Wednesday 10 January 2018

ADHABU YA KIFUNGO KISICHOPUNGUA MIEZI 6 KWA KUTOTOA MATUNZO YA MTOTO.

Image result for MTOTO

NA  BASHIR  YAKUB -

Wako  watu  bado wanalichukulia suala  la  kutoa  mahitaji  kwa  mtoto  kama  suala  la  madai  ya  kawaida.  Wanadhani  ni  suala  ambalo  linamhusu  mama  mzazi  na  baba  mzazi basi  wao  kama  wao tu.

Kwa  maana  ni  suala  la kuzungumza  tu  na likaisha  kwa  maelewano  yoyote yale. Kama  bado  una  mtazamo wa aina hii  juu  ya  suala  hili  basi  unahitaji kubadilika.
Kama  hutabadilika  basi  subiri  hapohapo ili sheria  mpya  ya  mtoto  ikubadilishe. Suala  la mahitaji ya  mtoto  ni suala  ambalo  lina  misingi  yake  kisheria . Si  suala  ambalo  umeachiwa uamue  unavyotaka  kwakuwa  wewe  ndiye mwenye mtoto.

Moja  ya  msingi  wa  suala  hili  ni  kuwa  hakuna  kusema  sina.  Huwezi  kutakiwa kutoa mahitaji  ya mtoto  ukasema sina kama si mgonjwa asiyejiweza ama vinginevyo.

Pili,  hata  ukitakiwa  kutoa  ni  wajibu  kutoa  kile ambacho  kwa  akili  ya  kawaida kitamwezesha  mtoto  kuishi  kama  binadamu. Hautatoa  chini  ya  kiwango  cha ubinadamu.   Ndio  maana  nikasema  suala  hili  sio  la  kuisha  kwa  namna  yoyote  tu  ambayo  wewe  unafikiria.

Juu  ya  hilo  suala la  matunzo  ya  mtoto  sio suala  la  kupelekana  tu  ustawi  wa jamii  au  pengine  mahakamani   na  kupewa  amri  ya  kulipa  tu  basi. Ni  kweli  ustawi  wa jamii  utapelekwa,  na  mahakamani  utapelekwa  ila  ni  kuwa  haiishii  tu  hapo.  

Zipo  adhabu  za  kisheria  ambazo  waweza  kupata  kwa kutotoa  tu  mahitaji  ya  mtoto. 
   
ADHABU.

Kifungu  cha  51 ( b ) cha  Sheria  ya  Mtoto  kimetoa  adhabu   kwa  yule anayeshindwa  kutoa  mahitaji  kwa  ajili  ya  mtoto  kuishi  na kwa  ajili  ya  maendeleo  yake. Kifungu  hiki  kinatofautisha  kati  ya  mahitaji  kwa  ajili  ya  mtoto  kuishi(necessities for survival)  na  mahitaji  kwa  ajili  ya  maendeleo ya mtoto (necessities for development).

Mahitaji  kwa  ajili  ya mtoto kuishi  ni  kama chakula, matibabu, makazi,mavazi nk,  na  mahitaji  kwa  ajili  ya maendeleo   zaidi  ni  elimu/shule. Ili  uwe  salama  yote  mawili  ni  lazima  yapatikane.. Hii  ni  kutokana  na  kifungu  hiki.

Aidha, kifungu  kimetoa adhabu  za  aina  tatu  kwa  mtu  atakayeshindwa  kutoa  hayo  mahitaji  kwa  mtoto.          

Kwanza , ni  adhabu  ya  faini. Kifungu  hiki  kinaainisha  faini  ya  fedha  taslimu  isiyopungua Tshs.  laki  tano  na isiyozidi  Tshs.  milioni  tano. Kwahiyo  humo katikati  unaweza  kuambiwa kulipa  milioni 3, 4, 2, au  laki 7, 8,9 nk.  Kumbuka hii ni faini  na sio  matunzo  unayotakiwa  kutoa. Ni  penalti. Ni       adhabu  ya  ukorofi.

Kwa  maana  ukilipa  hii   bado  itatolewa  amri  nyingine  ya kutoa  mahitaji  kama  inavyostahili.

Pili, ni  kifungo  jela  kisichopungua  miezi  6 na kisichozidi  miaka  3. Humo  katikati  waweza  kufungwa  miezi 7,8,9,10, au mwaka  1 ,2 au 3. Kumbuka  kufungwa  sio  mbadala  wa kutoa mahitaji  ya  mtoto. Utafungwa  na  ukitoka  huko jukumu  la  kutoa  mahitaji  linabaki  palepale.

Kifungu  cha  166  cha  Kanuni  za  adhabu  pia  kimezungumzia tendo  la  kutotoa  mahitaji  ya  mtoto  kama  kosa  la  jinai.

Tatu, ni  adhabu  ya  vyote  viwili yaani  kifungo  pamoja  na  faini. Jela  utaenda  na  faini  utatoa. Hii  nayo  sio  mbadala  wa  mahitaji  ya  mtoto. Utatumikia         adhabu  zote na mahitaji  ya  mtoto  nayo utatoa.

Basi  kumbe si  vyema  kulichukulia  mzaha  jambo  hili  kwani  linaweza  kuathiri  mustakabali  wako  mzima  wa  maisha.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI  WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment