Tuesday 6 February 2018

UTARATIBU WA SHERIA UNAPOHAMISHA OFISI ZA KAMPUNI.

Image result for COMPANY

NA  BASHIR  YAKUB -

Vijana  wengi  wamefungua  makampuni. Mengine  tayari  yanafanya  kazi  na  mengine  hayafanyi  kazi. Kutokana  na  sababu  mbalimbali  vijana  wamekuwa  wakihamisha  ofisi  za kampuni  zao. Wengine  sababu  za  kodi  ya  pango, wengine  kutafuta  maeneo  mazuri  zaidi  ya  biashara, na  sababu  nyingine  nyingi.Natumia neno vijana kwakuwa ndio wengi japo hili ni kwa kila mwenye kampuni.

Hata  hivyo  wengi  wao  wamekuwa  wakihamisha  ofisi  zao  kiholela. Kwa  maana  wanahamisha  kwa  utashi  wao  bila kuzingatia  kuwa  kuna  utaratibu  wa kisheria  unaotakiwa kufuatwa.  Niseme  tu  kuwa  unapokuwa  umefungua  kampuni  tayari  tafsiri  yake  ni  kuwa  upo  katika  mfumo  rasmi.  Mfumo  rasmi  maana  yake  biashara  zako zinalindwa  na  sheria  halikadhaliki biashara  hizohizo  zinawajibika  chini ya  sheria.

Lolote  utakalofanya  yafaa  ujue  sheria  inasemaje  kuhusu  hilo  ili usije  kuingia  katika  makosa au usije  ukajikosesha haki  zako. Niseme tu  kuwa  Sheria  Namba 12 , Sheria ya Makampuni imelifanya  kosa  tendo  la  kuhamisha  ofisi  bila kufuata  utaratibu  wa  kisheria  kama  tutakavyoona  hapa.

1.      OFISI  ZA  KAMPUNI  NI  ZIPI ?.

Mtakumbkua  kuwa  unapokuwa  unasajili  kampuni kuna  pahala huwa  unatakiwa  kujaza/kueleza  ni  wapi itakuwa  ofisi  za  kampuni  yako. Kipo  kifungu  cha  pili  katika  kila  katiba  ya  kampuni  ambacho  huwa  kinahitaji  kueleza  makao  makuu  ya  ofisi  za  kampuni (head office).

Lakini  pia  ipo  sehemu  unapokuwa  unajaza  fomu  namba 14(a)  huwa  inakutaka  kueleza  wapi  zitakuwa  ofisi  za  kampuni yako. Hapa  huwa  unatakiwa  kueleza  kinagaubaga. Hapa maelezo  ya  wapi  zitakuwa  ofisi  za kampuni huwa yanatakiwa yajitosheleze  kiasi  kwamba  mtu  akisoma  aweze  kufika  ofisi  ilipo  bila  hata  kuuliza.

Isiwe  tu ,P.O.BOX 200 DAR ES  SALAAM  bali  mtaa, kitongoji, kata, hata  nyumba  namba kama  ipo au  namba  ya  mlango na ghorofa  nk nk.  Hii  ndio huitwa  anuani  kamili  ya  ofisi  za  kampuni na  hizo  ndizo  ofisi  za  kampuni. Ni  kosa  kukutwa  umeweka  ofisi eneo  tofauti na  lile  lilioandikwa  kwenye  nyaraka. Vinginevyo  ofisi  ziwe  zimebadilishwa  tena kwa  utaratibu  huu  hapa  chini.

2.       UTARATIBU   UNAPOBADILISHA  OFISI.

Hatua  ya kwanza  ni  kuitisha  mkutano  wa  wanahisa(extraordiunary meeting)   ili  kukubaliana  kuhusu kuhamishwa  ofisi  za kampuni.

Hatua  ya  pili  katika  mkutano  huo mta pitisha maamuzi rasmi ya kampuni (company resolution)  kuwa wanahisa  mmekubaliana  kuhamisha ofisi  za kampuni. Nyaraka  maalum  ya maamuzi  rasmi ya  kampuni(company resolution)  itaandaliwa  na  kusainiwa.

Hatua  ya  tatu, mtajaza  fomu  maalum fomu  namba  111  inayoeleza  kuhama  kwa  ofisi  za  kampuni  na  wapi  zilipo  ofisi  mpya.  Fomu  hizi  mtazipata  kwenye  kanuni za  sheria  ya  makampuni za mwaka 2005  au  kwenye mtandao(website) wa BRELA.

Hatua  ya  nne, chukua  hiyo  nyaraka  ya  maamuzi  rasmi ya kampuni( company resolution) pamoja  na  hiyo  fomu namba  111 mliyojaza  ambatanisha  kwa  pamoja  kisha  peleka  BRELA kwa  taarifa na usajili wa  ofisi  mpya.

Hatua  ya  tano  baada ya  usajili  sasa  unaweza  kuhamisha  ofisi  za  kampuni  yako.
Nirudie  tena  kuwa  ni  makosa  kuhamisha  ofisi  za  kampuni  bila  kufuata  utaratibu  huu. Usiseme  kampuni  yangu  sijui  ni  ndogo, sijui  nini. Kampuni  ni  kampuni, ikishaitwa   kampuni hiyo ni kampuni tu ndugu, na ni  lazima kufuata  utaratibu  huu. 

Ni  muhimu  kusisitiza  hilo  kwakuwa  vijana  wengi  wajasiriamali  wenye  kampuni  ndogondogo  wamekuwa  wakihamamishahamisha  ofisi  wanavyotaka  wao  na hivyo  kuingia  katika  makosa  bila  kujua.
Fuata taratibu usisubiri kulalamika unaonewa na serikali.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com




0 comments:

Post a Comment