Thursday, 25 January 2018

JE MNAJUA NI KOSA KWA WATU BINAFSI KUKOPESHANA KWA RIBA ?.

Image result for MKOPO

NA  BASHIR  YAKUB -

Ni  muhimu  sana kwenu  kulijua  hili.  Anakuja  mtu anaomba  umkopeshe  hela. Unamkubalia  lakini  kwa  sharti  la  riba  ya  kiasi  fulani.  Au mkopaji  mwenyewe  anakushawisi  kuwa  ukimpa  atarejesha  kwa  riba. Vyovyote  itakavyokuwa suala  la  msingi  ni  kuwa  katika  makubaliano  yenu mmeweka  riba.  Basi  jambo  hili  ni  kinyume  cha  sheria  na  halikubaliki.

Ikiwa  uliyemkopa  atakataa  kukulipa  hela  yako basi  utakuwa  huna  la  kufanya.  Hata  ukienda  mahakamani bado mahakama  haiwezi  kukusaidia.  Haiwezi  kuamuru  ulipwe  hiyo  hela.  Utakuwa  umepoteza.  Na  si tu utapoteza   hizo  za riba  bali  pia hata  hizo  ulizomkopa(principal sum). Usimkopeshe  mtu kwa riba kwani   akiamua  asikulipe huna  la  kumfanya  kwa  mujibu  wa  sheria. 

Wengine  hukimbilia polisi kulalamika. Yumkini ni  makosa. Na huyo  askari anayeshughulikia  kesi  kama  hii  yupo  katika  makosa. Si  kazi  ya  polisi  kushughulikia masuala  kama  haya.  Yafaa  tuyajue  haya  ili  tuwe  makini.

Mahakama  kuu na  ya  rufaa zimeamua hivyo  katika  kesi  nyingi . Mojawapo  ni  Shauri  Namba  66/2007  kati  ya ULF NILSON dhidi  ya   DR. TITO  MZIRAY ANDREW . Katika  shauri  hili  Jaji A.F.NGWALA  alisema  kwamba  hata  kama  kuna  makubaliano  ya  maandishi   kuhusu  malipo  ya  riba bado  mtu  binafsi ambaye  hakusajiliwa  wala  hana  leseni  ya  kufanya  biashara  ya  fedha  hawezi  kutoza  riba.  Mwishoni  alibatilisha  makubaliano  yote  ya  huo  mkopo.

Kubatilishwa kwa  makubaliano  yote  ya  huo  mkopo maana yake  hata zile  fedha ulizomkopa  ambazo  sio  riba  nazo  zinakufa  kwasababu  mkataba  mzima  umebatilishwa, na  mahakama  imeuazimia(declare) kuwa  haramu. Unaweza  kuona  utakuwa  umepoteza  kiasi  gani.
Na hali  ni  hii  hii  hata  kwa  kampuni  ambazo  hufanya  biashara hizi  bila leseni ya  biashara  ya  fedha.

1.    KUHUSU  REHANI   YOYOTE  KAMA  IMEWEKWA.

Yawezekana  wakati  unamkopa  aliweka  mali  yoyote  rehani. Iwe baiskeli, pikipiki,gari, nyumba, kiwanja  au  kinginecho madhali tu  ni  rehani.  Hii  nayo  ni  haramu na  imekatazwa  na  sheria.  Kifungu  cha 6( 1 ) cha  Sheria  ya Mabenki  na Taasisi  za Fedha  kinasema  kuwa   mtu  yeyote ambaye hafanyi  biashara  ya  benki/fedha  na  hana  leseni ya biashara hiyo haruhusiwi  kupokea  rehani kwa  ajili  ya  mkopo  kutoka  kwa  mtu  yeyote.

Kifungu  kidogo  cha ( 2 ) kimetangaza  adhabu  ya  faini  isiyozidi  milioni 20, kifungo  kisichozidi  miaka  mitano, au  vyote kwa  pamoja  yaani  kifungo  pamoja  faini.  Kumbe  basi  utaona  kuwa  sio  tu  hairuhusiwi  bali  pia  waweza  kwenda  jela. Kwa  hiyo ni  vyote  kutoza  riba  pamoja  na kuomba/kupokea   rehani ni  makosa.

2.     KINACHOWACHANGANYA  WATU.      

Kuna maneno  mtaani  kuwa  mkataba  ni  mkataba na  makubaliano  ni  makubaliano  ilimradi  tu  wahusika  wote  wameridhia na  wameandikishana  na  kusaini  kwa hiari  zao.  
Mtu  anategemea kumwambia mwenzake si  ulisaini  hapa. Ulisaini ukitegemea nini, na maneno mengine kama  hayo. Ndugu, maneno hayo  hayana msaada kwako, unapoteza tu mda.

Kifungu  cha 10 cha  Sheria  ya Mikataba  kinasema  kuwa  makubaliano  yote  ni  mikataba  kama yamefanyika  kwa  hiari, na  wahusika  wenye  sifa,   kwa  biashara  halali, na makubaliano hayo yasiwe yamekatazwa  na sheria nyingine yoyote.  
Utaona kifungu  kinasisitiza  kuwa  hata kama  makubaliano  yatakuwa  kama  kifungu  kilivyosema  lakini  bado  makubaliano hayo  yasiwe yamekatazwa  na  sheria  nyingine  yoyote .

Kwahiyo  ni  kweli  kabisa  kuwa  makubaliano  ni makubaliano  isipokuwa yanakuwa makubaliano kamili na halali kama  hayajatangazwa  na  sheria  nyingine  kuwa  haramu. Na  makubaliano  ya  riba  na  rehani  kwa  ambao  sio  taasisi  ya  fedha  na wasio  na  leseni   yametangazwa  na  sheria nyingine  ambayo  ni  Sheria  ya  

Mabenki  na Taasisi  za  Fedha kuwa haramu.  Kwa  msingi  huu  ile  dhana  ya  makubaliano  ni  makubaliano tuliyoizoea mtaani  inakufa na haipo tena . Hivyo  usiifikirie  tena katika  mawazo na utetezi/kinga  yako.Haitakusaidia .

3.   KUHUSU  KUSAIDIANA  HELA  KAMA  WANADAMU.      

Sheria haikatazi kusaidiana hela kwa kuandikishana. Hela  mnaweza  kusidiana  kwa  kukopana. Lakini  iwe  tu  kiubinadamu(socially)  bila  ya  riba  wala  rehani(commercially).  Msaada  uwe  msaada  na  isiwe   katika  mfumo  wa  faida, mapato  au  biashara.  Na  hapa  mnaweza kuandikishana  na  mahakama  ikasaidia  kupatikana  haki  ikiwa  mkopwaji  amekaidi  malipo.
Kwahiyo  ndugu  jihadhari. Jihadhari  hasa  wewe  mtoa  mkopo.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment