Monday, 8 January 2018

UTARATIBU WA KUSAJILI CHAMA CHA SIASA HUU HAPA.

Image result for CHAMA CHA SIASA

NA  BASHIR  YAKUB -

Haki ya  kusajili  na  kuwa  na  chama  cha  siasa  ipo  kwa kila  mtanzania.  Hata  wewe  unaweza  kuwa  na  chama  cha  siasa  ikiwa  utataka  kufanya  hivyo.  Wako  wanaofikiri  kusajili  chama  siasa  ni  jambo  kubwa  mno. Laa  hasha  ni  jambo  la  kawaida    na  utaratibu  wa  usajili  si  mgumu  kama  wengi  wanavyodhani.

Tutaona  hapa  utaratibu  wa  kusajili  chama  cha  siasa.  Sheria  namba  5 ya  1992  Sheria ya  Vyama  vya  Siasa  na  kanuni  zake  za  mwaka  1992 ndizo  zinazoeleza  utaratibu utakaoelezwa  hapa  chini.

USAJILI  HUPITIA  HATUA  KUU  MBILI.

Kwa  mujibu  wa  kifungu  cha8( 1 ) cha  sheria  ya  vyama  vya  siasa  usajili  hupitia  katika  hatua  kuu  mbili.
Kwanza  usajili  wa  muda  na  pili  usajili  wa  kudumu.  Kwahiyo  ili  usajili  chama  cha  siasa  yakupasa  kupitia  hatua  hizi  mbili.

1.      USAJILI  WA  MUDA(PROVISIONAL REGISTRATION).        

Usajili  wa  muda  umeelezwa  katika kifungu  cha  9  cha  sheria  hiyo.  Usajili  wa  muda  maana  yake  chama  kitasajiliwa   na  kitaruhusiwa  kufanya  baadhi  ya  kazi  ila  usajili  huo  utakuwa  haujakamilika  mpaka  baada  ya  kutimiza  masharti, sifa  na  viwango  vilivyowekwa  na  sheria   ndani  ya  muda  maalum  ulioainishwa na sheria.  Usajili wa muda ndio  unaoanza  na  utaratibu  wake  ni huu ;

( a ) Andaa  katiba  ya  chama na  hakikisha  unakuwa  nayo. Mnajua  kila  chama  cha  siasa  huwa  na  katiba  yake, basi  hiyo  ndiyo  inayotakiwa hapa.

( b ) Hakikisha  mko  waanzilishi  wasiopungua  wawili.

( c ) Andaa  kanuni  za  chama. Kanuni  na  katiba  ni  tofauti. Kanuni  ndizo  zinazotafsiri  katiba kwahiyo  kanuni  hutokana  na  katiba.

( d ) Mtajaza  fomu  ya  maombi iitwayo PP 1. Inapatikana  kwa  msajili  na  pia ipo sehemu ya kwanza ya  kanuni  za vyama  vya  siasa  za 1992, waweza kutoa kopi.

( e ) Waanzilishi  watajaza  fomu maalum iitwayo PP 2 ambayo  ni  kama  kiapo(declaration).

( f ) Baada  ya  hapo  hivyo  vyote  vilivyoandaliwa  vitapelekwa  kwa msajili  wa vyama  vya  siasa  kwa  uhakiki. Baada  ya  uhakiki  na  kukidhi  sifa   mtatakiwa  kulipa ada kwa  maelekezo  ya  msajili  na  hapo  usajili  wa  muda  utakuwa  umekamilika.

( g ) Mtapewa  cheti  cha  usajili  wa  muda.

2.    USAJILI  WA   KUDUMU( FULL REGISTRATION).
Kifungu  cha  10 cha  Sheria ya  vyama  vya  siasa  ndicho  kinachoeleza  hili.

( a ) Usajili  hapa unatakiwa  ufanyike  ndani  ya  siku  180 tokea  kupata  cheti  cha  usajili  wa  muda.

( b ) Lazima  kuwe  na  cheti  cha  usajili  wa  muda.

( c ) Lazima  mpate  wanachama  wasiopungua 200 ambao  wana  sifa  za  mpiga  kura. Hawa  watatakiwa  kutoka  ndani  ya  mikoa  isiyopungua  10 ya Tanzania , ambapo  mikoa  isiyopungua  2 kati  ya  hiyo  10  iwe  ya  Zanzibar, na  katika  hiyo  2 ya  Zanzibar mkoa  mmoja  uwe  wa Unguja  na  mwingine  Pemba.

( d ) Mtajaza  fomu  nyingine  ya  maombi  iitwayo  PP 3

( e ) Pia  wanachama 2 waanzilishi  watajaza  fomu  maalum  iitwayo  PP 4.

( f ) Taarifa  zote  hapo  juu  zitapelekwa kwa  msajili,  na  huko  mtalipa  ada  kwa maelekezo  yake  ikiwa mmekamilisha  mahitaji.

( g ) Mtapewa  cheti  cha  usajili  wa  kudumu na mtaanza  rasmi  kazi  za siasa kupitia  chama.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment