Tuesday 13 February 2018

UNACHOSTAHILI BAADA YA KUACHISHWA/KUFUKUZWA KAZI KIMAKOSA.


Image result for WAFANYAKAZI
NA  BASHIR  YAKUB -

1.  NINI MAANA  YA  KUACHISHWA  KAZI  KIMAKOSA. 

Katika  ujumla  wake  kuachishwa  au  kufukuzwa  kazi  kimakosa ni  hatua  ambapo  mwajiri  anamwachisha  au  anamfukuza  kazi  mwajiriwa  wake  bila  kufuata  utaratibu  wa  sheria.  Mwajiri  asipofuata  sheria  katika  kumuondoa  mwajiriwa  kazini  ndipo  anapokuwa  amemiwachisha  kazi  kimakosa.

Na  hapa  haiongelewi  Sheria  ya  ajira  na  mahusano  kazini  tu  inayotakiwa kuzingatiwa, bali  sheria  zote  ambazo  huhusika katika  ajira na mikataba  ikiwemo  sheria ya  mikataba  na  nyinginezo. Sheria yoyote   haipaswi  kuvunjwa  au  kukiukwa  wakati  mwajiriwa  anapotakiwa  kuachishwa  kazi.

2.   AINA  MBILI  ZA  KUACHISHWA  KAZI  KIMAKOSA.
Kuachishwa  kazi  kimakosa  kumegawanyika  mara  mbili ;

( a ) KUACHISHWA KWA KOSA AMBALO HALIPO(WRONGFUL TERMINATION).

Hii  ni  pale  ambapo  mwajiri  anamtuhumu  mwajiriwa  kwa  kosa  ambalo  hajatenda  kabisa.  Anamtungia  kosa  ili  amuondoe  kazini  kwasababu   anazojua  mwenyewe.  Au  inakuwa  ni  kweli  mwajiriwa  ametenda  kosa  lakini kosa  lile  halina  hadhi  au  uzito  wa  kumwondoa   kazini.  Sio  kila  kosa  ni  la  kumwondoa  mtu  kazini.  Makosa  mengine  ni  ya  kuonya  au  kuelekeza  tu.

Kwahiyo  haya yakitokea  ndipo  tunaposema  kuwa mwajiriwa  ameachishwa  kazi   kimakosa.  Kimakosa  kwa  maana  kwa  kosa  ambalo  halipo  au  lipo  lakini  halitoshi  kumuachisha  mtu  kazi( not  justifiable).

( b ) KUACHISHWA KAZI KWA KOSA  AMBALO LIPO  LAKINI  BILA  KUFUATA UTARATIBU(UNFAIR TERMINATION).

Hapa  kosa  linakuwa  ni  kweli  kabisa  limetendwa.  Na  uzito  wa  kosa  lenyewe  unatosha  kabisa  kumuachisha mwajiriwa  kazi.  Tatizo  linakuja  kuwa  wakati  wa  kumuachisha  kazi  kwa  kosa  hilo  utaratibu  unakiukwa.  Kosa  sawa  lipo, lakini utaratibu  wa  kutumia  kosa  hilo kumwondoa  mtu  ndio  uliokiukwa.

Utaratibu  ni  kama  kutopewa  taarifa(notice) , au kupewa  taarifa  lakini  katika  muda  usiostahili, kutolipwa  stahili, kutopewa  nafasi  ya  kusikilizwa, nk.  Kwahiyo utaona  tofauti  ya aina  hizi  mbili  za  kuachishwa  kazi  kimakosa.

Hata hivyo, pamoja  na  utofauti  huu bado  unachostahili  baada  ya  kuachishwa  kazi  kimakosa  ni  kilekile.  Aliyeachishwa  kwa  kosa  ambalo  halipo  na  aliyeachishwa kwa  kosa  ambalo  lipo  lakini  kwa  kukiuka  utaratibu  wote  hustahili  stahili  sawa  kama  tutakavyoona hapa.

3.   UNACHOSTAHLI  BAADA  YA KUFUKUZWA KAZI KIMAKOSA.
Inapothibitika  kuwa mwajiriwa  aliachishwa  kazi  kimakosa  mambo  yafuatayo  yanatakiwa  kufanyika ;

( a ) Kumrejesha  mwajiriwa  kazini .

( b ) Kulipa  mishahara  yake  yote  katika  muda  wote ambao  hakuwa  kazini.

( c ) Kumlipa  posho  zake  zote, na  malipo  mengine  ambayo  yapo kimkataba  ambayo  angelipwa  kama  angekuwa  kazini.

( d ) Kumlipa  mwajiriwa  fidia kwa  kumwachisha  kazi  kimakosa  kwa  kiwango  cha mishahara  isiyopungua  miezi 12.

( e ) Kutekeleza masharti  mengine yaliyoamrishwa  na  mahakama  ikiwa  mgogoro  ulifika  mahakamani, au mliyokubaliana ikiwa mlifanya makubaliano. Pia mahakama  inaweza  kuongeza  kiwango  cha  malipo  kwa  namna  itakavyoona  inafaa.
Stahili  hizi  zote  unaweza  kulipwa  kwa  kuelewana  na  mwajiri  ikiwa  mtaelewana  au  kulipwa  kutokana  na  amri  ya  mahakama ikiwa  mtakuwa  mmefika  huko.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment