Monday 5 March 2018

NAMNA YA KUOMBA HATIMILIKI YA ARDHI YA KIMILA.

Image result for ARDHI KIJIJINI

NA BASHIR YAKUB -

1.     HATIMILIKI  YA KIMILA NI IPI.

Hati  ya  ardhi  ya kimila ni nyaraka  ya  umiliki  wa  ardhi ambayo  inatoa  utambuzi  maalum wa umiliki wa ardhi. Hizi ni sawa  na  hati  miliki  zile mnazozijua  ambazo  hutolewa kwa ardhi za mijini japo ipo tofauti kidogo. 

Moja ya tofauti  ya  hati  ya  kimila  na  hatimiliki za mijini  ni  kuwa  hizi  husimamia  ardhi  mijini wakati  hizi  nyingine husimamia ardhi za vijijini.

2.      HATI YA KIMILA HUTOLEWA NA NANI.    

Hati  ya  umiliki wa  ardhi  ya  kimila  hutolewa  na baraza la ardhi la kijiji( land village council). Kila kijiji  kinalo  baraza  hili. Pia  baraza hili  ndilo linalowajibika  kwa masuala ya kila siku ya ardhi ya kijiji. Kwa hiyo maombi  yote ya kuomba ardhi au hati ya kimila  yataelekezwa baraza hili.

3.    FAIDA ZA HATI YA KIMILA.

( a ) Unaweza kukopea kwenye taasisi ya fedha.
( b ) Inaweza kutumika kama dhamana mahakamani.
( c ) Ardhi  yako inakuwa  imerasimishwa na hivyo thamani yake kupanda, nk.

4.   NI SIFA ZIPI HUHITAJIKA ILI KUPATA HATI YA KIMILA.

( a ) Awe mtu aliyefikisha au zaidi ya Miaka 18.
( b ) Awe Mtanzania.
( c )Iwe kikundi,kampuni au familia.

5.     NAMNA YA KUOMBA HATI YA KIMILA.

( a )Andaa  maombi maalum na kuyaelekeza kwa baraza la ardhi la kijiji.

( b ) Maombi hayo yawe katika fomu maalum ambazo hupatikana kwenye serikali za vijiji.

( c ) Kama mwombaji ni familia,kikundi au kampuni ambayo ni ya wakazi wa  hapo kijijini basi wanahitajika watu wawili watakaosimama kama waombaji na watia saini.

( d ) Kama waombaji ni familia au kikundi ambacho waombaji wake sio wakaazi wa kijiji husika basi wadhaminiwe na wakaazi wa kijiji husika wasiopungua watano.

( e )Maombi hayo juu yaambatane na ;
-Kiapo kinachoeleza iwapo mwombaji anamiliki ardhi nyingine popote Tanzania  au hapana.
-Nyaraka nyingine  yoyote ambayo baraza la  kijiji litaomba kuwasilishwa.
-Kulipa ada iliyowekwa na baraza la ardhi la kijiji.
-Kwa waombaji ambao sio wakaazi  waambatanishe maelezo yaliyosainiwa na mashahidi kuwa wataendeleza ardhi husika  ndani ya miezi mitatu tokea kupewa kwao.

( f ) Baada ya  yote  hayo  juu basi  wasilisha  maombi  hayo baraza la ardhi la kijiji  na subiri au fuatilia ili upate hatimiliki ya kimila.
Makala yamefanunuliwa kutoka baadhi ya vifungu ndani ya Sheria Namba 5, Sheria ya Ardhi za Vijiji  ya 1999.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment