NA BASHIR YAKUB -
Inaweza kuwa nyaraka
muhimu kama hati ya nyumba, mkataba wa mauziano au mkataba mwingine
wowote, wosia, kadi ya gari au ya mashine yoyote,hati ya kusimamia mirathi,
cheti cha ndoa au vyeti vinginevyo, na nyaraka nyingine mbalimbali.
Nyaraka hii inaweza
kuwa inatakiwa sehemu muhimu kama mahakamani ili kuthibitisha shauri au kesi yako. Na
inaweza ikawa ni nyaraka ambayo kuwepo kwake ndio kushinda kwako na kutokuwepo
kwake ndio kushindwa kwako.
Pamoja na umuhimu wa nyaraka hii bado umeitafuta kote pa
kutafuta na hukuweza kuipata. Au hukuitafuta madhali tu unajua ilishapotea au
iko mikononi mwa mtu ambaye hujui alipo na hawezi kupatikana. Katika mazingira
ya namna hiyo makala yataeleza vitu vichache vinavyoweza kusaidia kutoka Sura
ya sita,Sheria ya Ushahidi.
1. USHAHIDI WAKO.
Kitu kikubwa
kinachomsaidia mtu kushinda kesi mahakamani ni ushahidi. Kadhalika
kushindwa kwako pia ni ushahidi. Ukisema hiki kiwanja au nyumba ni yangu unatakiwa kuonesha hati au
mkataba wa mauziano au vyote viwili. Ukisema hili gari ni langu kadhalika
uoneshe kadi yenye jina lako ama vinginevyo. Ukisema nilikuwa na ndoa halali
uoneshe cheti cha ndoa ama vinginevyo. Ukisema nilimuuzia au kununua kitu fulani
uoneshe mkataba ama risiti,vivyo hivyo nk, nk.
Hakimu au Jaji si mtu ambaye anakuwa eneo la tukio na hivyo
kuwa katika nafasi ya kujua nini kilitokea huko. Yeye hajui chochote
kilichotokea na hivyo taarifa zote anazipata kwenu mnaoshitakiana. Kwa msingi
huu yupo katika wakati mgumu kuamua nani yuko sahihi na nani hayuko sahihi kwa
kitu ambacho hakushuhudia na hakijui.
Kama hivi ndivyo kitu pekee cha kumuongoza hakimu/jaji huyu
ambaye hakuwepo wakati mnadhulumiana, ni ushahidi wa kila mmoja atakaowasilisha.
Hataangalia suraya mtu, kulia machozi kwa mtu, kuongea kwa kujiamini au kwa
unyonge kwa mtu, umri wa mtu, rangi ya mtu,wala jinsia, bali ushahidi ulio
uliowasilishwa na mtu.
2. MAMBO MAWILI
YANAYOWEZA KUKUSAIDIA IKIWA UMEPOTEZA NYARAKA.
Jambo la kwanza,
lipo kifungu cha65 ( a ) ,( b ) na ( c ) cha Sheria ya Ushahidi. Ni
uwepo wa nakala(kopi) ya nyaraka halisi(orijino). Kama umepoteza orijino lakini
ipo kopi au unajua sehemu ambayo unaweza kupata kopi basi inaweza kukusaidia.
Ndio maana ni muhimu kuwa na kopi ya kila nyaraka ambayo una
orijino yake. Kifungu cha 63 cha Sheria ya Ushahidi kinasema kuwa nakala isiyo
halisi/kopi inaweza kutumika kuthibitisha jambo. Lakini pia vitu vingine vinaweza kuhitajika
kuthibitisha kupotelewa na nakala halisi kwa mfano taarifa ya polisi ya
kupotelewa nk.
Jambo la pili, linaloweza kukusaidia lipo kifungu
cha 65( e ) cha Sheria hiyohiyo ya Ushahidi. Ni kumleta shahidi ambaye
anakumbuka na kujua kile kilichokuwa kimo/kimeandikwa katika nyaraka hiyo
ambayo haionekani.
Anaweza kuwa mtu aliyeiandaa, aliyeishuhudia,aliyeisoma, au
yeyote ambaye kwa uhakika alijua nini kilichokuwa kimeandikwa ndani mwake. Kazi
yake itakuwa ni kueleza nini kilikuwa kimo/kimeandikwa humo na atahojiwa na
kuulizwa kuhusu hicho alichosema. Hili nalo laweza kusaidia.
Na kama hivi vyote havipo, basi kuthibitisha kwaweza kukuwa vigumu kidogo na
hivyo kujikuta unapoteza hata kama haki ni yako.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment