Thursday 4 January 2018

JIIHADHARI, HAYA NDIYO HUITWA UCHOCHEZI.



NA  BASHIR  YAKUB -

Kama  hujajua ni kuwa  ni rahisi  sana  kuunganishwa  kwenye  makosa  ya  uchochezi. Sheria  mpya  ya Huduma  za Habari  ya mwaka 2016  imelipanua  sana  kosa  hili. Tafsiri na dhana  nzima   ya  uchochezi katika  vifungu vya 52 na 53 katika  sheria  hiyo   ni  tofauti  kabisa na  ilivyokuwa  katika  kifungu  cha  55  cha Kanuni  za adhabu na  kwenye sheria  ya  magazeti  ya  mwaka 1976.

Kuna  umuhimu  mkubwa  wa  kujua jambo  hili hasa  kipindi  hiki  ili  usijekujikuta  matatani.
Angalizo  ni  kuwa  sheria  hii  mpya ya  habari  haiwahusu  tu waandishi  wa  habari  bali  kila  mtu.

1.KWASASA  UCHOCHEZI  NI NINI.

Kifungu  cha 53 cha sheria  hiyo ya Huduma za Habari, 2016  kinaueleza uchochezi kama ;

( a ) Andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya   kujenga chuki kati ya watu na watu au watu na  serikali .

( b ) Andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya   kuvunja amani kwa namna yoyote.

( c ) Andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya   kuleta uasi (disaffection) /kutokubalika/kutoridhishwa  kwa/dhidi/na   mamlaka yoyote  ya  serikali .

( d ) Andiko, chapisho , sauti au video yenye nia ovu ya  kuleta taharuki, sintofahamu,mshituko katika jamii.

2.   UKIFANYA  HAYA   UTASHITAKIWA KWA UCHOCHEZI.      
Ni kutoka kifungu  cha 53 cha sheria hiyo ya Huduma za Habari ,2016 .

( a)  Kuuza  andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  nawe  muuzaji  utashitakiwa.

( b ) Kutangaza  tu  kuwa  utauza(offer to  sale)  andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  nawe  mtangaza kuuza  utashitakiwa. Kutangaza kuuza  ni  hujauza  ila unatangaza tu kuwa  utauza pengine  baadae .

(c ) Kusambaza andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  nawe  msambazaji  utashitakiwa.

( d ) Kuingiza  nchini ( import)  andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  nawe  muingizaji  utashitakiwa.

( e ) Kumiliki tu  andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  nawe mmiliki  utashitakiwa. Kwa  mfano  ukikutwa  na  gazeti  lenye  habari  ya  uchochezi  bila  sababu  za  msingi unaweza  kushitakiwa  mahakamani. Pia  audio  au  video  hizi  tunazohifadhi kwenye simu zetu , laptop  na  kwingineko  ikiwa zina viashiria vya uchochezi  ni  kosa  la  kufikishwa  mahakamani ukikutwa nazo.

( f ) Kutoa kopi ( reproducing) andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  nawe  mtoa kopi   utashitakiwa. Mtoa  kopi  anayeshitakiwa  hapa  ni  yule mwenye au mfanyakazi wa  stationery aliyetoa kopi.

( g) Kuzalisha (printing) andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi, wewe  mzalishaji   utashitakiwa. Ni  hadhari  kwa  wale  wenye  factory  za  kuprint  machapisho  kwenye  karatasi, matangazo  na  kwenye  nguo hasa tisheti.

( h ) Kutangaza( advertise) andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  nawe  mtangazaji  utashitakiwa.Mfano huyu ameprint tisheti na wewe umevaa  tisheti  hiyo. Kuvaa ni  kutangaza hivyo  nawe utashitakiwa kwa uchochezi.

( i ) Kujaribu  tu ( attempt) kuandika, kuchapisha , kutengeneza  sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  ni kosa  na   utashitakiwa. Hapa  ni  umejaribu  tu  na  wala  hujafanya.

( j ) Kufanya  maandalizi tu(preparation) ya kuandika, kuchapisha , kutengeneza  sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  ni kosa  na   utashitakiwa. Hapa  ni  maandalizi  tu  na  wala  hujafanya.

( k ) Kula njama( conspiracy)  Kutoa tamko ,kuchapisha na kutangaza andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  ni kosa  na   utashitakiwa. Njama ni mipango kabla ya kutenda kosa lenyewe.

( l ) Kutamka,kuandika,na kuchora   andiko, chapisho , sauti au video yenye  viashiria  vya  uchochezi  ni kosa  na   utashitakiwa.Hii ndiyo inayojulikana kwa wengi.

3.   ADHABU  ZA UCHOCHEZI.

Zinatoka kifungu  cha 53 sheria hiyo ya Huduma za Habari,2016.

( a ) Kunyang”anywa  na  kuchukuliwa  vifaa  vilivyotumika  katika  kuchapisha, kutangaza,kusambaza au kuandaa  andiko, chapisho , sauti au video   ya uchochezi.

( b ) Kukuzuia kutangaza,  kuchapisha  andiko, sauti au video nk, kwa muda fulani.

( c ) Kifungo jela kisichopungua   miaka 3 na kisichozidi  miaka 20.  Utafungwa kipindi  chochote humo katikati  kutegemea na kosa  ulilotenda kati  ya  hayo  juu katika 2.

( c ) Faini  inayoanzia milioni 2 hadi milioni 20 .  Utatozwa faini yoyote humo katikati  kutegemea na kosa  ulilotenda kati  ya  hayo  juu katika 2.

( d ) Adhabu  zote  katika a,b na c, yaani  utafungiwa, vifaa vyako vitachukuliwa, utalipa  faini  na utatumikia kifungo.
Jihadhari, Chukua hatua.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com






0 comments:

Post a Comment