamata nacho mtuhumiwa ni bangi. Mahakama ya wilaya ilikubali ushahidi
huo na kumtia hatiani. Kwenye rufaa
mahakama ilibatilisha hatia hiyo na kusema kuwa , askari ambaye si
mtaalam wa madawa ya kulevya hawezi
kuijua bangi.
Hivyo hakikisha si tu shahidi anakijua kitu hicho, bali pia
ni mtaalam wake(expert). Kama si mtaalam hata kama anakijua kitu hicho bado
hakijua mbele ya sheria. Ndio maana utaona polisi wanasema “kitu chenye ncha
kali” “kitu kigumu” nk. Wanajua ni panga au jiwe lakini hawasemi kwakuwa si
wataalam (expert) wa kusema hivyo.
D ).Mtaalam asiseme kwa akili yake mwenyewe(personal
knowledge) bali aseme taaluma au sayansi
inavyosema kuhusu jambo husika. Kwa mfano asitumie maneno kama “mimi
ninavyojua”, “ nionavyo mimi”, “ushauri wangu”, “nafikiri”, bali aseme “
sayansi inasema hivi”, “ kitaalam jambo hili liko hivi” nk.Huu ni msimamo
katika kesi ya LONGINUS KOMBA v R (1973) LRT 39.
E ).Pia aeleze amefikiaje jibu
lake(conclusion). Ni kama ilivyo kwenye hesabu ambapo si tu unatakiwa kuonesha
jibu, bali njia uliyotumia kufikia hilo jibu. Lengo ni hiyo njia ihojiwe kuona
kama inaweza kuzaa jibu sahihi au laah.
F ). Mahakama hailazimiki kukubaliana na ushahidi wa mtaalam hata
kama jaji au hakimu sio mtaalam wa hicho kitu kilichotolewa ushahidi.
Kwa hakimu au jaji ushahidi wa mtaalam(expert) ni maoni tu na sio
hukumu.Ataamua kuyabeba au kuyatupa. Ni msimamo wa mahakama katika kesi ya HASSAN SALUM v R (1964) E.A 126.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI
KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment